THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
|
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR
ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA UMMA
Tusaidie
kufunga masoko ya pembe za tembo duniani – Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Jumuiya ya
Kimataifa kusaidia kukomesha na kufunga masoko ya pembe za tembo na faru kama
moja ya njia za kukomesha mauaji na biashara haramu ya wanyapori hawa.
Akizungumza asubuhi
ya leo, Alhamisi, Februari 13, 2014 kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kukabiliana
na Ujangili na Biashara Haramu ya Pembe za Tembo kwenye Jumba la Lancaster
mjini London, Rais Kikwete amesema kuwa bila kufunga masoko hayo kazi ya
kudhibiti ujangili na mauaji ya wanyamapori hao itakuwa ngumu.
Rais Kikwete alikuwa
mmoja wa viongozi wa Afrika ambao walizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo
uliohudhuriwa na wakuu wa Serikali na nchi pamoja na wawakilishi wa nchi 60
duniani. Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Uingereza kwa ombi la Mtoto wa
Malkia wa Uingereza, Prince Charles.
Mbali na Rais
Kikwete, viongozi wengine wa Afrika walioshiriki Mkutano huo na kuzungumza ni
pamoja na Rais wa Botswana Mheshimiwa Jenerali Khama Iam Khama, Rais wa Gabon
Mheshimiwa Ali Omar Bongo na Rais wa Chad Mheshimiwa Idrissa Deby. Ethiopia
iliwakilishwa na Waziri.
Rais Kikwete
amewaambia mamia ya wajumbe wa Mkutano huo: “Mwisho, nataka kuiomba Jumuiya
ya Kimataifa kuweka msimamo na kusaidia kukomesha biashara ya pembe za tembo na
faru duniani. Kama hili litafanyika tembo na faru watakuwa salama.”
Ameongeza: “Wakati
CITES ilipopiga marufuku biashara ya pembe za tembo mwaka 1989, hali hiyo
ilisaidia kuongezeka kwa idadi ya tembo duniani. Naamini kuwa kama biashara
hiyo itapigwa marufuku tena leo, matokeo yatakuwa yale yale. Maisha ya tembo na
faru wengi yataokolewa na hatutakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi.”
Rais pia ametoa
mapendekezo mengine makuu wanne kama njia ya kukabiliana na ujangili na
biashara haramu ya pembe za ndovu ikiwa ni pamoja na ahadi kwamba Serikali
itaendelea kuongeza nguvukazi ya maofisa na askari wanyamapori na kuhakikisha
kuwa maofisa na askari hao wanapata mafunzo mwafaka ya kuifanya kazi hiyo.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13 Februari, 2014

Post a Comment