
Imesema ilitoa agizo la maboresho zaidi ya miaka mitatu iliyopita na
sasa inaandaa mikakati kuleta mapinduzi katika sekta ya nyama hasa machinjio
ili kuboresha huduma, afya ya jamii na kuhakikisha sheria na miongozo
inazingatiwa.
Hayo yalisemwa jana, jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa TFDA,
Raymond Wigenge alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua
semina ya siku mbili kwa wajasiriamali wadogo wa vyakula kutoka mikoa
mbalimbali nchini.
Wigenge aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika ufunguzi wa semina hiyo,
alisema TFDA inatambua changamoto zinazoikabili sekta ya nyama, ikiwemo uchafu
na miundombinu duni katika machinjio na imejiandaa kuweka mikakati mipya
kupambana na hali hiyo.
“Serikali haijakaa kimya, sasa tunaandaa mikakati mipya kuangalia kwa
undani sekta ya nyama hasa machinjio, miaka mitatu iliyopita tuliagiza pia
mabucha yote wawe na misumeno ya umeme, lakini kuna sehemu nyingine hakuna
umeme wanapaswa kutafuta ya plastiki, mambo haya ni changamoto bado,” alisema
Wigenge.
Alisema nchini kuna zaidi ya machinjio 900 lakini ni takribani 20 pekee
yamesajiliwa. Pia alisema wanashirikiana na halmashauri kuboresha usafi katika
masoko na alisisitiza kuwa bidhaa zozote za chakula hazipaswi kuwekwa chini
wakati zikiuzwa ni hatari kwa afya.
Kuhusu mafunzo hayo, alisema TFDA kwa kushirikiana na taasisi ya sekta
binafsi ya TPSF imeandaa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo 80 kutoka mikoa
mbalimbali nchini kwa lengo la kujifunza kanuni, sheria na miongozo ya uandaaji
na usindikaji wa vyakula kuboresha kipato na afya za walaji.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya TPSF
akiwakilisha wanawake, Anna Matinde alisema fursa hiyo imetokana na utekelezaji
wa agizo la Rais Jakaya Kikwete kwamba wajasiriamali wadogo wapatiwe vyeti vya
usindikaji vya TFDA na Shirika la Viwango (TBS) hivyo kabla ya kupewa vyeti
lazima wafahamu na kufuata sheria.
Post a Comment