SMZ YAANZA KUSOMESHA WATAALAMU MAFUTA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema jumla ya wanafunzi 20 wanaendelea na masomo katika fani ya mafuta na gesi pamoja na utafiti.
Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdallah Shaaban alisema hayo wakati alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu juhudi zinazofanywa na Wizara hiyo katika kusomesha vijana katika sekta ya nishati na gesi.
Alisema vijana hao ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali ikiwemo vya nje ya nchi na ndani wanadhaminiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo ya Raskgas.
Aidha, wanafunzi hao wanasoma katika viwango vya elimu kuanzia shahada ya kwanza na ya pili katika masuala ya mafuta gesi na utafiti.
“Tumeanza kusomesha vijana wetu ambao watakuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia masuala ya mafuta na gesi pamoja na utafiti na uendeshaji wa masuala hayo,” alisema.
Alizitaja baadhi ya nchi ambazo zimesaidia kusomesha vijana hao ikiwemo Norway pamoja na nchi ya Ras-Alkheimar.
Shaaban alifafanua na kusema Serikali imechukua hatua hizo kwa lengo la kuhakikisha inakuwa na wataalamu wa kutosheleza katika masuala ya gesi na mafuta.
Hatua hizo zinachukuliwa kufuatia kuwepo kwa taarifa za awali za mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Unguja na Pemba.
Zanzibar kwa sasa inataka suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano kwa lengo la kuona wananchi wanafaidika na nishati hiyo moja kwa moja.
Tayari Baraza la Wawakilishi tangu mwaka 2010 limepitisha azimio la kutaka mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wawakilishi cha bajeti kilichomalizika hivi karibuni, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi aliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka katika kambi ya upinzani kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ambalo ndiyo litakalolipatia ufumbuzi suala la mafuta na gesi.
Alisema kitendo cha kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kamwe halitazipatia ufumbuzi kero za Muungano ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu na wananchi wa Zanzibar.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamesusia vikao vya Bunge hilo kwa kuungana na kundi linalojiita Ukawa likiwahusisha wabunge wa kambi ya upinzani kutoka vyama vya siasa.

Post a Comment

Previous Post Next Post