Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma inayoendesha vikao vyake mjini Singida, ilitoa hukumu hiyo jana.
Waliohukumiwa ni Shani Mtua na Mohammed Salimu ambao wakati walipotenda kosa hilo, mwaka 2008, walikuwa Kidato cha Tatu na walikuwa na umri wa miaka 18 kila mmoja.
Ilielezwa mahakamani kwamba kulikuwa na washitakiwa wengine wawili katika kesi hiyo; Emmanuel Daud na Michael Msengi, walikufa wakiwa mahabusu wakisubiri kesi yao kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Hukumu ilitolewa na Jaji Rehema Mkuye baada ya washitakiwa hao kukiri shitaka la kuua bila kukusudia walilofanya katika Kijiji cha Mpambala, Tarafa ya Kirumi Wilaya ya Mkalama.
Awali, Mwanasheria wa Serikali, Zakaria Elisaria aliyekuwa anasaidiwa na Karen Mrango, alidai mahakamani kwamba washitakiwa walihusika na mauaji ya Rajabu Idude (49), aliyekuwa Mwalimu wa Nidhamu shuleni hapo. Ilidaiwa walifanya mauaji hayo Agosti 2008.
Mwanasheria huyo wa Serikali alidai chanzo cha mauaji hayo ni mshitakiwa wa kwanza , Shani, kupewa barua ya kusimamishwa masomo kwa wiki mbili kutokana na utovu wa nidhamu na kisha akashawishi wenzake watatu kumpiga mwalimu huyo.
Zakaria alisema wanafunzi hao walimvizia mwalimu huyo katika kichaka cha karibu na shule yao wakampiga ngumi na mateke, kisha wakamjeruhi mwilini kwa kisu alichokuwa nacho mshitakiwa wa kwanza.
Inadaiwa kutokana na kipigo hicho, Mwalimu Idude alipiga kelele na mwanawe aliyetajwa kwa jina la Maye Rajabu, alifika haraka kwenye eneo la tukio, lakini akakuta ameshakufa.
Wanafunzi hao (washitakiwa) hawakukutwa katika eneo hilo lakini msako ulifanyika usiku huo na wanafunzi wanne walikamatwa. Baada ya kuhojiwa kuanzia ngazi ya mlinzi wa amani kwenye kijiji hicho hadi jana mahakamani, walikiri kosa.
Kwa upande wake, Wakili wa washitakiwa, kutoka Kampuni ya Uwakili ya Kim & Company, Raymond Kimu, alimwomba Jaji Mkuye kutoa adhabu nafuu dhidi ya wateja wake, kutokana na kuonesha ushirikiano wa kutosha tangu siku waliyokamatwa.
Aidha, alidai washitakiwa walifanya kosa hilo kutokana na kusukumwa na umri mdogo wa utoto. Alidai ni wakosaji wa mara ya kwanza, wanajutia kosa hilo na kwamba wamekaa jela kwa muda mrefu wa miaka sita, hivyo wamejifunza kutokana na mauaji hayo.
Akitoa hukumu, Jaji Mkuye alisema hakuna ubishi kwa yote aliyosema wakili wa utetezi. Hata hivyo alisema, anadhani sababu hizo siyo kibali kwa washitakiwa hao kupanga na kutekeleza mauaji dhidi ya mwalimu wao aliyekuwa anasimamia nidhamu.
“Nadhani kosa walilofanya haliwezi kukubalika kwa jamii hata kidogo…fujo zimekuwa zikitokea kwenye mashule na vyuo, hata kusababisha vurugu kiasi cha kuathiri utendaji…, kufuatia kosa hili, kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka sita jela,” alisema Jaji Mkuye.
Post a Comment