Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta anahaha kulinusuru Bunge hilo, baada ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zilisema Sitta anawasaka viongozi wa Ukawa kwa lengo la kukaa nao katika meza ya mazungumzo, kutafuta maridhiano yatakayowezesha kundi hilo kurejea bungeni.
Sitta jana aliliambia Mwananchi kuwa wako njiapanda, kwa sababu hawafahamu kama wajumbe hao wa Ukawa wametoka tu nje ya ukumbi na watarudi au wamejiuzulu.
"Hapa ninapozungumza na wewe
nimesitisha kwenda mapumziko ya Pasaka... Nimewapigia simu Lipumba
(Ibrahim) na Mbowe (Freeman), lakini hawapokei simu," alisema Sitta na
kuongeza;
"Niliyempata ni Mbatia (James) peke
yake na ameniambia yeye yuko na wenzake na hana uamuzi wa
pamoja...Nataka nikutane nao ana kwa ana nasubiri kama inawezekana
tufanye mazungumzo."
Aliongeza: "Nasubiri hata kama
watatuma mwakilishi wao tukae tuzungumze hili jambo, lakini mpaka sasa
sijaona mwakilishi yoyote...huwezi kuamini sijaenda Pasaka niko hapa
Dodoma."
Sitta alisema pamoja na viongozi hao
wawili wakuu wa Ukawa hawapokei simu, lakini amefanya jitihada ikiwamo
kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), lakini hadi jana mchana alikuwa
hajajibiwa.
"Sitaki kuongeza chochote kuhusu hili
jambo kwa sababu kwa mazingira yenyewe nikisema chochote ninaweza
kuharibu japo nina maoni yangu binafsi kuhusu hili, lakini sitaki kusema
sasa," alisema Sitta.
Jana gazeti hili lilimtafuta Mbatia
ambaye alikiri kuzungumza na Sitta. "Ni kweli amenipigia simu na
nimemwambia kwamba nimemsikia, lakini siwezi kufanya uamuzi peke yangu,
lazima nishuriane na wenzangu."
Hata hivyo, Mbatia alisema kwa mtizamo
wake hadhani kama Sitta anaweza kutatua mvutano uliopo na kwamba
wanaopaswa kusimamia suala hilo ni viongozi wa vyama vya siasa
vinavyovutana.
"Mimi naamini katika maridhiano,
lakini vyama vya siasa ndivyo vinaweza kutatua mzozo huu, kwa hiyo
viongozi wa CCM ndiyo wanaweza kuonyesha nia ya kuzungumza, Sitta ni
kiongozi wa Bunge ambaye kazi yake ni kusimamia uendeshaji wa vikao,
hivyo suala la maridhiano kwake ni kumtwisha mzigo mzito ambao hapaswi
kuubeba," alisema Mbatia.
Kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo za
2014, zinasema kuwa ili ibara au Rasimu ya Katiba iweze kupitishwa
itahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe kwa pande zote za
Muungano.
Post a Comment