Operesheni wahamiaji haramu imeishia wapi?

Kutokana na wakimbizi hao kuzoea utamaduni wa Serikali wa kutosimamia utekelezaji wa uamuzi wake, wahamiaji wengi walikaidi agizo hilo la Serikali kwa kudhani mamlaka husika zisingekuwa na uthubutu na dhamira ya kuwarudisha makwao.PICHA|MAKTABA 

Operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu iliyofanyika nchi nzima mwishoni mwa mwaka jana ilionyesha mafanikio makubwa. Baada ya miaka mingi ya wahamiaji kuishi nchini kinyume cha sheria na kuifanya nchi yetu kuwa kama haina wenyewe, sasa raia wa nchi mbalimbali waliokuwa wakidhani Tanzania haina wenyewe wamesoma maandishi kwenye ukuta na kutambua kuwa, hakika Tanzania ina wenyewe, hivyo siyo rahisi tena kuingia nchini kiholela.
Ukweli ni kwamba nchi yetu ililea tatizo hilo la wahamiaji haramu. Ni siri iliyo wazi kwamba tatizo hilo halikuanza leo wala jana, bali lilianza mara baada ya nchi yetu kupata uhuru mwaka 1961 ambapo sera ya nchi yetu ya kuwaona Waafrika wote kama ndugu, ilipotoshwa ama ilitafsiriwa vibaya na baadhi ya Waafrika wenzetu, hivyo kuingia nchini kutoka kila pembe ya Afrika pasipo kufuata taratibu. Matokeo yake ni usalama wa taifa kuwekwa rehani kwa kuachia mipaka yetu kuingiwa kirahisi kwa namna ambayo ni vigumu kuielezea.
Matokeo yake ni Watanzania wenzetu katika mikoa ya mipakani kulazimishwa kuishi kama mateka au wakimbizi katika nchi yao. Wahamiaji haramu pamoja na wengine wengi walioitwa wakimbizi kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi zao, waliifanya Tanzania kama kimbilio pekee katika pembe hii ya dunia. Muda si mrefu tulianza kushuhudia kuzorota kwa hali ya usalama kutokana na kushamiri kwa vitendo vya uhalifu kama mauaji, utekaji wa magari na kuzagaa kwa silaha za kila aina. Uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji uliongezeka kwa kasi ya kutisha na kuleta njaa na hata kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha.
Wakati huo, tulimpongeza Rais Jakaya Kikwete alipoamuru wahamiaji wote haramu warudi makwao kwa hiari, vinginevyo ingeendeshwa operesheni maalumu ya kuwarudisha makwao kwa nguvu. Wakimbizi wapatao 14,000 walirudi makwao kwa hiari, lakini wenzao wengi walikaidi agizo hilo na kujibana kwa wenyeji na sehemu nyingine, yakiwamo mapori.
Kutokana na wakimbizi hao kuzoea utamaduni wa Serikali wa kutosimamia utekelezaji wa uamuzi wake, wahamiaji wengi walikaidi agizo hilo la Serikali kwa kudhani mamlaka husika zisingekuwa na uthubutu na dhamira ya kuwarudisha makwao. Hivyo, operesheni hiyo ilipoanza walitaharuki na kukumbwa na mfadhaiko mkubwa. Ndiyo maana operesheni hiyo iliwanasa wahamiaji wengi na wa kila aina, wakiwamo wachungaji, walimu, wafanyabiashara na wafanyakazi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika waliokuwa katika ajira mbalimbali kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na walioajiriwa katika sehemu nyeti kama viwanja vya ndege, ofisini na viwandani. Operesheni hiyo pia iliwatia mbaroni Watanzania waliokamatwa wakiwa wamewaficha majumbani mwao wahamiaji hao haramu.
Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kuendesha operesheni hiyo kwa ufanisi, tunasikitishwa na kushindwa kwake kuhakikisha operesheni hiyo inakuwa endelevu. Kila kukicha tumeendelea kushuhudia makundi ya wahamiaji haramu kutoka nchi za Ethiopia, Eritrea na Somalia yakiingia nchini na pindi yanapokamatwa yanadai yalikuwa yakielekea Afrika Kusini. Hii ina maana kwamba mipaka ya nchi yetu bado inavuja kwa kiwango kikubwa, hasa kutokana na vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa vikosi vya ulinzi na usalama. Ushauri wetu kwa Serikali ni kwamba iendeleze operesheni hiyo na ishirikiane na serikali za nchi hizo tulizozitaja hapo juu ili kwa pamoja zipate suluhisho la kudumu.
- Mwananchi- 

Post a Comment

Previous Post Next Post