Godfrey Mgimwa na Robby Mgimwa wakionesha hati yao ya ubunge baada ya kukabidhiwa leo
Mbunge mteule wa jimbo la Kalenga Bw Mgimwa akionyesha dole
Sehemu ya msafara wake
Boda boda nao walikuwepo
AKIWA ameambatana na mkewe, Robby Mgimwa, Godfrey Mgimwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jana alitangazwa mshindi wa ubunge katika uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga baada ya kuvibwaga kwa kura za kishindo vyama vingine viwili vilivyoshiriki uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili ya Machi 16, mwaka huu, Mgimwa alizoa kura 22, 962 ambazo ni sawa na asilimia 79.32 dhidi ya kura 5,853 sawa na asilimia 20 alizopata Grace Tendega wa Chadema na kura 150 sawa na asilimia 0.52 alizopata Richard Minja wa Chausta.
Msimamizi wa uchaguzi huo Pudenciana Kisaka ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa jana alimkabidhi Mgimwa hati yake ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Akizungumza na wanahabari baadaye Mgimwa alisema anazikumbuka ahadi zote alizotoa kwa wananchi wa jimbo hilo wakati wa kampeni zake na anajipanga kutekeleza moja baada ya nyingine.
“Kama mnavyojua nyingi ya ahadi hizo zitatekelezwa kupitia Ilani yetu ya CCM; nachowahakikishia wananchi wangu wawe na imani kwani mambo yatatekelezwa,” alisema huku akiwashukuru wapiga kura wa jimbo hilo kwa kumpa ushindi wa kishindo dhidi ya wapinzani wake.
Pamoja na Chadema kuleta wabunge wake wote siku tatu kabla ya uchaguzi huo na kutumia chopa kwenye kampeni zake kabla ya kuitumia kulinda kura siku ya uchaguzi, Mgimwa alimgaragaza mgombea wa Chadema hata katika kata zilizokuwa zikielezwa kuwa ni ngome ya chama hicho.
Kata hizo ni pamoja na Ifunda ambayo Mgimwa alipata jumla ya kura 1,627 dhidi ya 601 alizopata mgombea wa CCM na 13 za mgombea wa Chausta.
Nyingine ni Nzihi ambayo CCM ilipataa kura 1,793 dhidi ya 606 za Chadema na saba za Chausta.
Katika kata ya Magulilwa ambako mgombea wa Chadema ndiko anakotokea, Mgimwa alifanya vizuri zaidi kwa kupata kura 2,065 dhidi ya kura 549 za Chadema.
Matokeo ynayofana na hayo yalitokea pia katika kata zingine zote za jimbo hilo; wakati Mgimwa akipata kati ya kura 1,500 na 3,000, mgombea wa Chadema alipata kati ya kura 200 na 700 tu.
Grace Tendega
Post a Comment