NAIBU Spika, Job Ndugai ametetea uamuzi wake wa kuagiza kutolewa ndani 
ya ukumbi wa Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
 akisema alikuwa sahihi.
Mabishano hayo ambayo yalisababisha kuibuka kwa vurugu bungeni yalitokea
 mwishoni mwa wiki, muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu, 
ambapo kiongozi huyo wa Bunge aliruhusu mjadala kuhusu Muswada wa 
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uendelee.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe alisimama kutaka kutoa ufafanuzi juu ya 
mjadala huo, lakini Ndugai alimzima na kumtaka kukaa chini, jambo ambalo
 halikumfurahisha Mbowe na kumfanya agomee agizo lake.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Ndugai alitumia muda 
mwingi kutetea uamuzi wake na kukosoa hoja za watu wanaompinga juu ya 
uamuzi wake huo.
Ndugai alisema katika kikao hicho, Mbowe alifanya jeuri kubishana na 
kiti na kueleza kuwa kanuni za Bunge zinasema hakuna mbunge yeyote 
atakayesimama kuzungumza bila kuruhusiwa na kwamba uamuzi wa kiti ndiyo 
wa mwisho.
Ndugai alisema wanaomtuhumu kwamba hakutenda haki kumuamuru Mbowe akae chini, wanafanya hivyo kwa vile hawajui kanuni za Bunge.
Ndugai alisema kwa mujibu wa kanuni, ni Rais wa Jamhuri pekee ndiye 
anayeruhusiwa kulihutubia Bunge kwa wakati anaoona yeye unafaa, lakini 
si mbunge.
“Hata rais mwenyewe ni lazima amwandikie barua spika, huu ndiyo 
utaratibu lakini si mbunge au waziri anayeruhusiwa kusimama kwa wakati 
anaoutaka yeye kuzungumza akaruhusiwa, ni lazima ataomba ruhusa kwa 
Spika na kama ipo nafasi ya kufanya hivyo Spika atamruhusu, kama haipo 
hataruhusiwa.
Alipoulizwa kwamba haoni kama alivunja kanuni kwa kumzuia Kiongozi wa 
Upinzani bungeni wakati kanuni za mabunge ya Jumuiya ya Madola zinatoa 
upendeleo kwa kiongozi huyo na waziri mkuu ndani ya Bunge, Ndugai 
alisema:
“Katika vikao vya Bunge, uamuzi wowote wa Spika unakuwa wa mwisho na hauwezi kupingwa na mbunge au waziri yeyote.
“Mbowe nilimuomba kwa heshima sana atupishe kwanza, nilimuelekeza karibu mara tatu…lakini mtu mzima anavunja utaratibu.
“Huyu Mbowe amejivunjia heshima mwenyewe, hata kanisani anayeendesha 
ibada ni mtu mmoja tu, na wengine wanapaswa kufuata utaratibu.
“Kwanza Mbowe alijitoa mwenyewe kwenye orodha kwa maandishi na ninayo 
hapa.... yeye na Halima Mdee, sasa alisimama kufanya nini kama sio 
ujeuri?
“Kanuni anazijua mimi ningemruhusu tu, lakini kwa ujeuri hakufanya 
hivyo. Kuna taratibu za bunge, mbunge anakaa chini pale Spika 
anaposimama na wasome kanuni, sasa hapo mjeuri ni nani?
“Tujifunze kanuni haiwezekani mtu yeyote asimame saa yoyote, kila mmoja 
hawezi kufanya anavyotaka, kuna taratibu zake, kiti kikimuona atapewa 
nafasi kama ipo na iwapo kiti kikiridhika,” alisema Naibu Spika.
Awatetea askari wa Bunge
Akizungumzia hatua ya kuwaamuru askari wa bunge kuingia ndani ya ukumbi 
wa Bunge na kumtoa Kiongozi wa Upinzani, iwapo kama amevunja kanuni, 
Ndugai alisema hakuvunja kanuni na kufafanua kila askari aliye kwenye 
viunga vya bunge yuko chini ya himaya ya kiti.
“Kila askari aliye kwenye eneo la bunge au viunga vya bunge kuanzia 
polisi, usalama wa taifa na wengine wote siwezi kuwataja hapa, hao wote 
wako chini ya bunge ni Sajent at Arms.
“Askari polisi wote unaowaona bungeni wanaletwa na RPC Dodoma na 
wanakuwa chini yetu, hakuna askari aliyetoka nje siku ile…. Ni uongo na 
hawajui kanuni.
“Uamuzi wa kuita wanausalama ndani ya ukumbi ulikuwa ni uamuzi sahihi, 
hakuna askari aliyetoka nje ya bunge,” alisisitiza Ndugai.
Msekwa amuunga mkono Ndugai
Naye Spika Mstaafu aliyeongoza Bunge la nane, Pius Msekwa alimtetea 
Ndugai akisema kuwa haoni kosa lolote lililofanywa na kiongozi huyo wa 
Bunge.
Msekwa ambaye alipata kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), 
alisema ni jambo la kawaida ndani ya Bunge, Spika kumuamuru mbunge au 
waziri kukaa chini pale anapoona inafaa.
“Spika ni sawa na mwenyekiti wa kikao chochote, anayo madaraka ya kuruhusu nani aseme, nani asiseme.
“Tuje bungeni sasa, Ndugai ndiye anayeamua nani aseme, ni sahihi ndiye 
mwenye mamlaka hayo na ni jambo la kawaida kabisa,” alisema Msekwa.
Akitoa uzoefu wake wa bunge alilokuwa akilisimamia, Msekwa alisema 
matukio yanayotokea bungeni sasa yamegubikwa na hisia za ujana zaidi na 
kusisitiza wazee walio nje ya bunge wanatafakari cha kufanya kabla hali 
haijaharibika.
“Sisi yetu macho… lakini kila zama na kitabu chake, hizi ndio zama za 
vijana, wakati wetu haya hayakuwapo…lakini ikifikia hatua ya kutaka 
kuliteketeza bunge lazima tutachukua hatua… lakini dalili sio nzuri,” 
alisema Msekwa.
-Mtanzania 

Post a Comment