Na Hadija Jumanne, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakazi sita wa
Dar es Salaam maarufu Mbwa Mwitu au waanzilishi wa kundi la Watoto wa
Mbwa, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la
unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga aliwataja
washtakiwa hao kuwa ni Sijali Abdallah (19), Sadick Mpambe (25) maarufu
Chitemo na Balozi Inasio (19) wote wakazi wa Kiwalani.
Wengine ni Shahibu Japhary (30) maarufu Cardinal
Pengo mkazi wa Yombo Kwa Limboa, Mussa Muhunzi (31) maarufu Matikiti na
mkazi wa Kiwalani Kijiwesamli na Zegamba Kihongo (20) mkazi wa Kiwalani
Migombani.
Katuga alidai mahakamani hapo kuwa, washtakiwa kwa
pamoja walitenda kosa hilo Januari Mosi mwaka huu eneo la Yombo
Kiwalani, Wilaya ya Ilala.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa kwa
pamoja siku ya tukio waliiba Sh150,000 taslimu na simu moja ya mkononi,
mali ya Juma Fungo.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa,
washtakiwa kwa pamoja kabla na baada ya kufanya unyang’anyi huo
wanadaiwa walimtishia mlalamikaji kwa panga na kisu ili waweze kupata
vitu hivyo kwa urahisi.
Washtakiwa walikana shtaka na Hakimu Wilberforce Luhwago aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 31, mwaka huu itakapotajwa tena.
Washtakiwa walirudishwa rumande kutokana na shtaka
linalowakabili la unyang’anyi wa kutumia silaha kutokuwa na dhamana
hadi kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Post a Comment