
Maelezo –Zanzibar 20/5 2014
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar
imetakiwa kutoa elimu kwa wananchi ili kujua umuhimu wa utalii nchini na
kuhakikisha kuwa sekta hiyo inatoa huduma iliyobora na kuimarisha
uchumi wa Taifa.
Akiwasilisha Ripoti ya Kamati ya
Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuhusu Hali ya Uchumi na
Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015 Mwenyekiti wa Wenyeviti Hamza
Hassan Juma amesema ni muhimu kwa Serikali kuimarisha ulinzi kwenye
maeneo yote ya utalii na kuondosha vitendo vya uahalifu ili kuhakikisha
kuwa sekta hiyo inaimarika.
Amesema ipo haja Serikali
kuimarisha miundombinu itakayowawezesha watalii kupata huduma bora
wanapoingia nchini ikiwemo kuimarisha viwanja vya ndege, bara bara,
kuongeza vivutio vya utalii na maeneo ya kutembezea watalii, kuweka miji
katika hali ya usafi pamoja na kuimarisha ulinzi.
“Kwa kuwa nchi yetu inategemea
zaidi mapato yake kutokana na utalii, bado hatujaekeza ipasavyo katika
kutoa taaluma ya kutosha kwa ngazi zote, Chuo chetu cha Utalii
hakijaweza kutoa Shahada kwa wahitimu jambo linalosababisha nafasi za
juu katika ngazi ya ajira kuchukuliwa na wageni na vijana wetu kubakia
katika ngazi za chini”, alieleza Mhe. Hamza.
Aidha Kamati hiyo imeitaka
Serikali kudhibiti ujenzi uanaoendelea maeneo ya Mjimkongwe kwani
umeanza kupoteza uasilia wa majengo yake kwa kujengwa majengo ya kisasa
jambo ambalo linaweza kuiondoa Zanzibar kwenye miji yenye Urithi wa
Kimataifa.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo ameomba
Serikali kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuyalinda maeneo
yote ya kilimo pamoja na kuyaongezea wigo wa ruzuku na pembejeo kwa
mazao ili kuwahamasisha wakulima kuongeza kilimo na kupunguza nakisi ya
uagizaji chakula kutoka nje.
“Pamoja na Serikali kueleza kuwa
uchumi wetu unatarajia kuimarika katika mwaka ujao kwa kuimarisha
mazingira mazuri ya biashara lakini suala hili inabidi kutekelezwa kwa
vitendo na sio kwa maneno ya kwenye vitabu tu kwa kupunguza urasimu kwa
wawekezaji hasa wazalendo kwa kuwaondolea vikwazo wanapoamua kuwekeza”,
alifahamisha.
Akizungumzia mpango wa maendeleo
wa Bajeti, Mh. Hamza ameitaka Serikali kuimarisha huduma za Hospitali
za Mjini na Vijijini ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja ambayo
ndio kimbilio la wananchi wengi wa Zanzibar
Ameeleza kuwa Hospitali Kuu ya
Mnazimmoja, pamoja na kuwa na madaktari bingwa wa fani tofauti, imekuwa
ikipokea wagonjwa wachache wanaotumia Bima ya Afya ukilinganisha na
Hospitali za binafsi.
Amesisitiza kuwa Kamati yake
imeitaka Benki ya Watu wa Zaznibar (PBZ) kuanzishe huduma ya kadi ya
VISA na Master ili kuwa na wigo mpana wa kutoa huduma zake.
“Benki ya Watu wa Zanzibar
wakianzisha huduma hii itaweza kuwavutia wateja wengi hasa wale
wakumbwa ambao wengi wao ni wafanya Biashara, ”alisema Hamza.
Hamza Hassan amesema kwa upande
wa mapato imebainika kuwa Taasisi zinazokusanya mapato huwasilisha fedha
zote katika mfuko mkuu wa hazina jambo ambalo hupelekea Taasisi hizo
kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao kutokana na uhaba wa fedha
wanazopatiwa
Kutokana na hali hiyo, amesema
kamati yake inazishauri Serikali kuzipatia Taasisi hizo aslimia ya
makusanyo yake ili ziweze kutekeleza changamoto zinazowakabili.
“Tunaomba Taasisi kama hizo, aidha
zipangiwe utaratibu wa kupatiwa asili mia fulani yaani Retaintion ili
ziweze kujimarisha na kujenga uwezo wa kukusanya zaidi ili kuongeza
mapato ya Serikali”,alisema Hamza Hassan.
Ameisisitiza kwa Serikali
kufuatilia kwa karibu ukusanyaji wa mapato ya Taasisi inazozipa ruzuku
kwa lengo la kujipunguzia mzigo kwa zile Taasisi ambazo zina uwezo wa
kujitegemea.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Post a Comment