Wassira alisema hayo juzi alipokuwa akiwasilisha Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha wa 2014/15.
Alisema mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya
elimu ni kuongezeka kwa ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne kutoka
asilimia 43.08 mwaka 2012 hadi asilimia 58.25 mwaka 2013.
“Ngazi ya elimu ya msingi ufaulu umeongezeka
kutoka asilimia 31 mwaka 2012 hadi asilimia 50 mwaka 2013. Tumeongeza
maabara katika shule za kata, kuanza ukarabati wa shule kongwe za
kitaifa na kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika shule 56 kati ya 264
za awamu ya kwanza,” alisema.
Katika kilimo, alisema mafanikio ni kutoa mafunzo
ya kuendesha skimu ya umwagiliaji kwa maofisa 95 na wakulima 95, kupata
hatimiliki za mashamba makubwa mawili ya Bagamoyo na Mkulazi (Rufiji),
kutoa hati za kimila kwa mashamba madogo 185 na kutoa mafunzo kuhusu
biashara.
Wassira alisema katika nishati mafanikio
yaliyopatikana ni wateja wapya 138,931 kuunganishiwa umeme
ikilinganishwa na lengo lililowekwa la kuwaunganishia wateja 150,000 kwa
mwaka 2013/14.
“Tumepunguza upotevu wa umeme kutoka asilimia 21 mwaka 2012 hadi asilimia 19 mwaka 2013,” alisema.
Katika sekta ya uchukuzi, Wassira alisema Serikali
imeongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuhudumia zaidi
ya tani milioni 13, Desemba mwaka jana, ikilinganishwa na tani milioni
12, Desemba mwaka 2012.
“Katika Reli ya Kati, Serikali imekamilisha ujenzi
wa madaraja matatu, uundwaji upya wa vichwa vitatu vya treni na
kuendelea na uundaji wa vichwa vitano, kukamilisha malipo ya vichwa 13,
mabehewa ya mizigo 274, mabehewa 34 ya breki na toroli 30 za umeme,”
alisema Wassira.
Alisema katika sekta ya maji, mafanikio ni ujenzi
wa vituo vya kuchotea maji 9,644 na kuhudumia wananchi milioni 2.3
waishio vijijini ikilinganishwa na watu 300,000 hadi 500,000 awali.
Katika ukusanyaji wa mapato, Wassira alisema
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeanza kutumia kifaa bora cha
uthaminishaji wa bidhaa na kutoa makadirio bora zaidi ya viwango vya
kodi. Mpango huo wa BRN umegawanywa katika maeneo sita ambayo ni elimu,
kilimo, maji, nishati, utafutaji wa rasilimali fedha na uchukuzi.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment