Ni Tatu Na Ya Tanganyika Imo



UTEUZI WA UONGOZI
RASIMU hii ambayo ni ndefu kuliko ya awali, madaraka ya Rais hasa ya uteuzi yamepunguzwa kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na kwa baadhi ya vyeo, kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.
Rasimu hiyo yenye ibara 271 ikilinganishwa na ya awali yenye ibara 240 hata hivyo, imesisistiza Rais ndiye mwenye hadhi na heshima ya Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Serikali.
Vile vile imependekeza wabunge wasiwe mawaziri, kuwe na ukomo wa uwakilishi katika Bunge na wapiga kura wawe na madaraka ya kumwajibisha mbunge hata kabla ya kumalizika kwa muhula wake.
Mengine: Ni Spika na Naibu Spika, wasitokane na wabunge au kiongozi wa juu wa chama cha siasa. Uraia wa Jamhuri za Muungano. Rasimu imependekeza kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na kujiandikisha ambao ni wa nchi mmoja.
Imependekeza kuwapo hadhi maalumu kwa watu wenye asili au nasaba ya Tanzania ambao wameacha kuwa raia wa Tanzania kwa kuchukua uraia wa nchi nyingine.
Marufuku kiongozi wa umma kutumia wadhifa, nafasi au madaraka kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa, marafiki au mtu aliye na uhusiano naye wa karibu.
Tume kwa kuzingatia maoni ya wananchi, tofauti na ilivyokuwa katika Rasimu ya Awali, sasa inapendekeza msajili wa Vyama vya Siasa, iwe ni taasisi inayojitegema na isiwe sehemu ya Tume Huru ya Uchaguzi.
Imependekezwa pia, kuwepo Jeshi la Polisi moja na Idara ya Usalama wa Taifa mmoja katika Jamhuri za Muungano za Tanzania.
KIPINDI CHA MPITO
Rasimu inapendekeza muda wa mpito wa miaka minne, kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba mpya hadi Desemba 31, 2018 na kwamba sheria zilizopo sasa zitaendelea kutumika hadi zitakapobadilishwa.
Masuala yaliyopendekezwa yafanyiwe kazi katika kipindi cha mpito ambayo ni pamoja na kutungwa kwa Katiba ya Tanganyika na mgawanyo wa rasilimali baina ya serikali ya Muungano na serikali za nchi washirika.
Mengine ni kufanya maandalizi ya kuendesha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2014. Kuundwa kwa Tume na Taasisi za Kikatiba, zilizoainishwa kwenye Katiba.
Rasimu ya wananchi, akielezea mchakato wa maandalizi wa Rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema tofauti na wasiwasi uliyokuwapo kwa ushiriki wa wananchi wa kawaida, ungekuwa dhaifu. Sura tano za mwanzo za Rasimu zinatokana na mchango mkubwa kutoka kwa wananchi:
“Tume ilipoanza kulikuwa na wasiwasi kwamba ushiriki wa wananchi wa kawaida ungekuwa dhaifu kwa sababu iliaminika kwamba wananchi kwa ujumla wao hawana ujuzi wa Katiba,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Lakini Tume iligundua mapema kwamba wananchi wanajua mambo mengi ambayo ni msingi wa Katiba yoyote. Sura tano za mwanzo wa Rasimu ya Katiba zinatokana na mchango mkubwa kutoka kwa wananchi,”.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, maoni ya wananchi yalihusu misingi ya Taifa, tunu za Taifa, maadili na miiko ya viongozi, dira ya Taifa na haki za binadamu.
Wananchi pia walitoa maoni mazito kuhusu uongozi na utawala wa nchi, ikijumuisha pamoja na nafasi za Wawakilishi wao Bungeni.
Ilikotoka Tume: Rais Kikwete, aliteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Aprili 6, mwaka jana 2012 ikiwa na wajumbe 34 kutoka pande zote mbili za Tanzania, chini ya uenyekiti wa Jaji Warioba. Iliapishwa Aprili 13, 2012 na kuanza kazi rasmi Mei 2, mwaka huo huo.
Sheria ya mabadiliko ya Katiba, ilitoa miezi 18 kwa Tume, kukamilisha kazi yake. Sheria pia ilitoa nafasi kwa Tume kuongezwa muda usiozidi miezi miwili na iliomba muda huo ikakubaliwa kabla ya kukamilisha kazi yake jana, na kuikabidhi kwa Rais.
Chanzo: HabariLeo

Post a Comment

Previous Post Next Post