BALOZI wa Ubelgiji
nchini Tanzania Koen Adams amevitaka vyombo vya habari na hasa Radio na TV kuwa
chachu katika kuleta maendeleo na kubadilisha maisha ya wananchi badala ya
kutumika vibaya na hatimaye kuleta maafa.
Adam alisema hayo
mkoani Kigoma alipotembelea taasisi ya KICORA ambayo pamoja na mambo mengine
inajihusisha na utoaji wa elimu kwa njia ya Radio na kusema kuwa vyombo vya
habari vikitumiwa vizuri ni msaada mkubwa kwa maendeleo ya jamii.
Katika hilo alisema kuwa vyombo
vya habari vimekuwa vikisaidia kuhamasisha jamii katika kujiletea maendeleo yao
kwa haraka ambapo amewaomba wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuona namna
ambavyo wanaweza kuvitumia vyombo vyao iwezekanavyo katika kubadilisha maisha
ya jamii inayowazunguka na kuleta maendeleo.
Kinyume chake alionya kuwa
kilichotokea nchini Rwanda na kusababisha mauaji ya halaiki kinaweza kutokea
mahali popote nchini ambapo amesema kuwa asingeomba hilo litokee tena mahali
pengine duniani kwa vyombo vya habari kutumika vibaya.
Akizungumzia kauli hiyo ya
Balozi wa Ubelgiji Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya KICORA, Deo Baribwegure
alisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya mawasilianoi
nchini (TCRA) ambao wamekuwa wakisimamia kwa karibu matangazo yanayorushwa na
Radio na TV mbalimbali nchini.
Deo alisema kuwa Radio yake
kwa kiasi kikubwa imejikita katika kutoa msaada kwa jamii ikiwemo suala la
elimu na masuala mbalimbali ya kiuchumi na hasa kwa wakati huu wa sayansi na
teknolojia ambapo Radio zimekuwa na nafasi kubwa ya kusikilizwa na jamii
mbalimbali.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo
alisema kuwa bado taasisi yake ambayo imekuwa ikijiendesha bila faida
inakabiliwa na changamoto ya kupata mtaji wa kuifanya Taasisi hiyo kuendesha
shughuli zake kikamilifu.
Aidha ametoa shukrani za
dhati kwa serikali ya Ubelgiji na wananchi wan chi hiyo ambao wamekuwa na
msaada mkubwa katika kusaidia shughuli mbalimbali za taasisi hiyo ambazo
zimekuwa zikipata misaada na ufadhili kutoka nchini Ubelgiji.
Source Journalist press Kigoma

Post a Comment