Viumbe hai vinavyotumia maji katika ziwa Manyara
lililopo ndani ya mbuga ya Hifadhi ya Taifa ya Manyara wakiwemo ndege aina ya
korongo huenda wakatoweka kwa kufa kufuatia kunywa maji yanayodaiwa kuwa na
kemikali yenye sumu ambayo hutiririka katika ziwa hilo kutoka katika mito
inachimbwa na kuchekechwa madini ya dhahabu.
Mbali ya athari kwa ndege hao ambao ni kivutio
kikubwa cha watalii katika mbuga hiyo pia madhara mengine huenda yakawakuta
walaji wa samaki wanaovuliwa katika ziwa Manyara.
Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Manyara, Yustina Kiwango
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ndege aina ya korongo ni kivutio kikubwa
cha watalii katika mbuga hivyo jitihada za ziada zinahitaji kuhakikisha
kemikali hizo zinadhibitiwa zisiweze kuingia kwa wingi katika ziwa Manyara.
Kiwango alisema katika ziwa Manyara kuna vyakula
muhimu sana ambavyo hupendwa na ndege hao hivyo sio rahisi kuzuia ndege hao
kunywa maji hayo kufuatia kuwepo kwa kemikali hizo ambazo zipo katika madini
aina ya dhahabu yanayochekechwa katika mbuga hiyo.
Alisema wachimbaji wadogo wadogo wenye leseni halali
zilizotolewa na wizara ya Nishati na Madini huchimba madini ya dhahabu
ndani ya hifadhi ya Manyara katika mito ya Magara na Giheri na maji yenye
kemikali zenye suma huingia katika ziwa Manyara na kuua viumbe hai wakiwemo ndege
na samaki na pia mlaji naye huathirika.
Mbali ya kutojua kiwango rasmi cha ndege waliokufa
mpaka sasa, Mhifadhi huyo alisema utafiti unaendelea kujua idadi yao, lakini
jitihada za ziada zinahitajika kuelimisha jamii juu ya hali hiyo ili
ndege, samaki na viumbe wengine waliopo ndani ya ziwa hilo wasiweze kufa na
hatimaye kutoweka kabisa.
Mhifadhi huyo aliomba wadau wote kwa kushirikiana
kwa pamoja na Wizara ya Utalii na Maliasili, Nishati na Madini,Wizara ya
Ushirika na Kilimo na Mifugo kulichunguza suala hilo kwa kina na kulipatia
ufumbuzi kabla ya kuleta madhara zaidi kwa ndege hao muhimu kwa utalii.
Alisema mbali ya hilo pia uchimbaji huo hupeleka
tope jingi katika ziwa Manyara na kufanya kina cha ziwa hilo kwa sasa kuwa mita
moja badala ya mita 4 kama ilivyokuwa miaka 50 iliyopita.
Kiwango alisema na kuomba wadau wote kudhibiti hali
hiyo na kama hilo halitafanyika upo uwezekana mkubwa wa ziwa Manyara kutoweka
hivyo aliiomba wizara ya nishati na madini kuacha kutoa leseni mpya za
uchimbaji madini ndani mbuga hiyo pindi zinapokwisha ama kutoa leseni mpya.
‘’Hapa
tunapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kudhibiti kemikali zisiendelee kwenda
ziwa Manyara kwani zitaua kwa wingi ndege aina ya flamingo na viumbe hai
wengine waliopo katika
Ziwa Manyara.’’
‘’Kuongezeka kwa tope katika ziwa hilo nalo ni
tatizo lingine ambalo nalo linapaswa kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa hivyo
jitihada za ziada zinahitajika kwa wizara na sekta nyingine kukomesha hali
hiyo’’alisema Kiwango
Mhifadhi alitaja miji itayoathirika na hali hiyo ni
pamoja na Oltukai, Esilalei, Mto wa Mbu, Makuyuni na Minjingu kwani kwa
asilimia kubwa hufaidika na ziwa hilo.
Post a Comment