Yanga yasajili kiungo usiku

KLABU ya Yanga, jana usiku ilitarajiwa kumsainisha kiungo wa Taifa Stars, Said Juma.
Inadaiwa kuwa, aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ndiye aliyetoa mapendekezo ya kusajiliwa kwa kiungo huyo.
Jana usiku, Yanga ilitarajiwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili lakini kama ingeshindikana jana, basi anaweza akasajiliwa ndani ya siku mbili kuanzia leo.
Juma aliingia kwenye kikosi cha Taifa Stars hivi karibuni baada ya kupita kwenye kundi la wachezaji wa kuboresha kikosi hicho, lakini aliondolewa na kocha mkuu wa timu hiyo, Martius Nooj na jana hakuwepo uwanjani.
Taarifa ambazo zilipatikana jana zilisema kuwa mchezaji huyo ambaye anatokea Zanzibar alitarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo ya Jangwani.
“Anacheza namba sita uongozi ulimuona kwenye mchezo wa kirafiki kati ya Stars na Burundi na kuvutiwa naye.
“Wamekuwa wakisema kuwa ndiye mbadala sahihi wa Frank Domayo ambaye ametimkia kwenye kikosi cha Azam FC.
“Uhakika ni kwamba jana usiku baada ya mechi kati ya Stars na Zimbabwe ndiyo walikuwa na mpango wa kumpa mkataba.
“Walimtumia mchezaji wao mmoja ambaye yupo Taifa Stars naye anatokea Zanzibar ndiye aliyefanya mipango yote,” kilisema chanzo hicho.

Post a Comment

Previous Post Next Post