JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
(PRESS RELEASE)
Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inalaani vikali tukio la ukatili
na udhalilishaji dhidi ya mtoto Nasra (4) mkazi wa mjini Morogoro ambaye
alifichwa chumbani ilhali amefungiwa ndani ya kasha na mama yake mkubwa
kwa muda wa miaka nne, baada ya mtoto huyo kufiwa na mama yake mzazi.
Kitendo
hicho ni ukiukwaji wa haki za mtoto. Wizara inasisitiza kwamba mzazi au
mlezi yeyote anayekubali jukumu la kulea mtoto anaowajibu wa kuhakikisha
kuwa anampatia mahitaji yote muhimu ya kumwezesha mtoto kukua hadi
kufikia utimilifu wake. Wizara inakemea vikali kitendo hicho na vingine
vingi vya aina hiyo ambavyo vinaendelea kufanyika katika familia zetu na
jamii kwa ujumla.
Wizara
inaziomba mamlaka zinazohusika na udhibiti wa vitendo vya ukatili dhidi
ya watoto kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wanafikishwa mbele ya vyombo
vya sheria ili haki iweze kutendeka na kuwa fundisho kwa wanaoendeleza
ukatili dhidi ya watoto. Jamii inahimizwa kubadilika na kuhakikisha kuwa
familia ambayo ndio kitovu cha jamii panakuwa ni mahala salama; na
kuwahakikishia watoto haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi,
kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa.
Wizara
inapongeza Uongozi wa Manispaa ya Morogoro hasa Afisa Ustawi wa Jamii,
Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto na Afisa Mtendaji wa
Kata ya Kiwanja cha Ndege kwa kufuatilia suala hili kwa karibu. Vile
vile, Wizara inapongeza majirani na vyombo vya habari kwa uzalendo wao
mkubwa wa kufichua ukatili aliofanyiwa mtoto huyu maana taarifa zao
zimesaidia kunusuru uhai na maisha ya mtoto Nasra.
Wizara
inamwelekeza Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Morogoro awasiliane na
Afisa Ustawi wa Jamii husika kuona uwezekano wa kumkabidhi mtoto Nasra
kwenye taasisi zinazohusika na matunzo ya watoto ili awe kwenye mikono
salama, wakati taratibu za kisheria zikifanyika dhidi ya wanaohusika na
ukatili huo.
Anna T. Maembe
KATIBU MKUU
23 Mei, 2014
Post a Comment