Mwanachama wa chama kipya cha siasa cha Alliance for
Change and Transparency (ACT-Tanzania), Dk Kitila Mkumbo, amesema atahakikisha
anazungumza na viongozi wa chama hicho, ili wamshawishi mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Kabwe Zitto, ajiunge na chama hicho.
Mkumbo, aliyasema hayo, Dar es Salaam jana wakati
alipohojiwa na gazeti hili kuhusu kuhusika kwake na chama hicho kipya
kilichopata usajili wake wa kudumu juzi, ambapo alikiri kuwa mwanachama wa
chama hicho.
“Ni kweli mimi ni mwanachama wa ACT, lakini sina
nafasi yeyote ya uongozi kutokana na kazi yangu, ila nitakuwa natoa ushauri wa
namna ya kukiendeleza chama chetu, likiwemo suala hili la Zitto,” alisema.
Alisema yeye ni rafiki mkubwa wa Zitto na wamekuwa
wakishirikiana pamoja kwenye masuala ya siasa kwa miaka mingi na anatambua
uwezo wake hivyo endapo atashindwa na Chadema, atahakikisha mwanasiasa huyo
anajiunga na chama hicho cha ACT.
“Zitto ni mwanasiasa mashuhuri na ni mtu muhimu
katika siasa za nchi yetu, si vizuri aendelee kutangatanga, kwa sasa uhusiano
wake na Chadema si mzuri kwani ni mbunge kwa kupitia mahakama, endapo hali
itazidi kuwa mbaya, nitawashauri viongozi wangu, tumshawishi ajiunge huku
tuendeleze siasa ya kweli,” alisisitiza.
Mkumbo aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema
lakini yeye, Zitto pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, mkoani Arusha
Samson Mwigamba, walivuliwa nyadhifa zao na Chadema kwa madai ya uhaini na
hujuma dhidi ya chama hicho kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa
uchaguzi 2013.
Post a Comment