HUYU NDIYE KIGOGO SERIKALINI ANAYEVURUGA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA


Wakati Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ikifanya kila linalowezekana kuhakikisha inapambana kwa dhati na biashara haramu ya dawa za kulevya, baadhi ya vigogo serikalini wametajwa kutaka kudhoofisha juhudi hizo kwa kukumbatia watuhumiwa waliokamatwa.

Mmoja wa vigogo hao anayefanya kazi katika wizara nyeti, ametajwa 'kumpigania' bilionea aliyekamatwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam akituhumiwa kuhusika na shehena ya kilo 210 za dawa za kulevya aina ya heroin zinazokisiwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 10 ambazo zilikamatwa nchini mwaka 2012 mkoani Lindi.

Tayari bilionea huyo, Ali Khatib Haji 'Shikuba' ameshafunguliwa mashitaka, kesi yake ikiunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Lindi.

Kwa mara ya kwanza alipandishwa kizimbani Machi 13 mwaka huu akiunganishwa na watuhumiwa wengine, Maureen Liyumba, Othman Mohammed Nyamvi au maarufu kwa jina la Ismail Adam na Upendo Mohammed Cheusi ambaye kwa sasa ni marehemu. 

Kwa mara ya pili wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kesho mbele ya Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Lindi, Allu Nzowa.

Habari za uhakika ambazo mwandishi amezipata zinasema tangu kukamatwa kwa Shikuba, kigogo huyo amekuwa akihaha kutaka kumnusuru mfanyabiashara huyo maarufu dhidi ya kesi inayomkabili.

Kukamatwa kwa Shikuba kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa.

"Ni kweli tumemkamata. Juhudi zetu zimefanikiwa kukamata mmoja wa watu wazito wanaohusishwa na biashara hii," alisema.

Ingawa `mzigo' anaohusishwa nao Shikuba ulikamatwa mwaka 2012, inaelezwa hakukamatwa kutokana na mfanyabiashara huyo kuwa mafichoni nchini Afrika Kusini na kwamba akiwa huko, alitumia hila na kupata hati nyingine ya kusafiria iliyotolewa Februari 28, mwaka huu, hivyo kurejea nchini alikokumbana na vijana wa Nzowa mara baada ya kutua kwa ndege ya shirika la Ndege la Afrika Kusini, South African Airways.

Mara baada ya kumkamatwa, alisafirishwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi hadi mkoani Lindi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali kupitia kikosi cha kudhibiti dawa za kulevya kimekuwa kikifanya jitihada kubwa za kupambana na wahusika wa dawa za kulevya, ikinasa wengi katika maeneo mbalimbali, kuanzia viwanja vya ndege, hadi kwenye vyombo vya usafiri wa majini, mfano ukiwa ni shehena iliyokamatwa Lindi na pia nyingine ya heroine yenye uzito wa kilo 280 iliyokamatwa hivi karibuni katika bahari ya Hindi, kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Post a Comment

Previous Post Next Post