
USAJILI WA WACHEZAJI KUANZA JUNI 15
Usajili
wa wachezaji kwa hatua ya kwanza msimu huu (2014/2015) unaanza Juni 15
hadi Agosti 3 mwaka huu wakati kipindi cha kutangaza wachezaji
walioachwa au kusitishiwa mikataba ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu.
Kipindi
cha kwanza cha uhamisho wa wachezaji ni kuanzia Juni 15 mwaka huu hadi
Julai 30 mwaka huu. Kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya
Agosti 4 na 11 mwaka huu. Kuthibitisha usajili hatua ya awali ni Agosti
12 hadi 14 mwaka huu.
Usajili
hatua ya pili utakuwa kati ya Agosti 14 na 29 mwaka huu. Kupitia na
kutangaza majina ya pingamizi hatua ya pili ya usajili ni kuanzia Agosti
30 hadi Septemba 4 mwaka huu. Uthibitisho wa usajili hatua ya pili ni
Septemba 5 na 6 mwaka huu.
Kwa
upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka
huu, na ratiba inatarajiwa kutoka mwezi mmoja kabla (Julai 24 mwaka
huu).
MECHI YA TAIFA STARS YAINGIZA MIL 63/-
Mechi ya
mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika mwakani nchini
Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe iliyochezwa Jumapili
katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 63,345,000.
Mapato
hayo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi
wa bao 1-0 yametokana na washabiki 11,079 waliokata tiketi kushuhudia
pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000.
Mgawo wa
mapato hayo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo
ni sh. 9,662,796.61, gharama za kuchapa tiketi sh. 6,000,000, asilimia
15 ya uwanja ni sh. 7,152,330.51, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh.
9,536,440.68 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa pamoja wamepata sh.
30,993,432.20.
WASHABIKI KWENDA HARARE KUSHANGILIA STARS
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaandaa utaratibu utakaowawezesha
washabiki kwenda jijini Harare, Zimbabwe kushuhudia mechi ya Taifa
Stars.
Mechi
hiyo ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa ajili ya fainali zitakazochezwa
Morocco mwakani itafanyika Jumapili (Juni 1 mwaka huu) jijini Harare.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilishinda mechi ya
kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.
Usafiri
huo utakuwa wa basi ambapo washabiki wanatarajiwa kuondoka siku ya
Ijumaa na kuwasili Jumapili mchana jijini Harare ambapo watashuhudia
mechi na kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo.
Washabiki wanatakiwa kuwa na hati za kusafiria (pasipoti), nauli ya kwenda na kurudi itakuwa sh. 300,000.
TIMU YA U15 YAWASILI GABORONE
Timu ya
Tanzania ya umri chini ya miaka 15 imewasili salama jijini Gaborone,
Botswana kwa ajili ya michezo ya Afrika ambapo itacheza mechi yake ya
kwanza Mei 22 mwaka huu dhidi ya Mali.
Kikosi
hicho cha wachezaji 16 chini ya Kocha Abel Mtweve kimetua jijini
Gaborone jana (Mei 19 mwaka huu) jioni kwa ndege ya South African
Airways. Michezo hiyo itamalizika Mei 30 mwaka huu.
Wachezaji
waliopo kwenye kikosi cha Tanzania ni Adam Shayo, Amani Ally, Amos
Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid, David Uromi, Goodlove
Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin, Nasson Chanuka,
Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka.
Nchi nyingine zinazoshiriki michezo hiyo kwa upande wa mpira wa miguu ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Mali na Swaziland.
Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambazo nazo zilikuwa zishiriki kwenye michezo hiyo katika dakika za mwisho.
NGORONGORO HEROES YAENDA NIGERIA
Kikosi
cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heroes) chenye watu 25 kinaondoka kesho alfajiri kwenda Nigeria kwa
ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).
Mechi
hiyo itachezwa Jumamosi (Mei 24 mwaka huu) katika Jiji la Kaduna kwenye
Jimbo la Kaduna ambalo lipo katikati ya Nigeria. Msafara wa timu hiyo
unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi unaondoka kwa ndege ya Ethiopian
Airlines.
Ngorongoro
Heroes inayonolewa na Kocha John Simkoko ilipoteza mechi ya kwanza
iliyofanyika nyumbani jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-0.
Mwamuzi
Alhadi Allaou Mahamat wa Tchad ndiye atakayechezesha mechi hiyo.
Atasaidiwa na Issa Yaya, Alfred Madjihoudel na Idriss Biani wote kutoka
Tchad. Kamishna ni Aboubakar Alim Konate wa Cameroon.
BONIFACE WAMBURA, OFISA HABARI NA MAWASILIANO, SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Post a Comment