(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Frank Herbert aliwahi kusema
“Utawala bora, kamwe
hautegemei Sheria bali sifa binafsi za wale wanaotawala. Vyombo vya
Serikali mara zote vipo chini ya wale wanaowaongoza. Kwa hiyo sifa
muhimu ya Serikali ni namna ya kuteua/kuchagua viongozi”
Serikali ya awamu ya nne,
imeshindwa kuwajenga viongozi wake katika misingi bora na ndio maana
pamoja na matatizo ya kimfumo, wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea
kubadilisha viongozi na matokeo ya ufanisi wake yamekua ni kioja na
dhihaka katika utendaji.
2.0 UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO 16 YA BUNGE
Mheshimiwa Spika, kamati ya kudumu
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilileta Bungeni taarifa yake
tarehe 20 Disemba 2013 liyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Mhe. James
Lembeli kuhusu uchunguzi wa matatizo katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza Ujangili, iliyokua na maazimio kumi na sita (16). Taarifa hiyo
ndiyo iliyomuondoa aliyekua Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki na mawaziri wengine.
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya
maazimio ya Bunge, yaliyoongezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni
pamoja kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama. Aidha, ni takribani
miezi zaidi ya mitano kupita tangu Serikali iahidi Desemba mwaka jana,
kuahidi, kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuunda
tume maalumu ya kuchunguza kilichotokea wakati wa Operesheni Tokomeza
Ujangili. Katika makujukumu yake, Tume hiyo imepewa kazi zifuatazo;
a) Kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa;
b) Kuchunguza na kubaini iwapo sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza operesheni hiyo.
c) Kuchunguza na kubaini kama kuna mtu aliyekiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea wakati wa operesheni;
d) Kuchunguza na kubaini kama
kuna watu ambao walikiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa
operesheni hiyo na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali
zao zilikuwa stahiki;
e) Kupendekeza hatua zozote
zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu ambaye itabainika alikiuka sheria,
taratibu na hadidu za rejea pamoja na kupendekeza mambo ya kuzingatiwa
wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili
kuepuka kasoro.
Mheshimiwa Spika, pamoja na
kuundwa kwa Tume hii lakini Serikali haikupaswa tena kuipa tume kazi
mpya katika maeneo yote bali yale yaliyohitaji ushahidi wa ziada wa
kijinai, hii ni kwa sababu makosa mengine yako wazi ambayo Serikali
ilipaswa iwe imeshachukua hatua badala ya kusingizia inasubiri taarifa
ya tume. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, sasa inaitaka Serikali
iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge wakati wa
Majumuisho ya Bajeti ya Wizara ili maazimio ya Bunge hili yasiishie
kabatini kama ilivyokuwa kwa mengine ya miaka ya nyuma na ilivyozoeleka
sasa.
2.1 Uwajibishwaji Wa Watendaji Kutokana Na Maazimio Ya Bunge
Mheshimiwa Spika, aidha katika
azimio namba Saba (7), Bunge liliazimia pia kumwajibisha Mkurugenzi wa
Wanyamapori Prof. Alexander Songorwa kwa kutoa taarifa zisizo sahihi
kwenye vyombo vya habari na kuudanganya umma kuhusu mazingira na kifo
cha Emiliana Marrow wa Babati.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya
kushangaza Waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa, Mhe. Lazaro Nyalandu
ambaye akiwa katika nafasi yake ya unaibu waziri, kipindi kifupi tu
kabla ya uteuzi wake, kwa kasi ya ajabu aliandaa mikutano mingi na ziara
mbalimbali huku akiandamana na lundo la vyombo vya habari kama
kumbikumbi,na kutoa matamko makali dhidi ya ujangili na watumishi wasio
waaminifu. Akiwa katika ziara hizo, aliwahi kuikandia sana Ripoti ya
Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili iliyoongozwa na Mhe. James
Lembeli, huku akidai kuwa ilikuwa ya uwongo mtupu. Lakini baada ya
kubanwa zaidi, alikana kutoa kauli za kuikosoa ripoti hiyo ya kamati.
Sababu za kwanini akanushe maneno aliyoyasema zaidi ya mara nne,
inabakia kuwa siri yake mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, Waziri Nyalandu
alitoa taarifa za kuwavua nyadhifa zao Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori na
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori
nyadhifa zao. Nyalandu anadai kuwa moja ya sababu za kuwaondoa, ni
kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli kutokana na kutowajibika wakati
wa Operesheni Tokomeza. Jambo la kujiuliza, kama aliwahi kusema kuwa
taarifa ya kamati ni uongo mtupu, je ni lini amethibitisha kuwa kile
alichodai kwamba ni uwongo, ulikuwa ukweli? Cha ajabu, aliyeteuliwa
kukaimu nafasi ya ukurugenzi, Paul Sarakikya aliyekuwa kiongozi wa
utekelezaji wa operesheni tokomeza na aliyehusika moja kwa moja na
kinachodaiwa kuwa uvunjifu wa haki za binadamu, ndiye amepewa nafasi ya
kukaimu ukurugenzi! Wote tunafahamu ukiukwaji mkubwa wa haki za
binaadamu na ukatili uliofanywa katika operesheni tokomeza kiasi cha
kusababisha mawaziri wanne kuwajibishwa kwa kutenguliwa nafasi zao.
Mheshimiwa Spika, aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ilitumia vigezo gani kumteua
Sarakikya kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Wanyamapori huku ikijua
alivyoshindwa kutokomeza ujangili hapa nchini na jinsi aliyoendesha
operesheni tokomeza ujangili iliyokuwa imejaa dhuluma, uporaji, utesaji
na udhalilishaji dhini ya wananchi. Jambo ambalo liliishangaza zaidi
Kambi Rasmi ya Upinzani ni kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Ndugu
Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori huku akijua kuwa
Sarakikya alifanya makosa mengi katika utendaji wake wa kazi katika
idara hiyo ya Wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe pia
kuwa Ndg. Sarakikya ndiye aliyeongoza kikosi cha kuzuia ujangili hata
kabla ya operesheni tokomeza. Katika kipindi hicho, Tanzania ilishika
nafasi ya kwanza kati ya nchi nane duniani zilizoongoza kwa matukio ya
ujangili. Aidha, ili kuonyesha kwamba Serikali hii haizingatii weledi
katika utendaji, alietuliwa tena kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili.
2.2 Kauli Tata Za Serikali Juu ya Kufukuzwa Kazi kwa Wakurugenzi
Mheshimiwa Spika, mara baada ya
waziri kutangaza kuwavua nyadhifa zao wakurugenzi hao tarehe 24 Februari
2014, Katibu Mkuu wa wizara hii Bi. Maimuna Tarishi aliwarudisha kazini
wakurugenzi hao huku Serikali nayo kwa kupitia kurugenzi ya habari
maelezo,ikitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa taarifa za kufukuzwa
kwa wakurugenzi hao si sahihi. Pia, Ikulu kwa kupitia Katibu Kiongozi
Balozi Ombeni Sefue, ilitoa tamko la kuitaka Wizara kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu za utumishi wa umma za kumfukuza mtumishi kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu
Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Kifungu cha IV (23) (2)
inayozungumzia mamlaka ya Rais kumwondoa mtumishi aliyemteua kazini,
amri ya kumfukuza mtumishi wa umma itatekelezwa iwapo;
(a)hati ya mashtaka imeandikwa dhidi yake (b)mtumishi wa umma amepewa nafasi ya kujibu mashtaka hayo
(c)Maombi yametolewa kwenye hati ya mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizo chini ya kifungu namba 34.
Swali la kumuuliza Waziri
Nyalandu, je, hatua hizi zilifuatwa katika kuwasimamisha kazi
wakurugenzi hawa? Na je, maamuzi yake ya kumfukuza Prof. Songoro katika
vikao vya kamati na kumdhalilisha hata baada ya Ikulu kutoa maagizo ya
Wizara kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za kufukuza watumishi kazi ni
utawala bora?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali na Wizara kuhakikisha kuwa, uamuzi
wowote uliofanywa na kuendelea kufanywa katika kutekeleza maazimio ya
Bunge katika kuwawajibisha watumishi hao uzingatie sheria, taratibu na
kanuni kwa kuwa Sheria na Kanuni hizo zinaeleza wazi hatua zinazopaswa
kuchukuliwa. Vilevile, tunasikitishwa na mvutano baina ya waziri na
katibu mkuu wa wizara, hali ambayo inaonesha kuwa kuna mgongano aidha wa
kimaslahi na hivyo kuthibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa,
Waziri na Katibu Mkuu wa wizara moja wanafanya kazi bila kushirikiana na
kila mmoja akionekana kumvizia mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa
pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge lako tukufu.
Aidha, mvutano huu pia ni ishara
kuwa, maazimio ya Bunge yanaendelea kupuuzwa na Serikali kwa kigezo cha
kuzingatia sheria na kanuni huku zikiwaacha watumishi wenye tuhuma
wakihamishwa vitengo na idara na kuendelezea urasimu uleule hata uko
wanapohamishwa.
Mheshimiwa
Spika, ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi
mnafiki na debe tupu haliachi kutika (si maneno yangu, bali ya wahenga).
Si mara ya kwanza, kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhoji juu ya usafi wa
Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii, na mara kadhaa
tumeonesha kwa kiasi kikubwa udhaifu wake na kutoa vielelezo mbalimbali
vinavyotilia shaka utendaji wake kabla na hata baada ya kukabidhiwa
wizara hii nyeti!
3.0 TASWIRA YA TAIFA KATIKA JUMUIA ZA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu
Kambi Rasmi ya Upinzani imeendelea kutoa taarifa kwa Serikali juu ya
mtandao wa kimataifa wa ujangili ambao pia unahusisha viongozi
waandamizi wa Serikali, maafisa usalama wa taifa, wanajeshi
wafanyabiashara wakubwa, polisi, wanasiasa, Ikulu na watumishi wa umma.
Serikali ya CCM imekua ikitoa kauli za kubeza pamoja na majibu mepesi ya
tuhuma hizi huku tatizo la ujangili likiendelea kulichafua taifa katika
jumuia ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya
kushangaza baada ya gazeti la Mail on Sunday la nchini Uingereza kutoa
taarifa kuwa biashara ya ujangili inahusisha watu wa karibu na Rais
wakiwemo wanasiasa, maafisa wa Serikali na wafanya biashara wakubwa,
Serikali ilitoa matamko mbalimbali pamoja na kulaani taarifa ya gazeti
hilo na hatimaye Waziri Nyalandu, alimwalika mwandishi wa gazeti hilo
kujionea mwenyewe shughuli za Serikali za kupambana na ujangili ikiwemo
kutembembelea ghala ya kuhifadhia pembe za ndovu zilizokamatwa. Mwaliko
huo ilikua ni katika kuthibitisha kuwa Serikali ya CCM haina la kuficha.
Lakini katika hali ya kushangaza,
uchunguzi na taarifa zaidi umeonesha kuwa ndani ya miaka minane (8)
Serikali ya CCM, imekua ikiomba kibali bila mafanikio kutoka CITES
(Convention on International Trade on Endangered Species) cha kuuza
shehena ya pembe za ndovu takribani 34,000 zenye uzito wa tani 125 zenye
thamani ya dola za kimarekani milioni 150 sawa na shilingi Bilioni
244.5 za kitanzania (kwa wastani wa sh.1630 kwa dola 1).
Mheshimiwa Spika, jumuia ya
kimataifa imeshangazwa na kitendo cha Tanzania kuomba kibali cha kuuza
shehena iliyokamatwa ya pembe za ndovu kwa kuwa ni biashara haramu na
kitendo cha Serikali kuomba kuyauza ni sawa na kuchochea ujangili zaidi
kwa kuwa hali hii itaongeza uhitaji wa pembe za ndovu kwenye soko haramu
nchini China. Jambo hili ni aibu kubwa kwa taifa kuomba kufanya
biashara haramu kwa kuwa imelidhalilisha taifa. Hii ni sawa na Serikali
ikamate madawa ya kulevya, halafu iamue kuyauza ili kupata fedha.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha
waziri wa maliasili na utalii kumwalika nchini mwandishi aliyesemwa kuwa
ametoa taarifa za uongo na kulichafua taifa, ili ajithibitishie kuwa
Tanzania ni safi katika matukio ya ujangili, Bwana Martin Fletcher, na
kumtembeza katika sehemu mbalimbali nchini ikiwa na nia ya kumfunga
mdomo(damage control), haikusaidia bali ilivumbua uchafu mwingi na huu
wote umewekwa wazi katika vyombo vya habari vya kimataifa na kuendelea
kuonesha uozo wa Serikali katika kushughulikia tatizo la ujangili
nchini.
Mheshimiwa Spika, imeelezwa kuwa
Raisi ameshindwa kusimamia suala hili vizuri kwa kuwa wanaohusika na
ujangili ni watu wake wa karibu ama rafiki zake. Aidha, taarifa hizo
zimeendelea kubana kauli za Waziri Nyalandu za kuwa anawafahamu
majangili kwa majina na kuwataka majangili hao kuacha ujangili ama
watawachukulia hatua za kisheria. Maswali yanayoulizwa, je, ni kwa nini
waziri hawataji watu wanahousika na ujangili? Pili, inakuaje waziri
anawajua kwa majina na hata sehemu wanazokaa, lakini anashindwa
kuwachukulia hatua? Inakuaje waziri, awabembeleze watuhumiwa wakati kuna
sheria, kanuni na taratibu za kuwachukulia hatua wahalifu? Ni nini kipo
nyuma ya pazia katika kuwalinda na kuwaficha watuhumiwa wa ujangili?
3.1 Kukosekana kwa maafisa utalii katika balozi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kuna taarifa
kuwa katika balozi zetu mbalimbali na muhimu ulimwenguni kumekuwa
hakuna maafisa utalii ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa
wanaweza kuhakikisha kuwa tunapata watalii wa kutosha kwa ajili ya
kuinua pato la taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika ubalozi
wa Tanzania –Berlin ni kati ya balozi kubwa ulimwenguni ambao hauna
afisa utalii pamoja na ukweli kuwa ubalozi huu unahudumia nchi nyingine
za Poland,Austria,Hungary,Frankfut,Uswis,Romania,Bulgaria ,Slovakia na
Jamhuri ya Czech , kwa kipindi kirefu sana ubalozi huu umeomba kupatiwa
afisa utalii kutoka wizara ya mambo ya nje lakini mpaka leo hawajaweza
kupelekewa maafisa hao kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya
uchumi ambayo ndio msingi wetu wa diplomasia ya kimataifa .
Kambi ya Upinzani, inataka kupata
majibu ni lini serikali itawapeleka wataalamu hao katika ubalozi huu kwa
ajili ya kuimarisha sekta ya utalii kwenye nchi zote muhimu ambazo
zimekuwa mstari wa mbele katika sekta ya utalii katika taifa letu. [1]
4.0 BIASHARA HARAMU YA NYARA ZITOKANAZO NA WANYAMAPORI NA KUKITHIRI KWA TATIZO LA UJANGILI NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kumekuwa na ongezeko kubwa na watu
wanaojishughulisha na uwindaji na biashara ya nyara za Serikali bila
bila kuwa na kibali au leseni toka mamlaka zilizowekwa kisheria. Kwa
mujibu wa sheria ya wanyapori kifungu cha 80(1) sehemu ya 10 “mtu
yeyote haruhusiwi kujihusisha na biashara ya nyara (trophies) bila kuwa
na leseni ya biashara ya nyara (trophy dealer license). Na kifungu
cha 80(2) kinampa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori mamlaka ya kutoa
leseni ya biashara ya nyara kwa mtu yeyote ambaye ni raia wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania baada ya kupokea maombi kwenye fomu maalum na
kutimiza masharti yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kulipa ada
zilizopangwa.
Mheshimiwa Spika, leseni ya
biashara ya nyara inayotolewa katika Kifungu hiki haimruhusu mhusika
kuwinda, kuua au kupiga picha mnyama yoyote, badala yake inamruhusu
kukamata, kutengeneza bidhaa inayotokana na nyara, kununua au kuuza
nyara – 80(3)”[2].
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwepo
kwa sheria hiyo, bado wanyama wetu wanaendelea kuuwawa kwa kasi ya
ajabu. Aidha, kumekuwepo kwa taarifa zinazoonyesha kuwepo kwa mtandao
mpana wa wahusika wa biashara ya wanyama pori na bidhaa za wanyamapori
kutoka katika nchi kadhaa kama vile, Kenya, Msumbiji, DRC, Namibia na
Afrika ya Kusini.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa
maelezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu
aliyoyatoa mbele ya Waandishi wa Habari wakati akiwa Naibu Waziri wa
Wizara hii katika Hoteli ya Mount Meru – Arusha mwaka jana, ni kwamba;
kwa kipindi cha miaka mitatu, iliyopita tembo 31348 sawa na asilimia 42
walitoweka katika hifadhi ya Selous na Mikumi na kwamba kuna mtandao
wa kijangili wa kimataifa (Sophisticated International Syndicate)
unaofanya kazi hapa nchini. Aidha alitoa agizo kwa bodi ya wadhamini ya
mamlaka ya hifadhi za taifa (TANAPA) itoe maelezo ya kina kuhusu kuwepo
watumishi wa ndani ya mamlaka ya hifadhi wanaosadikiwa kushirikiana na
majangili hao kuendesha ujangili ambao unahatarisha hifadhi zetu na sifa
ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Waziri Nyalandu
aliirudia kauli hiyo mkoani Iringa, mwezi Juni, 2013 wakati wa kikao
cha siku mbili cha wadau wa ulinzi wa maliasili juu ya ujangili wa
tembo katika mikoa ya Nyanda za juu na kuahidi kwamba majina ya
majangili yakiwemo ya vigogo wanaojihusisha na ujangili wa tembo
yatatangazwa hadharani, lakini mpaka sasa hakuna majina yoyote
yaliyotangazwa hadharani.
Mheshimiwa Spika, utafiti
uliofanywa na Tanzania Wildlife Research Institute-TAWIRI katika mbuga
ya hifadhi ya Selou na Mikumi inaonyesha kuwa idadi ya Tembo imeshuka
kutoka 74,900 mwaka 2006 hadi kufikia 43,552 mwaka 2009. Hii ikiwa na
maana kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu takribani asilimia 42 ambayo
ni Tembo 31,348 katika hifadhi mbili tu waliuawa na majangili[3].
Hii ni hatari kubwa sana na kwa kutilia maanani kuwa Tembo mmoja
anapatikana baada ya miaka miwili (yaani Tembo hubeba mimba kwa kipindi
cha miaka miwili ndipo azae)
Mheshimiwa Spika, biashara haramu
ya nyara zitokanzao na wanyamapori hususan tembo imechangia sana
ujangili wa kutisha wa tembo kiasi kwamba idadi ya tembo imepungua mno
kiasi cha kuwafanya tembo wawe miongoni mwa jamii ya viiumbe waliopo
hatarini kutoweka kabisa (endangered species). Nasema hivi kwa sababu
idadi ya tembo kwa uchache, waliokuwepo katika nchi za Kiafrika kwa
miaka ya sabini walikuwa ni takribani milioni moja na laki mbili
(1,200,000) lakini kwa sasa wamebakia wasiozidi laki tano[4]
Mheshimiwa Spika, hali ya ujangili
nchini imefika pabaya na ina kiasharia kibaya kwa miaka michache ijayo.
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010, jumla ya tembo 10,000 waliuwawa
Tanzania, ikiwa ni sawa na wastani wa tembo 27 kwa siku. Mwaka 2012
pekee, tembo takribani 23,000 wameuwawa kwa mwaka ambayo ni sawa na
tembo 63 kwa siku. Hii ni sawa na ongezeko la 57% kwa kipindi cha miaka
2. Kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na tembo kati ya 150,000 na
170,000. Kutokana na takwimu hizi, ikiwa Tembo 63 wanauwawa kwa siku,
ni dhahiri kwamba kwa kipindi cha miaka 7 ijayo Tembo hawa watakuwa
wameuawa wote.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kupamba na madawa
ya kulevya na uhalifu (United Nation’s Office on Drugs and Crime-
UNODC-), inaonyesha kuwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na
nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ni wasambazaji wakubwa wa bidhaa
haramu za wanyamapori kwenye soko la China, Marekani na baadhi ya nchi
katika bara la Ulaya. Bidhaa hizo za wanyamapori ni pamoja na pembe za
ndovu, pembe za faru, ngozi za chui na simba na viungo mbalimbali vya
wanyamapori. Kwa mujibu wa utafiti huo ni kwamba mununuzi hulipa kiasi
cha dolla za kimarekani 2,500 kwa kila pembe moja ya faru.
Mheshimiwa Spika, tatizo la
Ujangili limekuwa gumu kumalizwa kabisa kwa kuna taarifa zinazohusisha
askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi katika matukio ya
ujangili na biashara haramu ya nyara na taarifa hizo zimeripotiwa sana
na vyombo vya habari, lakini cha kusikitisha ni kwamba hakuna hatua
zilizochukuliwa dhidi ya askari wa majeshi hayo (yaani jeshi la polisi
na jeshi la wananchi wa Tanzania). Mpaka sasa Jeshi la Polisi na Jeshi
la Wananchi wa Tanzania hawajakanusha taarifa hizo jambo linaloashiria
kwamba pengine taarifa hizo ni za kweli.
Mheshimiwa Spika, taarifa za baadhi ya askari walioripotiwa na vyombo vya habari kuhusika na ujangili ni kama ifuatavyo:
- Mnamo Tarehe 7 January 2013, Gazeti la habari leo lilitoa taarifa za askari wawili kujihusisha na biashara ya meno ya tembo na kuhusishwa na mauaji ya faru katika mbuga ya Serengeti na mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka Serikalini juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari hao.
- Mnamo Januari 20, 2013 Sajenti wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Azizi Athuman Yusufu alikamatwa mkoani Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu na bunduki aina ya Riffle yenye namba 458 huku akitumia gari ya mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe anayefundisha nchini.
- Tarehe 23 Julai, mwaka 2013, walikamatwa watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majangili , wakiwamo askari watatu wa Magereza Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wakiwa na gari la Magereza aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili STK 4394 lililokuwa limepakia nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55. Nyara hizo zilikuwa ni pamoja na Twiga wawili, Pundamilia wawili, Swala, Palapala majike wawili na Mbuni wawili.
Mheshimiwa Spika, Biashara haramu
ya pembe za ndovu imevuka mipaka ya nchi na imeanza kushamiri katika
ukanda wa Afrika ya Mashariki jambo ambalo linatishia kutoweka kabisa
kwa wanyama hao ambao ni kivutio kikubwa cha utalii. Taarifa katika
mtandao wa habari wa “Annamiticus” (www.annamiticus.com)
zinasema kwamba mwaka 2012, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania
yalikamatwa huko HongKong yakiwa yamebeba tani 4 (Kilo 4,000) za pembe
za ndovu.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa limeandikwa “plastic
scrap” ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya plastiki lakini baada ya
kufunguliwa kulikuwa na vipande 972 vya pembe halisi za ndovu zenye
uzito wa kilogramu 1,927 pamoja na kilo moja na nusu ya unga wa pembe za
ndovu zilizosagwa. Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa
“roscoco beans” yaani maharage aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa
kulikuwa na vipande 237 vya pembe za ndovu sawa na kilogramu 1,884.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
taarifa hiyo, wingi wa pembe hizi za ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha
kwamba tembo takriban 600 kwa uchache waliuwawa.
Mheshimiwa Spika, mwezi
Aprili,2013 kontena lingine lilikamatwa likiwa limesheheni pembe za
ndovu 113 huko China zenye thamani ya Dola za Kimarekani 400,000.Kontena
hili liliandikwa kwamba limebeba vipuri (spareparts) toka Burundi. Kwa
kuwa Burundi haina bandari, kuna uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo
lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo kuna uwezekano pia kwamba pembe
hizo zinatokana na tembo waliouwawa Tanzania.
5.0 MAENDELEO YA SEKTA YA WA WANYAMAPORI NCHINI
Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta ya wanyamapori katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu ni mkubwa sana. Takwimu[5]
zinaonyesha kuwa uwindaji wa kitalii kwa miaka mitatu kati ya 2009 na
2012 uliingiza shilingi bilioni 91. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Maliasili
na Utalii kupitia idara yake ya Wanyamapori inatakiwa kuilinda na
kuiendeleza sekta hii ili iendelee kuchangia zaidi katika uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, katika muktadha
wa kuilinda na kuiendeleza sekta ya wanyamapori, Bunge lilitunga Sheria
ya Uhifadhi ya 2009, ambayo inatumika pamoja na sera ya wanyamapori ya
mwaka 2007 ili kuratibu na kudhibiti shughuli za uwindaji wa
wanyamapori kwa namna ambayo sekta ya wanyampaori inakuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, ulinzi wa Sekta
ya wanyamapori ni muhumu kwa kuwa sekta inachangia ukuaji wa uchumi
katika Nyanja mbalimbali. Kwa mfano wanyamapori ni kivutio kikubwa cha
watalii ambao hutoa fedha nyingi za kigeni wajapo kutalii hapa nchini
kwa ajili ya kutazama na kuwapiga picha wanyama hao. Aidha sekta ya
wanyama pori inachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutoa ajira
kwa wananchi na pia kukuza soko la bidhaa za ndani.
Mheshimiwa Spika, licha ya umuhimu
wa sekta hii, Serikali imekuwa haifuatilii makampuni ya uwindaji yenye
leseni kuona kama wanafuata sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya 2009.
Matokeo ya udhaifu wa Serikali katika ufuatiliaji, kumekuwa na uvunjaji
mkubwa wa sheria jambo ambalo limesababisha uwindaji ufanyike kiholela.
Kwa mfano, Kampuni ya Uwindaji ya Green Miles Safaris Limited imekuwa
ikiwakimbiza na kuwakamata watoto wa wanyamapori pindi wanapozaliwa
kinyume na kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Wanyamapori ya 2009. Aidha
Sheria hiyo inapendekeza adhabu ya kifungo cha miaka mitano gerezani na
au faini kati ya shilingi 500,000/= hadi shilingi 2,000,000/=
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inataarifa kwamba Kampuni hii ya Green Miles Safaris Limited
ilishapewa zuio na Mahakama la kufanya uwindaji kutokana na uwindaji
usiozingatia sheria lakini Kampuni hiyo ilipita mlango wa nyuma na
kuomba kilbali cha uwindaji kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori na Mkurugenzi
akatoa kibali na hivyo wote wawili wakapuuza uamuzi wa Mahakama.
Mheshimiwa Spika, Kampuni hii ya
Green Miles Safaris Limited, pamoja na uhalifu mwingi inaoufanya katika
mbuga zetu wakati wa uwindaji, imekuwa ikilindwa na Serikali ndio maana
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Upinzani Bungeni inashawishika kuamini
kwamba Serikali ndio chimbuko la tatizo la Ujangili na uwindaji haramu
wa wanyamapori hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo mbele ya bunge hili ni kwa nini
haijaichukulia Kampuni ya Uwindaji Green Miles kwa kufanya uwindaji
haramu hapa nchini?
Mheshimiwa Spika, Tatizo kubwa la
Maendeleo ya Sekta ya Wanyapori ni kwamba Serikali huwa haifuati hata
mapendekezo yanayotolewa na Kamati za zinazoudwa na Serikali yenyewe.
Kwa mfano, mwaka 2006, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa
wakati huo Mheshimiwa Anthony Mwandu Diallo (Mb), aliunda Kamati ya
Wataalam ambayo aliitaka ifanye uchambuzi wa kina wa shughuli za
uwindaji wa kitalii nchini. Uchambuzi huo ulitakiwa uzingatie utendaji
kazi katika shughuli za uwindaji wa kitalii, mafanikio yaliyofikiwa
mpaka sasa na matatizo yanayoikabili tasnia hiyo. Hatimaye, Kamati
ilitakiwa kumshauri Mheshimiwa Waziri namna ya kuleta mabadiliko ndani
ya sekta hiyo kwa minajili ya kulinda uhifadhi, kuwawezesha wananchi
kushiriki katika uwindaji wa kitalii kwa lengo la kuongeza ufanisi na
tija ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuondoa umaskini na
kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Hadidu za rejea kamati hiyo ilizopewa ziliitaka Kamati:[6]
(i)
Ipitie utaratibu wa sasa wa uombaji na ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji
wa Kitalii pamoja na chombo chake cha ugawaji kuona kama havibagui wala
havisababishi malalamiko kwa wadau mbalimbali;
(ii)
Ichambue kwa makini vigezo na masharti yaliyopo yanayohusu ukaguzi wa
uwezo wa Kampuni za Uwindaji zinazowasilisha maombi kwa ajili ya
Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama yanafaa kwa mazingira ya sasa;
(iii)
Ichambue Mikataba mbalimbali ya kampuni za uwindaji; ya zamani na
inayoendelea kwa lengo la kujiridhisha kama inafaa au ina upungufu
unaohitaji marekebisho ili kulinda uhifadhi na maslahi ya umma.
(iv)
Iangalie Kanuni za Uwindaji wa Kitalii na zile za Utalii wa picha
pamoja na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 na kushauri namna ya
kuondoa migongano ambayo imejitokeza baada ya kuruhusu utalii wa picha
kwenye maeneo ya uwindaji wa kitalii.
(v)
Ichambue Sera na Sheria zinazohusiana na Wanyamapori na Utalii, na
Kanuni za Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama Wananchi wanafaidika na
uwindaji huo wa kitalii.
(vi)
Ichambue utaratibu wa ukusanyaji mapato, kubaini njia ambazo zitaongeza
maduhuli ya Serikali, na kutathmini utaratibu wa ugawaji vitalu kwa
njia ya zabuni.
(vii)
Mwisho, Kamati iangalie uwezekano wa Serikali kuwawezesha Wananchi
kushiriki kikamilifu katika tasnia hii ya uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Kamati hiyo yalikuwa ni kama ifuatavyo:
- Kuboresha utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa kuipa Kamati ya Ugawaji Vitalu nguvu za kisheria na kwa kupanua uwakilishi wake.
- Kuunda Wakala wa Serikali wa kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii badala ya Idara ya Wanyamapori.
- Kuangalia upya umiliki wa vitalu ili kuwawezesha wananchi kushiriki zaidi katika uwindaji wa kitalii kwa njia ya ubia na baadaye kumilikishwa vitalu wakati wageni na wananchi watafanya kazi ya kuwindisha.
- Serikali iwawezeshe Wawindaji Bingwa wa Kitanzania ili waweze kumiliki vitalu na kutumia ujuzi na uzoefu walionao. Serikali inaweza kuwawezesha wananchi kwa kuzungumza na mabenki ili wapunguze riba ya kukopa fedha benki na kuruhusu matumizi ya vitalu kama dhamana. Pia wawindaji bingwa waanzishe bodi yao ya kitaalam.
- Kuthamini vitalu vya uwindaji wa kitalii na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato ya Serikali.
- Kuweka ukomo wa umiliki wa kitalu wa vipindi viwili vya miaka mitano ili ili kuruhusu waombaji wapya.
- Kuboresha taarifa za sekta ya Wanyamapori kwa kuweka taarifa zote muhimu zinazohusu shughuli za uwindaji wa kitalii kwenye Tovuti ya Idara.
- Idara iimarishe ufuatiliaji na tathmini ya vitalu kwa kuanzisha chombo huru cha kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa kiwango
gani mapendekezo ya Kamati hiyo yametekelezwa na ni mangapi ambayo
bado kutekelezwa na ni kwanini?
6.0 UTALII NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA
Mheshimiwa Spika,
Kwa eneo kubwa la ardhi
lililofunikwa na wingi wa misitu pamoja na aina mbalimbali za maua na
viumbe, Tanzania ni mojawapo ya vivutio vikubwa vya utalii barani
Afrika. Nchi yetu ina raslimali nyingi asilia ikiwemo pamoja na maeneo
mengi ya nyika za mapori yenye aina nyingi za banoai.
Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa
vivutio vya utalii ni pamoja na Mbuga za wanyama , hifadhi za taifa,
hifadhi zilizozuiliwa na maeneo ya kihistoria. Hata hivyo kwa sababu ya
ongezeko la joto, baadhi ya hivi vivutio ikiwemo theluji katika kilele
cha mlima Kilimanjaro iko katika hatari ya kupotea. Na baadhi ya wanyama
katika mbunga zenye ukame mkubwa wameanza kupungua na kuathirika.
Mheshimiwa Spika, Licha ya kuwa na
neema ya kuwa na vivutio vingi vya utalii, bado sekta ya utalii
inakabiliwa na chamgamoto kadhaa, zikiwa ni;
(i) Uendelezaji wa kazi
zitakazohakikisha kuendelea kuwepo kwa vivutio mbalimbali vya utalii kwa
kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi;
(ii) Ukarabati wa miundombinu kama
vile barabara, madaraja, kambi za watalii na upatikanaji wa umeme kwa
ajili ya watalii wa mbugani;
(iii) Uwezo
mdogo wa idara zinazohusika kusimamia, kulinda vivutio vya utalii, kama
vile kuendesha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani, inaamini kabisa tatizo la umeme katika vivutio vya utalii
vilivyopo mbugani, suluhisho ni kutumia umeme wa jua (solar energy),
hili ni rahisi katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo
nitaonyesha hapo baadae makusanyo yanayopatikana kutoka sekta ya utalii
hayana uwiano wa moja kwa moja na uwekezaji katika sekta hiii. Ndiyo
sababu kubwa ya mapato ya sekta kutokuakisi vivutio tulivyonavyo hapa
nchini.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika
Sekta ya Utalii ni suala lenye tija kubwa katika uchumi wetu kwa kuwa
sekta hiyo imekuwa ikichangia katika uchumi wa Taifa licha ya uwekezaji
mdogo uliofanyika katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo
zinaonyesha kuwa katika maeneo yote ya hifadhi zetu kwa sasa kuna
kuna hoteli zenye uwezo wa kutoa huduma za malazi (carrying capacity)
kwa watu 6,681 ambapo kwa miaka mitano ijayo idadi hii itafikia uwezo
wa kulaza watu 8,421. Hiki ni kwango kidogo sana cha huduma za malazi
kiasi kwamba tunapoteza fursa ya kunufaika katika sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, japokuwa
uwekezaji katika sekta ya utalii ni mdogo lakini sekta imeendelea kuwa
nguzo muhimu katika uchumi wetu. Kwa mwaka 2011 utalii na usafiri wa
kitalii ulichangia asilimia 13 kwenye pato la taifa na kuchangia
takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni. Aidha, Mpango unaeleza kuwa
lengo ni kuongeza wageni kwa asilimia 40 kutoka wageni 671,886 kwa
sasa hadi 940,640 ifikap June 2016. Aidha Mpango unalenga pia kuzidisha
siku za mtalii kutembelea maeneo yenye vivutio vya kitalii nchini kutoka
siku wastani wa siku 11 za sasa hadi wastani wa siku 18[7].
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kutoa tathmini ya mpango huo ili wananchi
wajue tumefanikiwa kwa kiwango gani katiaka kuboresha sekta ya
wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, miundombinu ya
usafiri na usafirishaji ya ndani ya nchi, uwekezaji katika ujenzi wa
hotel kwenye maeneo muhimu ya utalii kama vile kwenye hifadhi, mikoa
inayozunguka mlima Kilimanjaro kutasaidia sana kuvutia watalii. Hivyo
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuboresha miundo mbinu ya
usafiri hasa wa anga ili na kujenga hoteli za viwango vya Kimataifa
katika maeneo yenye vivutio vya watalii ili kuvutia mashirika ya mengi
ya ndege toka nje kuja hapa.
Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani
kwa Serikali kwamba ifufue shirika letu la Ndege la Taifa ili tuweze
kumudu ushindani katika usafiri wa anga na hapohapo kuongeza idadi ya
watalii katika nchi yetu. Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na ule wa
Julius Nyerere Dar es Salaam vikiboreshwa vinaweza kuwa ni kitovu cha
mashirika mengi ya kimataifa kubadilishia wasafiri kama kuna mkakati
makini.
Mheshimiwa Spika, watalii toka nje
wanapenda sana kupanda ndege za nchi wanazotembelea zaidi kuliko
kupanda ndege za kuunganisha. Kwa njia moja au nyingine usafiri huo
unawapunguzia gharama. Mfano mzuri ni miaka ya themanini wakati
Air-Tanzania ilipokuwa inafanya safari zake nchi za Ulaya, watalii wengi
walikuwa wanakuja kwa ndege zetu. Hoja ni kwamba Serikali ina mkakati
gani wa kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATC) Kambi Rasmi ya Upinzani
inapendekeza Serikali kuingia ubia na makampuni binafsi kupitia mpango
wa Private Public Pertnership – ( PPP) ili kuboresha huduma za usafiri
wa anga hapa nchini ambao unachoche watalii wengi kuja kwa kuwa kuna
usafiri wa moja kwa moja.
7.0 SEKTA YA MISITU
Mheshimiwa Spika, misitu ina
nafasi muhimu ya kumeza hewa ukaa duniani wakati ikizuia uharibifu wa
udongo/ardhi. Ukataji miti na uondoaji misitu uliokithiri unachangia
katika ongezeko la uzalishaji wa hewa ukaa Tanzania. Kupitia misitu
mingi tuliyonayo Tanzania imeendelea kutoa huduma ya kumeza hewa ukaa
duniani, bila ya kuwepo utaratibu wowote wa kimataifa kutoa fidia
yoyote.
Mheshimiwa Spika, mbali ya kuwa na misitu mingi, kumekuwepo na changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya misitu, nazo ni:
a) Kufanya uendelezaji wa misitu kama raslimali ya kumeza hewa ukaa na kuinufaisha jamii inayoizunguka;
b) Kuthibiti ubora na uendelevu wa misitu
c) Jamii inayoizunguka misitu kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani;
d) Ujenzi wa uwezo wa kufanya tafiti za uendelezaji misitu nchini;
e) Uendelezaji wa njia bora zinazowezesha jamii inayozunguka misitu kunufaika na raslimali hiyo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
changamoto hizo, zinazoikabili sekta hii ya misitu, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka kuhakikisha kwa kadri misitu ya Tanzania inavyoendelea
kutoa huduma ya kimataifa ya kumeza hewa ukaa duniani, hivyo ni lazima
nchi na wananchi wetu tunufaike kwa kupata kazi na teknolojia
zinazochangia maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo
ni kwamba, ni muhimu Serikali kuhakikisha unajengwa uelewa kwa jamii na
wadau wa misitu juu ya uwepo wa fursa za kutumia uwezo wa misitu kumeza
kumeza hewa ukaa kama chanzo cha kunufaika na biashara ya hewa ukaa
duniani. Kuhamasisha ongezeko la matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati
ya kupikia na kuchemshia na kupunguza msongo kwenye misitu yetu kwa
hitaji hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inasema kuwa katika kuhamasisha hilo, ni muhimu kuwepo kwa
misitu mfano na miradi mfano katika ngazi za wilaya na vijiji ili
wananchi waone jinsi misitu inavyoweza kuwanufaisha wananchi
wanaozunguka misitu mfano hiyo. Hili linawezekana kama mipango na
umakini katika utekelezaji wake utakuwepo.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika
kilimo cha miti ni mojawapo ya kilimo ambacho kwa muda mrefu kinaweza
kuleta tija kubwa kwa wananchi hasa hapa nchini, uwekezaji huu
unakabiliwa na chamgamoto kubwa ya kukosekana kwa mikopo ya muda mrefu
na ambayo inaweza kuwa-accommodate wakulima ambao hawana dhamana ya
kuweka zaidi ya umiliki wa kimira wa ardhi husika, jjambo ambalo
halikubaliwi na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huu wa
kilimo cha miti ni maarufu sana katika mikoa ya Iringa na Njombe, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni utaratibu gani
hadi sasa ambao wakulima wadogo hasa wa miti wanasaidiwa kupata mikopo
ya muda mrefu katika kukabiliana na tatizo hili la uwepo wa hewa ukaa na
kuongeza kipato.
8.0 MAPITIO YA BAJETI KWA IDARA NA VITENGO VYA WIZARA
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa
fedha 2013/14 wizara ilitarajia kukusanya maduhuli ya jumla ya shilingi
bilioni 148.97 kutoka katika Idara na taasisi zilizo chini yake. Mwaka
huu wa fedha wizara inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni
144.6, ambayo ni pungufu ya shilingi bilioni 4.37 kwa kulinganisha na
makadirio ya mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, randama
inaonyesha kuwa Idara ya wanyamapori kwa kipindi cha mwaka 2013/14 ili
kadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.65, Lakini hadi mwezi
Machi, 2014 ilikuwa imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 8.92 ambayo ni
sawa na asilimia 31.13 ya malengo. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2014/15
Idara ya Wanyamapori imepanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 15.55
kutoka kwenye vyanzo vyake vilivyo chini ya idara. Makadirio haya ni
pungufu ya shilingi bilioni 13.1 kwa kulinganisha na mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo
ni kwamba Sekta ya Maliasili na Utalii inashuka kimapato. Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza sababu zilizofanya mapato
yatokanayo na makusanya ya maduhuli kwa shuka kwa kiasi kikubwa namna
hiyo. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na taarifa ya
uchunguzi maalum ni kwamba kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2012
Idara ilikusanya shilingi bilioni 91 na hali halisi ni kwamba uwezekano
kukusanya zaidi ni mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi
ya kawaida, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 19.163 kwa
ajili ya matumizi ya Idara hiyo, ambayo ni sawa na asilimia 22.7 ya
makusanyo yake. Lakini hadi mwezi machi 2014, Serikali imetoa kiasi cha
shilingi bilioni 9.161 tu. Swali hapa ni kwamba idara itawezaje
kujiendesha ikiwa fedha iliyotolewa ni kidogo namna hiyo? Ikumbukwe
kwamba Idara hii inasimamia taasisi/vyuo na wakala zipatazo sita ambazo
ni TANAPA, NCAA, TAWIRI,CAWM-Mweka, PWTI na CBCTC ambazo zinahitaji
fedha za kutosha kuziendesha.
Mheshimiwa Spika, fedha za
maendeleo zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenye sekta ya
wanyamapori, ni kwa miradi miwili tu ambayo ni mradi wa KILORWEMP
unaotekelezwa kwa ushirika kati ya Tanzania na Serikali ya Ubelgiji.
Mwaka 2013/14 zilitengwa jumla ya shilingi bilioni 1.82, lakini hadi
Machi 2014 shilingi milioni 310 ambazo zilitoka Serikali ya Ubelgiji.
Mheshimiwa Spika, mradi wa pili ni
ule wa Kulinda ushoroba wa Selous-Niassa, ambao unatekelezwa kwenye
wilaya za Namtumbo na Tunduru kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani.
Kwa mwaka jana hakuna fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa
fedha 2013/14 Idara ya Utalii ilikadiriwa kukusanya jumla ya shilingi
bilioni 16.896 lakini hadi mwezi mach, 2014 ilikuwa imekusanya shilingi
bilioni 3.25 ambayo ni sawa na asilimia 19 tu ya matarajio kwa mwaka.
Aidha, fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida kwa idara
na Taasisi zilizo chini yake ni shilingi bilioni 12.1, lakini hadi
Machi, zilikuwa zimetolewa shilingi bilioni 3.36.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha
2014/15 idara hii ya Utalii inatarajia kukusanya jumla ya shilingi
bilioni 16.91. Aidha, kwa maendeleo Iadara hii imetengewa jumla ya
shilingi bilioni 1.2. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza inakuwaje Idara
inakusanya shilingi bilioni 16.91 lakini uwekezaji unakuwa wa shilingi
bilioni 1.2, aidha uwekezaji huo hauna matokeo ya moja kwa moja na
ukuaji wa utalii. Je ni kwa vipi katika Dunia hii ya ushindani katika
sekta ya utalii inaweza kuleta tija na kuinua uchumi?
9.0 HITIMISHO
Kambi Rasmi ya Upinzani,
haitochoka kuikosoa Serikali kwa kuwa, kwa muda mrefu sasa katika Wizara
hii tumekua tunatoa mapendekezo ambayo yanabezwa. Na kwa kuwa ni wajibu
wetu kuisimamia ipasavyo Serikali ya CCM, tunazidi kusisitiza kuwa ili
sekta ya maliasili na utalii iendelee kuna haja nzima ya kubadilisha
mfumo wa usimamizi, uendeshaji na utekelezaji wa Wizara, ambao utatoa
fursa kwa viongozi waandamizi wa Wizara pamoja na watumishi kutimiza na
kutekeleza majukumu yake bila mashinikizo ya kisiasa.
Ni rai yetu kuwa, Serikali
itayafanyia kazi mapungufu yote ambayo tumekua tukiyasema kwa muda mrefu
sasa na kuisimamia ipasavyo sekta hii hili iwe mhimili wa uchumi kwa
taifa kwa kuongeza mapato pamoja na kutoa nafasi za ajira kwa wananchi
wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
…………………………………………..
Mch. Peter S. Msigwa (MB)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Maliasili na Utalii.
13.05.2014
[1] ripoti ya CAG 2012/2013 pg 148.
[2] Sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009
[3] www.reuters.com/video/feuters-tv
[4] Haken, J. (2011), “Transnational Crime in the Developing World” in the Global Financial Integrity Journal of February, 2011.
[5] Ripoti ya CAG-ukaguzi wa ufanisi na ukaguzi maalum kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Machi, 2014
[6]
Wizara ya maliasili na utalii- Taarifa ya kamati kuhusu
uboreshaji wa tasnia ya uwindaji wa kitalii Tanzania, JUNI, 2006
[7] Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011 – 2016
Post a Comment