Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar iko
katika harakati za kukifufua upya Kituo cha kupandishia Ngombe
kilichopo katika eneo la Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ili
kirejee katika utaratibu wake wa kutoa huduma bora kwa wafugaji wa
Ngo’mbe wa kisasa hapa Nchini.
Kituo hichoanzishwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 70 na kusitisha huduma zake
kutokana na mabadiliko ya sera ya ufugaji kwa kuachiliwa suala hilo
kuendeshwa na wananchi moja kwa moja.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Zanzibar Dr. Kassim Gharib alieleza hayo wakati wa ziara fupi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika katika eneo
hilo kukagua juhudi zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kukifufua
tena kituo hicho.
Dr. Kassim alimueleza Balozi Seif kwamba
Wizara hiyo imeanza na hatua ya kuzunguusha ukuta eneo hilo ili kuzuia
uvamizi wa ujenzi holela wa nyumba pamoja na uchimbwaji ovyo wa mchanga
uliokuwa ukitishia uchafuzi wa mazingira.
Alisema hatua hiyo itakapokamilika
itatoa fursa kwa wafanyakazi wa Mifugo kuendelea na hatua ya pili ya
upandaji majani kwa ajili ya malisho ya madume ya ng’ombe watakaotumiwa
kutoa mbegu na kuendelea kusambazwa kwa wafugaji kwenye maeneo mbali
mbali nchini.
Dr. Kassim alifahamisha kwamba licha ya
matatizo na changamoto mbali mbali zilizokuwa zikikikabili kituo hicho
lakini bado kinaendelea kutoa huduma za upandishiaji ng’ombe kikiwa na
Madume Sita bora ya kisasa hivi sasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif pia alipata fursa ya kukagua kara kana inayohudumia
matengenezo ya dharura ya vyombo vya moto vya Wizara hiyo ya Mifugo na
Uvuvi iliyopo jirani na kituo hicho.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Post a Comment