Rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa hivi karibuni lakini hata hivyo padri huyo pamoja na wakili wake hawakufika mahakamani. Upande wa Jamhuri una hoja saba katika rufani hiyo.
Kabla ya kuachiwa huru baada ya kukata rufaa, Padri Kimaro alihukumiwa kifungo cha miaka 35 jela na kulipa faini ya Sh milioni mbili kwa mtoto baada ya kupatikana na hatia.
Kutokana na kushindwa kwa jopo hilo kusikiliza rufani hiyo wiki iliyopita, kwa kutotokea mahakamani hapo padri huyo wala wakili wake, jopo limeagiza upande wa Jamhuri kutoa taarifa ya mwito kuwa anahitajika mahakamani hapo kupitia vyombo vya habari.
Hatua ya kuamriwa kutumika vyombo vya habari kunatokana na wakili wa Serikali, Salum Malick kudai kuwa amepata taarifa kutoka kwa msajili wa mahakama hiyo kuwa, hati ya mwito wa kumtaka afike mahakamani hapo ilipelekwa kwa Kanisa Katoliki.
Alidai kwa mujibu wa taarifa hiyo ya msajili wa mahakama, hati hiyo ilipelekwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam lakini waliambiwa na jimbo hilo kuwa Padri Kimaro si mwajiriwa wao na wala hawajui alipo.
Jopo la majaji hao watatu ambao ni Engela Kileo, Steven Bwana na Sauda Mjasiri, limeamrisha mwito huo umtake afike kusikiliza rufaa yake kwa tarehe nyingine itakayopangwa na mahakama hiyo.
Akitoa amri hiyo, Jaji Kileo alisema endapo padri huyo hatafika mahakamani baada ya matangazo hayo, rufaa hiyo itaendelea kusikilizwa upande mmoja.
Katika kesi ya msingi, Padri Kimaro alikuwa anakabiliwa na mashitaka matatu; kumlawiti mtoto wa miaka 17, shambulio la aibu na kumdhalilisha mtoto huyo.
Ilidaiwa kuwa usiku wa Mei 18 mwaka 2005 katika eneo la Changanyikeni, Dampo, Padri Kimaro alikamatwa na askari aliyekuwa doria, akitenda makosa hayo.
Katika hukumu iliyotolewa Agosti 9, 2006 na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Pelagia Khaday, Padri Kimaro alipatikana na hatia katika makosa yote na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 35 jela na kulipa fidia ya Sh milioni mbili kwa mtoto aliyeathirika na kitendo hicho.
Alikata rufaa Mahakama Kuu iliyosikilizwa na Jaji Robert Makaramba, ambapo aliachiwa huru baada ya Jaji huyo kudai kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani.
Hata hivyo upande wa Jamhuri umekata rufaa kupinga uamuzi huo wa kuachiwa huru kwa padri huyo wakiwa na hoja saba ya msingi, ikiwa ni kwamba Jaji aliyesikiliza rufaa hiyo alikosea kisheria na kiusahihi kueleza kuwa hapakuwa na ushahidi wa moja kwa moja kuhusu walichokuwa wakifanya mjibu rufani (padre) na mtoto huyo eneo la Dampo.
Post a Comment