Waandishi walishuhudia mamia ya magari hayo
yakikwama baada ya kushindwa kushindwa kupita katika barabara kuu ya Dar
es Salaam-Morogoro, eneo la Ruvu Sekondari, wilayani Kibaha na Ruvu
Darajani, wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani, baada ya mto Ruvu kufurika na
maji kuziba njia na madaraja, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha
katika mikoa ya Ukanda wa Pwani.
Abiria hao waliokwama katika barabara hiyo kwa zaidi ya saa
15 Aprili 13, mwaka huu ni wale waliokuwa wakisafiri kuelekea mikoa ya
Morogoro na Tanga .
Na wengine ni wale waliokuwa wakiafiri kwenda mikoa ya Kusini
(Lindi na Mtwara) baada ya daraja la mto Mzinga uliopo Kongowe kubomoka
na kusombwa na mafuriko.
ATHARI YA MVUA KIBAHA, BAGAMOYO
Mbali na kukatika kwa mawasiliano ya usafiri kufuatia mto huo
kufurika, pia nyumba zaidi ya 10 zilizojengwa kwa saruji zimebomoka,
huku nyigine zaidi ya 20 zilizojengwa kwa udongo zikiripotiwa
kumomonyoka kabisa huku nyasi zilizokuwa zimetumika kuezeka zikisombwa
na mafuriko.
Ramadhani Mnyamani na Said Mtotole, ambao ni wakazi wa
maeneo hayo, kwa nyakati tofauti walisema maji yaliyosambaa eneo lote
hilo hayajasimama, bali yanatembea kwa kasi kutokana na mto Ruvu
kufurika baada ya mvua kunyesha kwa siku tatu mfululizo.
Walisema hali hiyo imesababisha mafuriko, hususan katika eneo la darajani.
KAULI YA KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, amethitibisha kukwama kwa magari hayo pamoja na abiria.
Aliwataka wananchi wenye lengo la kusafiri kuelekea mikoani
kupitia eneo hilo, kuangalia uwezekano wa kuahirissha kama hakuna
ulazima kuliko kuendelea wakati njia ipo mashakani kutokana na mvua
zinazonyesha.
“Naomba kama mtu hana ulazima wa kusafiri kwa sasa kuelekea
mikoani, abaki kwanza, aangalie usalama wake. Na kama safari hiyo ina
ulazima, basi watafute njia mbadala ya kupitia kutokea Dar es Salaam.
Mfano, wapitie Bagamoyo wakatokee Msata na kuendelea na safari, kama
Tanga sawa. Na kama Mororgoro, arudi hadi Chalinze kisha aende zake,”
alisema Matei.
Alisema kwenye matatizo siyo lazima mtu aambiwe, ila kutokana
na hali halisi, hapana budi kutoa ushauri ili kuepusha matatizo kwa
abiria au mtu anayetaka kutumia barabara hiyo kuwa kwa sasa haipitiki
kutokana na uharibifu wa miundombinu na baadhi ya magari kukwama.
JK ATEMBELEA DARAJA MTO RUVU
Rais Jakaya Kikwete alifika katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi na kuwataka wawe wavumilivu kwa kuwa ni janga la kitaifa.
Rais Kikwete alisema kama kiongozi wa serikali hali hiyo inamuumiza japo haiwezi kuzuilika.
“Kwa kweli tuwe wavumilivu. Nimeagiza jeshi wahakikishe
usalama na maji yatakapopungua mtaruhusiwa kupita na kuendelea na safari
japo tunajua mmechelewa,” alisema Kikwete.
Alisema ni muhimu wananchi wakawa wanapenda kufuatilia vyombo
vya habari ili kujua hali ya nchi inavyokwenda, kwani toka jana
ilionekana wazi kuwa kuna maeneo hayatapitika ikiwamo Pwani.
Katika tukio hilo lililochangia kifo cha mtoto wa mwaka mmoja
na nusu baada ya kuugua ghafla kutokana na hali ya hewa kubadilika.
MAHIZA ANENA
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza,
aliwataka wasafiri wote pamoja na wananchi kuwa watulivu mpaka hali
itakapotulia na kuruhusu gari kuanza kupita.
“Tunawaomba jamani watu kuwa watulivu. Nimeagiza wanaofanya
biashara ya chakula kutopandisha bei, huku Jeshi la Wananchi likiagizwa
kupunguza bei ya chakula katika baa yao, iliyopo eneo hilo,” alisema
Mahiza.
Aliiomba Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi kavu
(Sumatra) kuzuia magari kusafiri mpaka kutakapokuwa na uhakika wa hali
ya hewa na kuwataka wafanyabiashara kuwa na utu na kuacha kupenda fedha
kunapokuwa na majanga kama hayo.
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya abiria walisema imewaletea
karaha katika safari yao kwani walitegemea kufika mapema lakini
hawajui kama kuna uwezekano wa kupita.
Shabani Issa, abiria wa basi la Musoma Express linalofanya
safari zake Dar-Musoma alisema: “Namuachia Mungu kwa kweli. Maana sijui
hatma yangu nini mpaka sasa, ikitokea nakwenda sawa ikitokea nimekwama
sawa. Nimechanganyikiwa kabisa.”
Juma Kaiko, ambaye ni abiria wa basi la Kampuni ya Saibaba ya
Arusha, alisema: “Mimi naenda msibani nimefiwa na mama yangu mzazi
wanazika saa 10 jioni na mfukoni nina hela ya nauli tu. Kwa hiyo,
nimepata pigo kubwa sana.”
NDUGAI AKWAMA
Adha hiyo pia iliwakuta baadhi ya viongozi akiwamo Naibu Spika
wa Bunge, Job Ndugai na kulazimika kuungana na wananchi kusubiri saa
kadhaa katika eneo hilo.
Ndugai aliwataka baadhi ya madereva kuwa wasikivu kutii amri ya Serikali inapotolewa ili kuepuka maafa.
“Hii hali hakuna wa kumlaumu, maana viongozi wanatoa taarifa,
lakini matokeo kama haya ni Mungu anapanga na kutekeleza mwenyewe,”
alisema Ndugai.
Hata hivyo, hali ilianza kutengemaa na magari kuruhusiwa kupita kuanzia saa 11 jioni.
DARAJA MSUGUSUGU LAVUNJIKA
Wakati huo huo; katika barabara hiyo eneo la Msugusugu daraja
limevunjika na kusababisha magari mizigo kushindwa kuendelea na safari.
MTO MZINGA WAKWAMISHA ABIRIA
Wakati hali ikiwa hivyo katika daraja la mto Ruvu, maelfu ya
abiria waliotarajia kusafiri kwenda mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara)
jana walishindwa kufanya hivyo baada ya daraja la Mto Mzinga lililopo
eneo la Kongowe, jijini Dar es Salaam, kubomoka na kusombwa na mafuriko
kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo na mikoa ya jirani.
Akizungumza na NIPASHE jana, mmoja wa mashuhuda, Hamisi
Mohamed, ambaye ni mkazi wa Kongowe, alisema daraja hilo lilibomoka
jana, majira ya saa 12:00 asubuhi baada ya mabasi matatu kuvuka.
Alisema mbali na daraja hilo kubomoka, pia nyumba tisa
zilizokuwa na familia zaidi ya 15 zilisombwa na mafuriko na nyingine
kujaa maji, ikiwamo yake.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, hali hiyo imesababisha zaidi ya familia 50 kukosa makazi kutokana na kusombwa na mafuriko.
“Daraja lilibomoka saa 12:00 asubuhi leo (jana) na kufanya
msururu wa mabasi yaendayo mikoa ya Kusini kushindwa kufanya safari
zake… pia familia zaidi ya 50 hazina makazi baada ya nyumba tisa
kubomoka na nyingine zaidi ya 110 kujaa maji,” alisema Mohamed.
“Mimi mwenyewe nimeihamisha familia yangu baada ya nyumba yangu kujaa maji, ” aliongeza.
Alisema kutokana na daraja hilo kubomoka, watu walioko upande
wa Kongowe na Mbagala hawezi kuvuka kutoka upande mmoja kwenda
mwingine.
NIPASHE ilishuhudia msururu wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kwenda mikoa hiyo, huku yakiwa na abiria.
Mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Kimara jijini Dar es Salaam,
Fridah Mwidadi, alisema alitarajia kusafiri na kufika Wilaya ya Newala
mkoani Mtwara jana kufanya mazoezi ya vitendo katika Hospitali ya Wilaya
hiyo, lakini safari yake iliishia Mbagala baada ya uongozi wa basi la
Ibra kuomba radhi saa 6:30 mchana kwa kuahirisha safari hiyo.
KAWE WABOMOA NYUMBA ZAO
Pia baadhi ya wakazi wa Kawe wanaoishi pembezoni mwa mto Mbezi
jijini Dar es Salaam, jana walilazimika kubomoa nyumba zao kutokana
kwakuhofia kuharibika.
NIPASHE lilishuhudia wakazi hao wakihaha kubomoa nyumba zao,
kung’oa madirisha, milango na mabati ili kunusuru zizisombwe na
mafuriko huku nyingine zikijaa maji na kuzolewa.
Wakizungumza baadhi yao, walisema wameamua
kubomoa nyumba hizo ili kuokoa mabati, madirisha na milango kuliko
kuacha vikisombwa na mafuriko.
Mmoja wa wamiliki wa nyumba kwenye eneo hilo , Ally Abdalah,
alisema hakutegemea kama mto huo unaweza kufurika na kuleta madhara
makubwa na kwamba, alilazimika kuwaamuru wapangaji wake kuhamisha mali
zao kabla ya maji kujaa ndani ya nyumba.
Hawa Hamisi alisema amelazimika kuhamisha vitu vyake na
kuvipeleka mbali ili kuepusha uharibifu na kunusuru maisha yao na watoto
wao kutokana na nyumba hizo kuanza kujaa maji.
“Hapa nilipo sina fedha ya kupanga nyumba nyingine na kwenye
nyumba hii mkataba wangu haujaisha. Kwa sasa nimehifadhi vitu kwa ndugu
zangu…hatima yangu siijui na nyumba ndiyo hiyo imebomoka,” alisema.
Waliiomba serikali kuwasaidia kila yanapotokea majanga kwa watu wa maeneo ya Jangwani, Kigogo na Mbuyuni.

Post a Comment