Na Rajab Ramah, Nairobi
Utengaji wa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) katika utekelezaji wa mipango ya muungano kunaweza kusababisha
kuvunjika kwa jitihada za muungano kamili wa kanda, wachambuzi wasema.
Wakuu wa usalama kutoka Uganda, Kenya na Rwanda walikutana mjini Kigali,
Rwanda mapema mwezi huu ambapo walitia saini mkataba wa usalama na
ulinzi kurahisisha harakati za raia na watalii za kutoka sehemu moja
kwenda nyingine katika kanda unaolenga kuongeza biashara kati ya mpaka
wa nchi moja na nyingine.
Mkutano huo wa tarehe 9 Januari wa maofisa wa jeshi, polisi, upelelezi
na uhamiaji umefuatia uanzishwaji wa visa ya pamoja ya utalii na nchi
hizo tatu ambayo ilianza rasmi tarehe 1 Januari.
Hii ilikuwa ni mara ya nne viongozi hao wa Uganda, Kenya na Rwanda
kufanya makubaliano kuhusu masuala ya muungano pasipo ushiriki wa
Tanzania na Burundi, ambazo pia ni mwanachama wa muungano huo wa nchi
tano.
Tanzania na Burundi hazikuhudhuria mkutano uliofanyika Uganda na Kenya
mwezi Agosti mwaka uliopita, au mkutano uliofanyika huko Kigali mwezi
Oktoba 2013.
Tanzania ililalamika kutengwa katika mazungumzo, na rais Jakaya Kikwete
alisema, "Wameunda umoja wa hiari. Nani ambaye hana hiari?"
Kuvunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki siku zijazo?
Katika Mkutano wake wa Kawaida wa 15 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa
Wakuu wa Nchi huko Kampala mwezi Novemba mwaka jana, viongozi walisema
watajitolea kufanya kazi pamoja, lakini wachambuzi wa mambo wanasema
kuwa hakuna uwezekano wa kutokea hilo.
"Nina wasiwasi kama wakuu wa nchi tatu -- Museveni, Kenyatta na Kagame
-- walikuwa makini wakati wa mkutano kuhusu ahadi yao ya kusaidia
wanachama wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika shughuli zao kwa
sababu kinyume na azimio lao walikuwa Rwanda peke yao," alisema Rais wa
Chama cha Sheria Afrika Mashariki (EALS) James Aggrey Mwamu. "Huo ni
uthibitisho wa kutosha kwamba wanajitoa kufanya kazi bila ya Tanzania na
Burundi."
Makubaliano ya pande tatu ni tishio kwa mtangamano wa kanda kwa kuwa yanazitenga kwa makusudi Tanzania na Burundi, alisema.
"Kile tunachokiona kinachoitwa hatua ya 'muungano wa hiari' ni ujengaji
wa wingu la wasiwasi na jambo baya miongoni mwa nchi wanachama ambavyo
vinaweza kuchochea mgawanyiko na kupanda mbegu ya kutoelewana
ikisababisha kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kama ilivyofanya
mwaka 1977," Mwamu aliiambia Sabahi. "Kwetu sisi, 'muungano huo wa
hiari' haukubaliki kwa kuwa ni kinyume na mkataba ambao uliiunganisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki."
Kushindwa kwa nchi zote wanachama kuungana katika mipango ya pamoja
kisiasa na kimaendeleo ni sawa na kuiacha kanda isambaratike, alisema.
"Kwa sasa kanda inakabiliwa na changamoto nyingi zikianzia katika kukosa
utulivu wa kisiasa, uharamia na ugaidi, kwa hiyo, [hatutarajii]
kuwatenga wengine na kuhisi kwamba tutafanikiwa," Mwamu alisema,
akiwaomba viongozi wa kanda kushauriana mara kwa mara ili wasiendelee
kufanya makosa.
Mgawanyiko wadhoofisha mshikamano wa kanda
Ingawa kujumuika pamoja kunachukuliwa kuwa bora na viongozi wa kanda
walio wengi, Tanzania imepata sifa ya kutoharakisha masuala ya
mtangamano na Burundi inachukuliwa kama nchi isiyo na chochote cha
kutoa, alisema George Omondi, mwandishi wa habari wa gazeti la The East
African anayeandika kuhusu masuala ya kanda.
"Tanzania imekuwa ikiibua masuala ya umiliki wa ardhi, shirikisho la
kisiasa na uraia ambavyo inataka mwongozo ulio wazi, lakini washirika
wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, badala ya kukaa chini kutatua
hili, wanaliona kama dalili ya kuleta mvutano," Omondi aliiambia Sabahi.
"Wamechagua njia iliyo rahisi zaidi, ambayo ni kujitenga, [na] ambayo
sio sahihi."
"Burundi inaonekana kama mshirika masikini ambaye hana thamani katika
mtangamano hivyo wanachagua kuipuuza wakisahau kwamba nchi ina watu
zaidi ya milioni 9 ambayo inaweza kwa urahisi kuwa soko kwa bidhaa za
Kenya, Uganda au hata Rwanda," alisema.
Manu Chandaria, mfanyabiashara wa Kenya na mwenyekiti wa Kundi la
Comcraft ambalo linazalisha bidhaa za chuma, plastiki na aluminiamu
katika Afrika Mashariki, alisema mgawanyiko wa hivi karibuni
utadhoofisha ufanikishaji wa malengo ya mtangamano wa kanda yaliyowekwa.
"Sisi katika sekta ya biashara tunahisi kuwa kuvunjika tena au kujitenga
kutaanzisha vikwazo vipya katika biashara," Chandaria aliiambia Sabahi.
"Kila nchi inaanzisha na kutumia mifumo yake tofauti ya biashara …
itakuwa ni pigo kwa biashara huria ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo
muda wote huu."
Ili kufurahia kikamilifu faida inayotokana na umoja wa forodha na
itifaki ya soko la pamoja, na kukamilisha uanzishaji wa fedha ya pamoja
na shirikisho la kisiasa, alisema viongozi wa kanda hiyo wanapaswa
kuvumiliana na kuwa tayari kushughulikia masuala ya msingi.
Kuiacha nchi moja nyuma kutazuia mchakato mzima, alisema.
"Tunachokiona ni kutokuwa na uvumilivu kwa baadhi ya viongozi. Hatuwezi
kudhani kwamba tutaendelea kwa kuwaacha wale walioibua maswali kuhusu
mchakato," alisema Chandaria. "Wangepaswa kukaa na kujaribu kutatua
matatizo yaliyoibuliwa na Tanzania badala ya kuamua kuendelea."
EAC imeungana na ni yenye malengo, asema Kandie
Kwa upande wake, Katibu wa Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki Kenya
Phyllis Kandie alipinga hisia za kujitenga, akisema muungani wa EAC
utafanyika kama ilivyopangwa.
"Sitapenda kuingizwa katika mjadala huo 'muungano wa hiyari', lakini
ninachoweza kukueleza ni kwamba sisi ni muungano kama tulivyokuwa awali
na kwamba tuna malengo ya kufanikisha misingi ya EAC," Kandie aliiambia
Sabahi.
Katika kujibu swali la iwapo mikutano ya nchi hizo tatu zinapingana na
mkataba wa EAC, alisema, "Uganda, Kenya na Rwanda wanatumia utengano wa
nchi kadhaa ambayo imeelezwa katika mkataba."
Utengano huo ni msingi katika Kifungu cha 7 cha Mkataba wa EAC, ambacho
kinaruhusu maendeleo katika umoja miongoni mwa kundi dogo la wajumbe
katika muungano mkubwa katika maeneo tofauti na katika kasi tofauti.
Hata hivyo, chini ya kifungu hicho, nchi wanachama ambazo zinataka
kuendeleza kwa haraka bado zinatakiwa kuwafahamisha wajumbe wengine,
ambalo halijafanyika katika suala hili, kwa mujibu wa Mwamu.
Jaribio la kumpata Katibu Mkuu wa EAC Richard Sezibera kwa ajili ya maoni halikufaulu.

Post a Comment