Yanga wauvuruga Uchaguzi Mkuu Simba


KLABU ya Yanga imetajwa kuingilia kati na kuuvuruga Uchaguzi Mkuu wa Simba unaotarajiwa kufanyika
Juni 29, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Police Officer’s Mess, Masaki jijini Dar es Salaam.
Simba hivi sasa ipo kwenye matayarisho ya uchaguzi huo ambapo tayari imemaliza usaili wa wagombea wake wa nafasi mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Championi Jumamosi, wapo baadhi ya watu wa Yanga wanatajwa kumsaidia Mgombea wa Urais wa Simba, Michael Wambura aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Tumegundua kitu kimoja ambacho wenyewe wanafanya siri, lakini kama sisi viongozi wa Simba, tumeshajua mchezo mzima unavyoendelea.
“Upo uwezekano mkubwa wa Wambura kurejeshwa kugombea Simba baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba kumuondoa na kukimbilia TFF kwenda kukata rufaa ili arejeshwe kugombea.
“Sisi tumelishtukia hilo, tunajua TFF wapo marafiki wake wa karibu waliowahi kuiongoza na wanachama wa Yanga, tunatoa angalizo kwa viongozi hao kuhakikisha wanafuata kanuni zote za uchaguzi.
“Uzuri wake kanuni na katiba za uchaguzi zipo wazi kabisa kwa wagombea wa Simba, kati ya hizo mojawapo ikivunjwa basi kanuni za uchaguzi zinakiukwa,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza:
“Katiba moja iliyopo Simba inasema kuwa, mgombea yeyote atakayepeleka masuala ya soka mahakamani basi atajitoa uanachama, kitu ambacho amekifanya Wambura, tunaamini Rais wa TFF, Jamal Malinzi ni mwelewa na anayefuata katiba, hivyo tunamuomba kuwa makini nalo.”
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope, alisema kiukweli katiba ya Simba ipo wazi katika hilo, ni vema TFF wakawa makini nalo katika kutoa maamuzi sahihi kwenye rufaa hiyo ya Wambura.
“Ujue katiba ya Simba ipo wazi kwa wagombea, hivyo nitashangaa kuona Wambura anarejeshwa kugombea urais, kitu ambacho hakiwezekani kwa mujibu wa katiba ya Simba, hilo ni angalizo kwangu tu kwa TFF,” alisema Hanspope.

Post a Comment

Previous Post Next Post