Nia ya kuishambulia Syria: Rais Obama amwita Seneta McCain

 
Rais wa Marekani Barack Obama, baada ya kutamka mwishoni mwa wiki ya kuwa atahitaji uungwaji mkono na baraza la Congress kuhusu nia yake ya kushambulia maeneo muhimu nchini Syria ili kuupunguza nguvu na mashambulizi ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad, leo hii imetaarifiwa kuwa Rais Obama amemwalika Ikulu (White House) mpinzani wake wa kisiasa bwana John McCain kwa nia ya kumtaka awahutubie wajumbe wa Congress kwa kuamini kuwa anaweza kuwashawishi wajumbe hao umuhimu wa Marekani kuingilia mzozo unaoendelea nchini Syria.

McCain aliyeshindwa na Obama katika kinyang’anyiro cha kiti cha Urais wa Marakani mwaka 2008, ni Seneta wa jimbo la Arizona kwa sasa na ana heshima yap eke, si tu katika chama chake cha Republican bali pia na anaheshimiwa wananchi wengi kwa kuwa ni askari mstaafu, mpiganaji mateka (POW - Prisoner of War) aliyepigana na kuongoza vikosi vya Marekani vilivyopambana na Vietnam wakati wa nchi hizo zilipokuwa vitani, ameshatamka wazi kuwa ikiwa nia ya Rais Obama si kuangusha utawala wa Assad bali kuupunguza makali tu, basi hatahatashawishi wajumbe wa Congress kuunga mkono nia hiyo.

Baadhi ya wajumbe wa Congress wa vyama vyote vikuu (Republicans na Democrats), watamka wazi kuwa
watamuunga mkono McCain katika hilo. Hiki ni kipindi mbacho kuna mgawanyiko wa wazi baina ya wajumbe na wananchi wote bila kujali mrengo wao.

Juzi kwenye kipindi cha Mac & Gaydos kinachosikika kupitia KTAR 92.3 FM radio ya jijini Phoenix, Arizona, Seneta McCain alialikwa kuzungumza  na katika mambo matatu ya aliyoombwa kuzungumzia (ObamaCare, Immigration na Syria) alibainisha wazi kuwa haoni mantiki ya kuishambulia Syria kwa nia ya kuharibu baadhi ya maeneo muhimu yanayotumiwa na utawala wa Assad na kuondoka, bila ya kuwa na nia madhubuti ya kuuondoa utawala huo.

Itakumbukwa kuwa mwezi Mei mwaka huu, Seneta McCain alisafiri hadi nchini Syria kwa ajili ya kuzuru na kujionea baadhi ya maeneo na hali halisi.

Juzi baadhi ya wananchi waliandamana juzi Jumamosi kupinga nia ya Serikali ya Marekani kutaka kuishambulia Syria. Baadhi yao walitoa maoni kuwa hawaoni ni kwa jinsi gani Marekani inatishiwa moja kwa moja na vita inayoendelea nchini Syria hasa ikizingatiwa kuwa Syria haina historia ya urafiki na Marekani.

 Lakini wapo pia waliounga mkono kupunguzwa nguvu kivita kwa Assad kwa kuwa wanaamini utawala wake ndiyo uliotumia sumu ya sarin katika kuwashambulia raia na kuwaua 1429, miongoni mwao wakiwa watoto zaidi ya mianne. Ama ikiwa nani aliitumia sumu hiyo kati ya Serikali na waasi (rebels) ni vigumu kung’amua na kuthibitisha kwani hata waasi (rebels) wanaosaidiwa vifaa vya vita kutoka sehemu mbalimbali, inawezekana kabisa wakawa walipora sumu hiyo kutoka kwenye maghala ya Serikali na kuitumia na hivyo itaonekana kuwa imetumika na Serikali.

Wapo pia wale wanaotaka Marekani iingilie kati vita inayoendelea Syria kwa sababu za kiutu na kibinadamu tu, kwa lengo la kusaidia kuzuia mauaji zaidi yanayoendelea . Hawa wanaona si vyema kukaa pembeni na kusema hayanihusu wakati wanaokufa ni wanadamu wenzako. Ikiwa una uwezo, basi fanya lolote kuokoa uhai wa wale waliojikuta wamenasa katika vita pasina kutaka lakini hawana namna yoyote ya kujinasua.

Vita inayoendelea nchini Syria ilianza takribani miaka miwili u nusu hivi iliyopita, katika kufuata upepo wa mabadiliko ya kutaka kuwan’goa viongozi na watawala katika ukanda wa nchi za Kiarabu (Arab Spring). Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya laki moja wameshapoteza maisha katika mapigano hayo.

Marekani ilisita kuingilia kati kama ilivyofanya kwenye baadhi ya nchi hizo baada ya kusema kuwa ilipata taarifa zisizo na tashwishi kuwa baadhi ya wanabamabadiliko (waasi/rebels), walikuwa wanachama wa mtandao wa makundi ya kigaidi.

Post a Comment

Previous Post Next Post