Wakati
watu 400 wakithibitika kuwa na ugonjwa wa
homa ya dengue, huku wengine watatu wakifariki dunia, Serikali imetoa
taarifa kuhusu dalili za ugonjwa huo na namna inavyokabiliana nao.
Mbali
na kutoa taarifa hizo, Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania popote walipo,
wakipata dalili hizo, wasinywe dawa hovyo, badala yake waende kupima hospitali
na kufuata ushauri wa kitaalamu.
“Naomba
watu wakiona dalili za homa waende hospitali kupima maana hivi sasa kuna
ugonjwa huu wa dengu…msinywe dawa tu bila kupima maana
sasa unasambaa hivyo muende hospitali,” alisema Rais Kikwete.
Pia
Rais Kikwete aliagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Wizara ya Fedha,
kuhakikisha kunakuwa na dawa pamoja na vifaa tiba vya kutosha kudhibiti ugonjwa
huo, kwa kuwa ni wa dharura.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, alisema dalili za
ugonjwa huo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu na dalii hizo huanza
kujitokeza kuanzia siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya
dengue.
“Kwa
wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana na dalili za malaria,
hivyo basi tunawaomba wananchi wakipata homa kuhakikisha wanapima kama wana
malaria au la, ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Pallangyo.
Aliongeza
kuwa kuna aina tatu tofauti za ugonjwa huo katika namna unavyojitokeza, iwapo
mtu aking’atwa na mbu mwenye virusi hivu.
Aina
ya kwanza ndio homa ya dengue yenyewe, ambayo huambatana na dalili kuu tatu za
homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu. Kwa Tanzania
mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wamejitokeza wakiwa na dalili hizo.
Aina
ya pili ni dengue ya damu, ambayo huambatana na dalili za magonjwa kutokwa na
damu kwenye fizi au puani na kutokwa na damu chini ya ngozi. Iwapo mgonjwa huyo
ataumia sehemu yoyote, ni rahisi kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko.
Aina
ya tatu ni dengue ya kupoteza fahamu, ambayo huambatana na mgonjwa kupoteza
damu nyingi ambayo husababisha mgonjwa kupoteza fahamu.
Mpaka
sasa dalili hizo zimeonekana kwa mgonjwa mmoja kati ya wagonjwa 400
waliokwishwa thibitika kuwa na ugonjwa hapa nchini.
Pallangyo
alisema kwa wiki iliyoisha Mei 9, idadi ya wagonjwa waliogundulika mkoani Dar
es Salaam ilikuwa 60; katika Wilaya ya
Kinondoni watu 42; Temeke 14 na Ilala
wanne. Mpaka sasa wagonjwa waliopo wodini 13 na wengine wameruhusiwa kwenda
nyumbani.
Alifafanua
kwamba mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini, kwani uligundulika kawa mara
ya kwanza Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu 40 walithibitika
kuwa na ugonjwa huo. Pia kati ya Mei hadi Julai 2013 wagonjwa 172 walithibitika
kuugua ugonjwa huu.
Alisema
ugonjwa huu unasababishwa na mbu aina ya Aedes na kirusi cha dengue
kinaambukiza kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kwa kuunmwa na mbu huyo.
Mbu
huyo anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu na huuma wakati wa mchana
ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani asubuhi na jioni kabla
jua halijazama.
Aliwashauri
wananchi kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huo, kwani hauambukizwi kwa kumhudumia
mgonjwa au kwa kugusa maji yanayotoka kwa mgonjwa.
Akizungumzia
kinga, Pallangyo alisema kinga pekee iliyopo ni kuangamiza mazalia ya mbu ikiwemo kufukia
madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyuzia viatilifu vya kuua viluwiluwi vya
mbu kwenye madimbwi hayo.
Katika
kuua mazalia hayo, ametaka wananchi kuondoa vitu vyote vinavyoweka mazalio ya
mbu kama vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yalipotupwa hovyo.
Pia
alitaka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu vifyekwe na kuhakikisha maua
yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya
maji taka kwa mifuniko imara na kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu
maji kutuama.
Alisema
mpaka sasa ugonjwa huu hauna chanjo wala dawa maalumu kwa ajili ya kudhibiti
ugonjwa huo, na njia kubwa ya kupambana na ugonjwa huo ni kumzuia binadamu
asiumwe na mbu.
Wakati
huo huo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa
kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kinatarajia kufanya utafiti
kuhusu ugonjwa wa dengue ili kupata matokeo yatakayowezesha
kukabiliana
nao.
Utafiti
huo utakaoanza hivi karibuni, utafanyika kupitia Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa
ya Binadamu (NIMR).
Kaimu
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eligius Lyamuya, alisema hayo jana
na kufafanua kwamba kuanzia Aprili 3 mwaka huu hadi Mei 9, wanafunzi 56
walikuwa na dalili za ugonjwa huo na baada ya kufanyiwa vipimo 17 walithibitika
kuugua na kupewa matibabu na kupona.
Kutokana
na dalili za awali kuonesha wameathirika, chuo kimeamua kupeleka sampuli za
wale wengine NIMR kwenye vipimo madhubuti ili kupimwa na kupatiwa majibu
sahihi.
“Baada
ya kuna wanafunzi wetu wameathirika, tuliamua kuchukua tahadhari kwa
kushughulikia maeneo yote yanayoonesha kuna mazalio ya mbu, lakini bao
tunahitaji ushirikiano na manispaa kudhibiti maeneo kama katika bonde la
Jangwani,” alisema.
Akizungumzia
utafiti watakaofanya, alisema pia watashirikiana na Hospitali ya Taifa
Muhimbili na manispaa za jiji ili kuangalia tatizo na kujipanga
kukabiliana nalo.
Alisema
muda wa kutoa matokeo ya utafiti huo itategemea aina ya utafiti watakaofanya
kama kutumia wagonjwa kuchukua sampuli au kuangalia maeneo yanayozaliana mbu na
baadhi ya viashiria lakini alihaidi kutoka mapema.
Wakati
Serikali ilishaanza kufanyia kazi ugonjwa huo, Bunge jana lilitaka taarifa
rasmi juu ya ugonjwa huo ulioibuka hivi karibuni na kusababisha vifo kikiwemo
cha Mganga wa Hospitali ya Temeke,
mkoani Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Bunge, Mussa Zungu alitoa agizo hilo jana bungeni kutokana na mwongozo
ulioombwa na Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile (CCM) akitaka wabunge
na wananchi waelezwe rasmi juu ya ugonjwa huo kupitia bungeni.
Post a Comment