Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kimetangaza kwamba hakina mpango wa kushawishi viongozi wa
Serikali au viongozi wa kitaifa,
wawalazimishe au wawabembeleze wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni.
Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitoa
kauli hiyo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kikao cha
dharura cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika juzi.
Nnauye alisema
badala yake, CCM kupitia Sekretarieti yake itaendelea kushughulika na wajumbe
hao mitaani, kutokana na upotoshaji ambao wamekuwa wakiueneza.
“Watu wenyewe
hata kwenye kiganja cha mkono hawajai,” alisema Nape akielezea Mkakati wa CCM
kukabiliana na upotoshaji wa Ukawa.
Alisema kama ni
theluthi mbili, itapatikana hata bila wao kurudi bungeni na kuwataka waendelee
kukaa hukohuko.
Nape alisema
Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti ya CCM kwa kazi inayoifanya ya kujibu uongo
unaoenezwa na baadhi ya wajumbe hao wa Ukawa, kuhusu mchakato wa kuandika
Katiba mpya.
“Tayari
tumefanya mkutano Unguja na Pemba iliyokuwa na mafanikio kwa hiyo hatuna sababu
ya kuwa na hofu,” alisema.
Mbali na uamuzi
huo, Nape pia alisema Kamati Kuu imesikitishwa na baadhi ya watu au vikundi
ambavyo kwa makusudi,
wamekuwa wakieneza uongo au kupotosha kuhusu mchakato wa Katiba.
Alisema kwa
mujibu wa tathimini iliyofanywa na Kamati Kuu, pamoja na upungufu uliojitokeza,
imeridhishwa na jinsi mchakato huo unavyoendelea.
“Kamati Kuu
imewapongeza Wazalendo ambao waliendelea kubaki ndani ya Bunge kwa ajili ya
kuendelea na mchakato wa kuandika Katiba,” alisema.
Alisema Kamati
Kuu pia imesikitishwa na baadhi ya wajumbe ambao kwa maneno na vitendo vyao
wameonesha hawana nia ya kutunga Katiba, hasa wajumbe wa Ukawa waliokimbia
chombo cha kisheria cha kutengeneza Katiba mpya, badala yake wamekimbilia kwa
wananchi.
Nape alisema
Kamati Kuu inawakumbusha kwamba muda wa kupeleka Rasimu ya Katiba kwa wananchi
bado haujafika na sasa si wakati wake.
Post a Comment