Mgahawa maarufu jijini Dar es Salaam
unaozunguka juu ya jengo la Golden Jubilee lenye zaidi ya ghorofa 20,
umekamatwa kwa kukwepa kodi baada ya kuacha kutumia Mashine ya Kodi ya
Kielektroniki (EFDs) licha ya kuwa nayo.
Kutokana
na hali hiyo, wamiliki wa mghahawa huo, wametozwa faini ya Sh milioni tatu kwa
kuwa ni kosa la kwanza na iwapo watabainika kuendelea kukwepa kodi,
watafikishwa mahakamani na hatimaye kufungiwa biashara.
Maofisa
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jana mchana walifika katika mgahawa huo
uliopo katikati ya Jiji wakiwa na risiti za kielektroniki zenye jina la Akemi,
wanazotoa badala ya zile za TRA na kuuonyesha uongozi wa hoteli hiyo.
Naibu
Kamishna wa Idara ya Kodi za Ndani, Generosa Bateyunga, alisema walipata
taarifa kutoka kwa wateja wa mgahawa huo, kupewa risiti zao na siyo za TRA
ambazo walikuwa wamepata huduma za Sh 175,000.
“Ndipo
tuliamua kuwatuma wafanyakazi wetu ambao walilipa na kupewa risiti ambayo siyo
ya TRA, na walipojitambulisha walipewa risiti halali, jambo linaloonyesha kuwa
wanayo mashine lakini hawatumii kwa wateja wote na hiyo ni kukwepa kodi
makusudi,”alisema.
Alidai
mgahawa huo unatoa risiti za kielektroniki zenye jina la mgahawa, lakini siyo
za TRA, kwani risiti halali ni zenye nembo ya Mamlaka, jina la Mmiliki, Anuani
na mengineyo. Alidai kati ya wateja 10, wanaowapa risiti za TRA ni mmoja.
Alisema
mgahawa huo ni kati ya michache yenye viwango vya juu kutokana na kuzunguka, na
mlipakodi mkubwa aliyesajiliwa katika orodha ya wafanyabiashara wanaolipa Kodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT) hivyo ni lazima itoa risiti za TRA.
Akizungumzia
suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Alcove group ambao ni wamiliki wa mgahawa huo,
Sanjay Kanabar, alisema alisaini barua ya kupokea taarifa ya kulipa faini,
lakini siyo kweli kwamba hawatoi risiti za TRA, bali inatokana na kusumbua kwa
mtandao.
Alisema
risiti zao wanazotoa ni kwa ajili ya kumpa bili mteja, lakini mtandao ukikataa,
wanawapa kama risiti jambo ambalo wameishatoa taarifa mara kadhaa kwa kampuni
iliyowauzia mashine hiyo.
Post a Comment