Rais
Jakaya Kikwete amemteua, Rished Bade kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA).
Taarifa
ya uteuzi huo imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue.
Kwa
mujibu wa Balozi Sefue uteuzi huo unaanza Mei 6, mwaka huu akichukua nafasi
iliyoachwa wazi na Harry Kitilya ambaye alistaafu Desemba 14, 2013.
Kabla
ya uteuzi huo, Bade alikuwa Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na
kukaimu nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania toka Kitilya
alipostaafu.
Kamishna
huyo mkuu mpya ana Shahada ya Kwanza ya Biashara na Menejimenti ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (1995); Shahada ya pili ya Biashara, Fedha na Benki ya Chuo
Kikuu cha Sydney (1999), pia ni Mhasibu aliyethibitishwa na Bodi ya Wahasibu
(CPA).
Wakati
huo huo Rais Kikwete juzi amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu
wa China, Li Keqiang.
Rais
alikutana na Waziri Mkuu huyo katika Hoteli ya Transcorp Hilton ya mjini Abuja
nchini Nigeria ambako wote wawili wamefikia wakati wanashiriki Kongamano la
Uchumi Duniani Afrika (World Economic Forum -Africa).
Taarifa
ya Ikulu inasema kwamba viongozi hao wawili wamezungumzia, kimsingi, mambo
yanayohusu uhusiano wa Tanzania na China.
Katika
mkutano huo, Rais Kikwete amemuomba Li Keqiang kuisaidia Tanzania kuboresha
mfumo wake wa kutunza na kuhifadhi nafaka kutokana na ongezeko kubwa la
uzalishaji wa nafaka, ambao unatokana na kukua kwa kilimo cha
Tanzania.
Waziri
Mkuu Li Keqiang amekubali ombi hilo la Tanzania.
Rais
Kikwete pia amemwomba Waziri Mkuu huyo wa China kusaidia kuhakikisha kuwa kazi
ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo inaanza mapema iwezekanavyo, ombi ambalo
Waziri Mkuu Li Keqiang pia amelikubali.
China
ni moja ya wawekezaji wakuu katika uchumi wa Tanzania kwa kiasi cha dola za
Marekani bilioni 2.5.
Post a Comment