TIB toka taasisi ya fedha mpaka Benki ya maendeleo nchini


01
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro (kulika) akikata utepe kuzindua ofisi za Makao Makuu ya Benki ya Maendelea Tanzania (TIB) ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Tawi la benki hiyo Mkoa wa Mbeya iliyofanyika jijini Mbeya jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa TIB, Peter Noni na Mwenyekiti wa Bodi ya TIB, Prof. William Lyakurwa.
02
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Prof. William Lyakurwa (kushoto), akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa ofisi za Makao Makuu ya TIB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Tawi la benki hiyo Mkoa wa Mbeya iliyofanyika jijini Mbeya. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Mkurugenzi Mwezeshaji wa TIB, Peter Noni.
03
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro (katikati) akijaza fomu ili kufunguliwa akaunti ya Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) Tawi la Mbeya, katika hafla ya ufunguzi wa ofisi za Makao Makuu ya TIB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na tawi hilo Mkoa wa Mbeya iliyofanyika jijini humo. wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa TIB, Peter Noni na anayeongea naye ni Mbunge wa Mbozi Masharibi, Godfrey Zambi.
04
Mcheza ngoma akionyesha manjonjo yake kuwaburudisha watu waliohudhuria uzinduzi huo.
05
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro (katikati) akiagana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Peter Noni (kulia), baada ya hafla ya ufunguzi wa ofisi za Makao Makuu ya TIB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Tawi la benki hiyo Mkoani  Mbeya. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TIB, Prof. William Lyakurwa.
.ilianzishwa mwaka 1970 ina takribani miaka 40 kwenye huduma za kifedha
.sasa kuwekeza kwenye miundombinu ya reli, mawasiliano na barabara
.Benki ya wanyonge, mafanikio kichelee, wakulima nao kunufaika
Na Damas Makangale, Moblog 
Baada ya kujiendesha Kwa faida Kwa takribani muongo mmoja, Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) iliyoanzishwa mwaka 1970 Kama Taasisi ya Maendeleo ya fedha, Development Finance Institution (DFI), TIB inakusudia kuanza kuwekeza katika miradi mikubwa yenye kuleta matokeo makubwa na kuendana na kauli mbiu mpya ya Serikali “Matokeo Makubwa sasa” (Big Results Now).
Baada ya kufanya kazi Kama taasisi ya maendeleo ya fedha Kwa miaka 25, TIB ilikuja kubadilishwa na kuwa benki ya uwekezaji (Tanzania Investment Bank) ili kuongeza uwezo wake wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya soko hapa nchini.
TIB lengo lake kuu ni kutoa Fedha na huduma za uwekezaji na maendeleo katika Nyanja mbalimbali kama vile kilimo kupitia dirisha lake maalum la kukopesha wakulima wadogo wadogo (Special Agriculture Window), mikopo kwa wafanyabiashara na watu wa kipato cha chini ili kuweza kuinua maisha yao na kuondokana na umaskini.
Akizungumza kwenye sherehe za uzinduzi wa makao makuu mapya ya benki hiyo kwa kanda za Nyanda za Juu kusini iliyofanyika jijini Mbeya hivi karibuni, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TIB, Ndugu Peter Noni amesema kwamba benki hiyo imejipanga kuwekeza katika miundombinu ya reli, umeme, barabara na mawasiliano.
“TIB ina nia ya dhati kabisa uwekeza katika miundombinu hiyo ili kuisaidia serikali kuongeza kasi ya kuboresha mtandao wa miundombinu ya kiuchumi kama injini ya kukuza Uchumi wa ndani,” amesema.
 “Benki yetu kwa sasa inajipanga kuanza uwekezaji katika miradi mikubwa ya miundombinu ya kiuchumi. Miradi hiyo ni kama vile reli, barabara, umeme na mawasiliano,” amesema Noni.
Noni alinukuliwa akisema kuwa ili kufanikisha azma hiyo, watashirikiana na benki nyingine za maendeleo nje ya nchi ambazo zina ushirikiano na TIB. Akazitaja baadhi ya benki hizo ambazo TIB inakusudia kushirikiana nazo kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu nchini kuwa ni DBSA, IDC, BNDES na CDB.
Amesema kwa kuanzia mwaka wa 2013, Benki ya TIB imejipanga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 379, ambazo zitaiingizia benki hiyo faida isiyopungua shilingi billioni 16 kabla ya kulipa kodi ya Serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TIB, Prof. William Lyakurwa alisema kuwa Baada ya Serikali kuamua kuifufua TIB, imeamuliwa kuwa sasa benki hiyo itajiendesha kwa mfumo wa makampuni tazu yanayotegemeana ndani ya benki hiyo.
Amesema Kampuni ya kwanza itakuwa ni TIB Development Bank Ltd na kampuni ya pili itajulikana kwa jina la TIB Corporate Finance Bank Ltd ambayo itakuwa benki ya kibiashara, mahususi kwa ajili ya wateja wa benki ya maendeleo.
Amesema kuwa kampuni ya tatu itakuwa ni TIB Railimali Ltd ambayo kazi yake itakuwa ni udalali wa hisa za makampuni mbalimbali akisema kuwa mfumo huo unatarajiwa kuboresha ufanisi katika shughuli za kibenki na hivyo kutoa huduma bora kwa wateja wake.
Mgeni Rasmi wa Sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amesema kuwa nia ya Serikali ni kuiwezesha TIB kuwa taasisi imara ambayo italeta chachu ya uwekezaji katika viwanda vya kusindika mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji na miradi mingine ya uzalishaji ili kuwawezesha wananchi kupata masoko ya uhakika ya mazao yao na hivyo kujiongezea kipato.
Amesema kuwa ili wananchi waweze kunufaika na jasho lao litokanalo na  kilimo, ni lazima taifa liachane na mfumo wa kuuza mazao ghafi nje ya nchi badala yake mazao hayo yawe yanasindikwa hapa nchini  kabla ya kuuzwa nje ya nchi ili kuyaongezea thamani.
Amesema kuwa ili kuonyesha mfano, hivi sasa Serikali mkoani Mbeya inaandaa program ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ili kanda hiyo ianze kuzalisha matunda, mboga mboga na maua kwa ajili ya masoko ya mazao hayo nje ya nchi.
Benki ya Maendeleo nchini (TIB) ilizinduliwa upya na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete Novemba 30, 2010.

Post a Comment

Previous Post Next Post