
MWANASHERIA
Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, amewataka Watanzania, hususan wanachama wa
chama hicho kutopoteza muda kujadili suala la baadhi ya wanachama
waliopatikana na makosa ya usaliti na utovu wa maadili ndani ya chama
hicho, kisha kuchukuliwa hatua bali wajikite kukiimarisha chama hicho
kila mahali na kujadili masuala yanayowahusu wananchi.
Lissu ambaye
aliambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA),
John Heche, alisema kuwa taifa linakabiliwa na masuala mengi ambayo
yanahitaji umakini wa kila mwanachama wa chama hicho akitolea mfano wa
kujadili maudhui ya Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, ili taifa lipate
katiba mpya na bora.
Mwanasheria
huyo pia aliwaambia wananchi wa maeneo hayo kwamba kutokana na uongozi
mbovu, rasilimali za Tanzania zimeendelea kutafunwa na watu wachache kwa
kupitia sera za ubinafsishaji ambazo zimetumiwa na watawala kama mianya
ya kujigawia mali kwa mgongo wa uwekezaji, huku wazawa wengi wakiwa
hawana la kufanya.
Alitumia
mikutano hiyo kusoma taarifa za kila mwaka wa bajeti za serikali ambazo
zinaonesha mgawo wa fedha wa kila eneo kwa sekta hususan zinazohusu
huduma za jamii, akisema wananchi wengi hawajui kwa sababu viongozi wao
hawataki wajue.
Kwa upande
wake, John Heche aliwaambia wananchi kwamba bila kuupiga vita na
kuutokomeza ufisadi ambao unaendelea kulitafuna taifa akidai unalelewa
na Serikali ya CCM, wananchi hawatapata matumaini na maendeleo
wanayoyahitaji.
Alisema kuwa
hata ujangili unaoendelea kwa kasi kubwa kiasi cha kutia shakani uwepo
wa tembo katika mbunga za wanyama ni matokeo ya ufisadi ambao CHADEMA
kimekuwa kikihamasisha umma kuupiga vita kwa nguvu zote kwa sababu
utaliangamiza taifa.
Alisema kuwa
pamoja na Tanzania kuwa moja ya mataifa machache yaliyobarikiwa kila
aina ya utajiri wa rasilimali, wananchi wake wanazidi kuwa maskini huku
viongozi wao wakitembea nje ya nchi kuomba vitu vidogo kama vyandarua,
wakati taifa lina uwezo wa kuhudumia watu wake kwa vitu kama hivyo
endapo kungelikuwa na viongozi bora wanaojali watu wao.
“Ninyi
wananchi mnajua kwamba viongozi wa Serikali ya CCM wanakwenda karibu
kila siku Ulaya kutembeza bakuli la kuomba misaada, lakini misaada
wanayoomba si ile ambayo inaweza kutusaidia kama taifa kuondokana na
matatizo yetu ya umaskini, ujinga, maradhi na sasa ufisadi, wanakwenda
Ulaya kuomba vyandarua wakiwa wanarudi wanapishana angani na Wazungu
wamebeba dhahabu, almasi na vitu vingine vya thamani kutoka Tanzania,”
alisema Heche.
Post a Comment