Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Baraza
la mawaziri limeendelea kuwashiwa moto bungeni, baada ya Mbunge wa
Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), kulitaka Bunge kuwang’oa mawaziri
walioshindwa kuwajibika.
Aliyasema hayo bungeni juzi jioni wakati
akichangia ripoti za Kamati za Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii,
kwamba udhaifu wa mawaziri umekuwa ukionekana kwenye ripoti za kamati za
bunge.
Aliwashangaa wabunge waliokuwa wakisimama na kutamka hakuna waziri anayejiuzulu.
“Kwa hiyo anaposimama mheshimiwa mbunge anasema
hakuna waziri anayejiuzulu hapa, timu ya mpira inaposhindwa anajiuzulu
kocha ambaye yeye hachezi,” alisema na kuongeza kuwa;
“Ni kawaida kabisa, ustaarabu kama huo
tujifundishe duniani, siyo lazima tuwe tunasukwasukwa, mpaka wasimame
wapinzani waseme ndiyo na sisi tunatekeleza hapana, ikionekana huwezi
(waziri), utoke.”
Alisema kila zinapokuja ripoti za kamati za Bunge na mawaziri kuonekana wizara zao hazijafanya vizuri wawajibike.
“Bahati nzuri mmenipeleka China wenyewe. Kule
hakuna wakati ambapo mbunge anapungua kama wakati wa Bunge. Sisi hapa
mawaziri wanazidi kunenepa, unawaona wanaingia katika Facebook,” alisema
na kuongeza;
“Unapata wapi nafasi ya kuingia kwenye Facebook
wakati Bunge linakutana, ni vichekesho vikubwa sana, vitu vya ajabu
sana. Tumekwenda pale China, tumekuta hakuna wakati unaogopwa na Bunge
kama wakati Bunge linakutana. Waziri anasimamisha wizara yake siku 10
kabla ya Bunge kukutana ili kulipa nafasi Bunge, lakini hapa Bunge
linaendelea unaambiwa waziri yuko ziarani.”
“Tunamsifu hayati Mwalimu kwa kulala vijijini.
Leo kuna waziri gani ambaye anakubali kulala vijijini? Wamepewa magari
mazuri, wanajaziwa mafuta, wanapewa dereva lakini kwenda kwenye kijiji
shida, unawaona kila siku wako Dar es Salaam, sijui wako Iringa Mjini.
Nendeni vijijini mkaone shida za watu, mkitembea wenyewe
mtalia,”alisema.
Aliwataka kutowaonea aibu mawaziri ambao hawatoshi, hata kama ni rafiki zao.
“Tusione aibu hata mtu akiwa rafiki yetu, kama
hatoshi tumwambie atupishe na huu uwe ni utaratibu. Kila Bunge likija
lazima liondoke na waziri mchovu, ndiyo bunge hili
litaheshimika,”alisema na kuongeza;
“Lakini tukianza kutafuta mchawi ni nani alete
majina, hivi kweli nchi hii haijui kuwa kuna watu wameweka hela nje,
mbona tunasema eti lete majina, mnatuletea mambo ya mbwembwe hapa,”
alisema
Post a Comment