NESI ANASWA AKIFANYA UFIRAUNI HOSPITALI. HATARI SANA


Nesi Maria (kushoto) mara baada ya kunaswa na OFM.

MARA nyingi manesi wamekuwa wakishiriki katika matukio mbalimbali ya kuua watoto wachanga na kutegemea kulipwa ujira kutokana na kazi hiyo. 

 Matukio mengi ya aina hiyo yamekuwa hayaripotiwi kutokana na usiri wa wahusika kutaka mambo yao yasiwekwe hadharani lakini Oparesheni Fichua Maovu (OFM), inaendelea kufichua unyama huo na kuumwaga hadharani.
 Mara kadhaa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, chini ya Waziri Sophia Simba imekuwa ikikemea tabia mbaya ya baadhi ya manesi kutumia vibaya taaluma yao na kuendeleza mauaji hayo.   

SAFARI HII NI MBAGALA
Baadhi ya wazazi wanaoishi Mbagala Kizuiani jijini Dar waliochoshwa na tabia ya manesi kuua vichanga, walipiga simu OFM na kulalamikia vitendo vilivyokithiri vya utoaji mimba katika dispensari iliyopo maeneo yao.
Nesi Maria akiwa katika harakati za kuandaa sindano ya ganzi na vifaa vingine kufanikisha zoezi la kutoa mimba.
 OFM iliambiwa kuwa dispensari hiyo ina manesi wengi wenye ujuzi na fani yao lakini shughuli kubwa wanayoifanya ni kutoa mimba ili kujipatia fedha kwa njia haramu.
 “Manesi wa kike wanafanya shughuli za kuua vichanga ambavyo bado havijapata ruhusa ya kuingia duniani, kwa kweli inauma sana,” alisema mmoja wa wazazi hao.
Taarifa zikasema kwamba manesi hao wapo wengi lakini anayefahamika zaidi ni Maria ambaye amejizolea umaarufu kwa kazi hiyo katika eneo lote la Mbagala.
 “Ni muda mrefu amekuwa akifanya mchezo huo, tena anafanya shughuli zake bila ya hofu utadhani vitendo hivyo vimeruhusiwa na mamlaka husika,” aliongeza mzazi mwingine.
Badhi ya vifaa vilivyoandaliwa na nesi kwa ajili ya zoezi la utoaji mimba.
 OFM IMEJENGA HESHIMA
Wazazi hao wamesema kuwa wanaamini kuwa Maria atanaswa  kama alivyonaswa Dokta Mambo wa Kawe jijini Dar ambaye naye alikuwa maarufu kwa shughuli kama hizo lakini OFM ikamshikisha adabu.
Baada ya kutoa maelezo hayo, mmoja wa wazazi hao alitoa namba ya simu ya Maria kwa kamanda mkuu wa OFM.
 MTEGO WAANDALIWA
Kamanda Mkuu wa OFM alimpigia simu Maria na kumwambia kuwa alikuwa akitaka huduma ya kumtoa mimba mke wa mtu aliyempa kwa bahati mbaya kabla mumewe hajarudi kutoka safarini.
Maria: Hakuna shaka wee njoo tu dispensari kwetu, si umeelekezwa?
Kamanda: Ndiyo.
 Maria: Njoo basi tumalize kazi leoleo. 
Kamanda: Hiyo kazi inaweza kufanyika kwa ufasaha?
Maria: Miye huwa sishindwi na chochote, wee njoo utafurahi kwa huduma yangu lakini wahi kwani namaliza shifti jioni.
Sindano zilizoandaliwa tayari kwa ajili ya zoezi la utoaji mimba.
 OFM YAJIPANGA
Baada ya maelezo hayo, kamanda wa OFM akaanza kuwapanga vijana  wake kwa ajili ya kumnasa Maria katika mtego huo siku hiyohiyo ya Machi 15, mwaka huu.
 Mmoja kati ya vijana waliopangwa katika zoezi hilo ni mwanamke mjazito ambaye alitolewa hofu kwamba mimba yake haitatolewa na OFM watakuwa wameshavamia katika chumba cha utoaji mimba.
Pia, OFM iliwasiliana na polisi wa Kituo cha Mbagala Kizuiani kwa lengo la kumkamata Maria.
 MCHEZO MZIMA
Saa tisa mchana, OFM walikuwa wametanda katika dispensari husika wakiwa na askari waliokuwa wamevaa nguo za kiraia.
 KAMANDA ATINGA FRONTI
Baada ya kupeana ishara za kikazi, OFM na baadhi ya polisi waliingia ndani ya dispensari hiyo kwa nyakati tofauti huku wakijifanya ni wagonjwa.
 
Nesi Maria akijuta mara baada ya kunaswa na OFM.
 Baadhi yao walijidai wamefika hapo kwa ajili ya kupima malaria huku wakimuacha kamanda mkuu wa OFM akisonga fronti akiongozana na binti anayetakiwa kutolewa mimba.
 NESI MARIA AITWA MAPOKEZI
Kamanda wa OFM alipofika mapokezi ya dispensari hiyo, alipokewa na kusema shida yake ilikuwa ni kuonana  na nesi Maria.
 Bila ya kinyongo wafanyakazi wa mapokezi waliwasiliana na Maria ambaye naye alimtuma msaidizi wake aitwaye Maimuna kuwapokea wageni hao kisha kuwapeleka katika chumba maalum.
Maimuna alizungumza na kamanda na kuanza kuelewana kuhusu malipo ya kazi hiyo ya utoaji mimba.
Maimuna: Huwa tunatoa huduma hiyo kwa shilingi 80,000.
Kamanda: Dah! Miye nina shilingi 50,000.
 Maimuna: Ongeza kidogo maana ni kazi ngumu sana.
Kamanda: Naomba mnisaidie tafadhali.
 Baada ya maongezi ya muda mrefu, Maimuna alikubali kupokea shilingi 50,000 na kuanza kumpima mjamzito baada ya kumuelekeza kupanda kitandani kwa ajili ya maandalizi ya zoezi zima la utoaji mimba. 
MIMBA YA MIEZI MIWILI
Vipimo vya dispensari hiyo vilionesha kuwa ujauzito ulikuwa na umri wa miezi miwili, Maimuna akatoka na kwenda kuchemsha vifaa vya kazi.
 SINDANO TATU ZAANDALIWA
Katika chumba maalum cha kutolea mimba, Maimuna aliweka vifaa vyote zikiwemo sindano tatu za ganzi alizokuwa achomwe mjamzito huyo ili asisikie maumivu.
 MARIA AINGIA MZIMAMZIMA
Baada ya Maimuna kukamilisha kazi yake, aliendelea kubaki kwenye chumba maalum, ndipo Maria akaingia chumbani humo mzimazima akitaka kukamilisha kazi yake.
 Kamanda wa OFM alipiga hesabu zake na kutoa ishara maalum kwa wenzake waliokuwa nje ili wavamie kwa kuwa mtego ulikuwa umeshakamilika.
 MARIA APIGWA NA BUTWAA
Akiwa haelewi kilichokuwa kikiendelea, Maria alipigwa na butwaa alipoona amevamiwa chumbani humo na watu asiowajua.
Taharuki yake ikamfanya ahisi kuwa alikuwa amenasa kwenye mikono ya OFM baada ya kuona kamera zikifanya kazi yake.
 ALIJUA ATANASWA
OFM na askari walijitambulisha lakini Maria aliomba sana asitolewe gazetini.
“Chondechonde msinitoe gazetini kwani yatakuwa ni kama yale ya Dokta Mambo,” alisema akiwa ametahayari.
 Alipoulizwa kama alikuwa akifahamu kilichomkuta Dokta Mambo, Maria alisema aliposoma habari ya dokta huyo alijua kuwa naye kuna siku angenasa ila hakujua ni lini.
 Ama kweli nimepatikana, yaani kama mlivyomnasa Dokta Mambo, nilijua tu kwamba lazima siku moja na mimi nitanaswa na OFM, kweli sitarudia tena,” alisema  Maria akiomba mambo yaishe palepale.
Baada ya OFM  kumaliza  kazi yao, waliwaachia polisi ambao waliwachukua Maria na Maimuna na kuwapeleka kituoni.
 DAKTARI WA MUHIMBILI ATAJWA
Hata hivyo, Maria alimtaja daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (jina tunalo) kuwa ndiye anayehusika na dispensari hiyo.
 Alipotakiwa kumpigia simu na kumtaka afike dispensari hapo, daktari huyo alikubali kufika kabla ya saa 11 jioni lakini hadi saa mbili usiku hakuwa ametia mguu wake.
Uchunguzi umebaini kuwa huenda alipenyezewa taarifa za kilichotokea na kushauriwa kutofika kwenye dispensari kukwepa msala huo.
 Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, ingawa mmoja wa wasaidizi wake ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea. 
KUTOKA KWA  MHARIRI
Bado OFM iko kazini na kamwe haitalala, Maria alijua iko siku atanaswa ila hakujua siku wala saa, bado wewe ambaye unadhani hatutakukamata! Itafika zamu yako, acha kufanya uovu na mambo yasiyokubalika katika jamii.
-GPL

Post a Comment

Previous Post Next Post