Bado juhudi zinaendelea katika kuisaka ndege ya Malaysia
aina ya Boeing 777 na habari mpya kuhusu kinachoendelea zinazidi
kutolewa licha ya ukweli kuwa bado ni mtihani mkubwa kwa nchi
zilizoingia kwenye msako huo.
Chanzo cha karibu na vikosi vinavyofanya msako wa ndege hiyo
kimeiambia CNN kuwa radar ya kijeshi imeonesha kuwa ndege hiyo ilibadili
muelekeo na kukata kona kali katika eneo la kusini mwa bahari ya China
wakati ikielekea Malacca.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa imeonekana kuwa baada ya kupiga kona hiyo
ilishuka chini na iliruka umbali wa futi 12,000 kabla haijatoweka
kabisa kwenye radar.
Inasadikika kuwa ndege hiyo ilipiga kona kwa kukusudia na sio
kutokana na tatizo kwa kuwa kulikuwa na kila uwezekano wa marubani wa
ndege hiyo kuonesha ishara ya hatari.
Hata hivyo baadhi ya wachunguzi wanasema bado inawezekana marubani
walishindwa kabisa kufanya mawasiliano kutokana na hali ilivyokuwa.
Katika hatua nyingine, imeripotiwa kuwa kikosi cha China kimeona vitu
vinavyosadikika kuwa mabaki ya ndege hiyo kusini mwa bahari ya Hindi.
Shirika la habari la ABC America, limeripoti kuwa kikosi hicho
kimeeleza kuwa kimeona vitu viwili vikubwa vyenye rangi nyeupe vikiwa
vinaelea baharini.
Vitu hivyo vimeonekana kuwa kuwa na rangi nyeupe na vilishuhudiwa pia
na askari mmoja wa Australia aliyekuwa katika ndege ya kikosi hicho cha
China.
Ni zaidi ya siku 16 sasa tangu ndege hiyo ipotee ikiwa na watu 239 na hadi sasa haijafahamika chanzo cha kupotea kwa ndege hiyo.
Post a Comment