MAGUFULI AAMURU KITUO CHA MABASI DODOMA KUHAMISHIWA NJE YA MJI

Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli ameagiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhamishia kituo kikuu cha mabasi cha Dodoma  nje ya mji, ili kudhibiti msongamano wa magari unaochangiwa na kukua kwa haraka kwa mji.
Alitoa agizo hilo juzi katika  uzinduzi wa mradi wa taa za kuongozea magari na watumiaji wa barabara katika manispaa ya Dodoma. 
Taa zote zimegharimu Sh milioni 384 na aliyejenga ni mkandarasi wa ndani.
Alisema kuwepo kwa kituo hicho cha mabasi katikati ya mji mbali na kusababisha uwepo wa msongamano wa magari, lakini pia kinachangia kuchelewesha maendeleo ya mji wa Dodoma.
Pia akizungumzia ujenzi na ukarabati wa barabara za manispaa ya Dodoma alisema Serikali imetumia zaidi ya Sh bilioni 490 kugharamia miradi mbalimbali ya barabara nchini ikiwemo ile inayounganisha mikoa na ni vyema mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinasimamia ipasavyo matumizi ya barabara hizo ili ziweze kudumu.
Alisema  Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 9.5 kupitia fedha za mfuko wa barabara kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika halmashauri za Dodoma, Kondoa, Chemba, Bahi, Kongwa Mpwapwa na Chamwino ili kuchochea ukuaji wa uchumi katika Mkoa wa Dodoma
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi alisema mpango uliopo ni kuhamisha stendi za mabasi ya mikoani ziende nje ya mji kwani haiwezekani Dodoma kuwa Jiji kwa stendi iliyopo.
Alisema Dodoma inatarajiwa kuwa na stendi nne ambapo moja itakuwa eneo la Ihumwa, nyingine barabara ya Singida, pia Barabara ya Arusha na barabara ya Iringa.
Dk Nchimbi alisema taa za kuongozea magari zina thamani kubwa na kutaka kuwe na mipango ya kujenga barabara nzuri ili iwe rahisi kujenga taa za kuongozea magari.

Post a Comment

Previous Post Next Post