Awali, wakizungumza nje ya ofisi
za kampuni hiyo zilizopo Ubungo jijini Dar es Salaam juzi, wafanyakazi
hao wanaojenga barabara za mabasi yaendayo kasi chini ya Mradi wa DART,
walisema walifikia hatua ya kugoma kwa madai ya kuona wanazungushwa
kupewa marupurupu hayo huku wakihofu muda uliobaki kwa kampuni hiyo
kabla ya kumaliza kazi yake.
“Marupurupu hayo yanayohusisha fedha za
chakula, usafiri, matibabu ambayo jumla yake ni shilingi elfu sabini kwa
kila mwezi yapo katika mkataba wa kazi na mwanzoni tulikuwa tukilipwa
lakini cha kushangaza baadaye yalisitishwa bila sababu zozote za
msingi,” walisema wafanyakazi hao, ambao hata hivyo hawakupenda majina
yao yaandikwe gazetini.
Kwa mujibu wao, muda wa kampuni hiyo
kumaliza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo, unaelekea ukingoni jambo
linalowapa hofu ya kupewa malipo hayo huku kesi ya msingi iliyopo
mahakamani ikiwa bado haijakwisha wala kujua itakwisha lini huku
wakidai kuendelea kuumizwa na majukumu mbalimbali ya kimaisha.
“Walikimbilia
kufungua kesi katika Mahakama ya Kazi ya Kinondoni kutaka kuondolewa
kwa malipo hayo, na hadi sasa ni miezi saba kesi bado ipo mahakamani
ikipigwa danadana hatujui lini itakwisha na kama unavyojua karibu
wanamaliza kazi tuna hofu haki yetu kupotea,” walisema wafanyakazi hao.
Walisema
wakati wao wakifanyiwa kitendo hicho, wafanyakazi wenzao kutoka nchi za
Kenya,Kongo na India wanaendelea kulipwa marupurupu hayo kama kawaida
huku wakidai kuwa hawaelewi kwa nini wanafanyiwa hivyo wakati kazi
wanazozifanya wao zinalingana na wafanyakazi hao wa kigeni.
Wafanyakazi
wakiwemo madereva, waendeshaji wa mitambo, wasimamizi na makundi
mengine walisema wanachotaka ni malipo yao bila kujua lini hatma ya kesi
iliyotolewa itafikiwa vinginevyo hawatokuwa tayari kurejea kazini.
Wakati
huo huo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana amewataka
wafanyakazi hao kurejea kazini wakati suala lao likiendelea
kushughulikiwa na mamlaka zinazohusika.
Akizungumza na mwandishi
jana, alisema baada ya kupata taarifa hizo juzi, Katibu Tawala wa Wilaya
hiyo, uongozi wa Strabag, viongozi wa wakala wa Barabara nchini
(TANROADS) pamoja na viongozi wa Ofisi ya DART walikutana kuzungumzia
suala hilo alilosema kuwa hata hivyo linahitaji busara kwa kuwa kesi
yake bado ipo mahakamani.
Post a Comment