
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad
Dar es Salaam. Katibu
Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad amesema juhudi zinazofanywa
kuusambaratisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hazitafanikiwa.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa CUF
uliofanyika katika Kata ya Makurumla, Wilaya ya Kinondoni, Dar es
Salaam, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
alisema kumekuwa na juhudi za hapa na pale za kutaka kuusambaratisha
umoja huo na kusisitiza kuwa zitakwama.
“Umoja huu umeundwa kwa lengo la kutetea
masilahi ya wananchi kupata Katiba wanayoitaka na wala siyo kwa masilahi
binafsi… Nimefurahishwa na vyama vya upinzani kuunda umoja huu, kwani
vinginevyo CCM ingewaburuza na kufanya uamuzi wanaoutaka kinyume na
matakwa ya wananchi walio wengi,” alisema.
Alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
inalitaka Bunge Maalumu la Katiba kujadili Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Tume hiyo na siyo kujadili rasimu nyingine yenye
matakwa ya kundi maalumu.
Hamad alirejea kauli kwamba Ukawa
wanaweza kurudi bungeni endapo tu Rais Jakaya Kikwete atawahakikishia
kuwa rasimu itakayojadiliwa ni ile iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba na iwapo itakwenda kinyume, wanaweza kutoka tena kwenye Bunge
hilo.
Akizungumzia kuhusu Muundo wa Muungano,
Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema hakuna mbadala mwingine wa kumaliza kero
za Muungano isipokuwa serikali tatu zitakazotoa mamlaka kwa serikali za
nchi washirika.
Alisema hata Katiba ikitoa mamlaka kwa
Zanzibar kuhusu kuweza kujiunga na mashirika ya Kimataifa yakiwamo; Afya
(Who), Chakula (Fao) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mamlaka
hayo hayatokuwa na nguvu kwani mashirika hayo yanahitaji kufanya
ushirikiano na nchi zenye mamlaka kamili (sovereign states). Pia mamlaka
hayo ya kikatiba bila kuwa kamili yatakuwa ni kiini macho.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara),
Julius Mtatiro, alisema vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa,
vitaendelea kupigania Katiba inayotokana na maoni ya wananchi.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment