Hatua hiyo ya walimu
wenye Shahada kuanza kufundisha shule za msingi tofauti na
ilivyozoeleka, chini ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, ni
sehemu ya mageuzi makubwa, yanayotarajiwa kufanyika katika sekta ya
elimu nchini.
Rais Kikwete alishawahi kutamka mpango huo wa kutumia
wasomi wa vyuo vikuu katika shule za msingi, kutokana na idadi kubwa ya
wahitimu wa ualimu, kutarajiwa kuwa kwenye soko la ajira.
Alisisitiza
kuwa baada ya mwaka, wahitimu wa vyuo vikuu watafundisha katika shule
hizo na kwamba kufanya hivyo si kuwashushia hadhi.
Akihutubia
wananchi mjini Mbinga, kabla ya kufungua kituo cha mabasi na barabara ya
Peramiho- Mbinga yenye urefu wa kilometa 78, Kikwete alisema barani
Ulaya, hata walimu wa shule za chekechekea wana Shahada na kwamba hicho
ni kipimo cha maendeleo.
Kwa utaratibu uliozoeleka chini ya Sera ya
Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, walimu wa shule za msingi ni wenye
cheti. Hata hivyo, kulingana na taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, wapo wanaochukua Shahada, wanaosomea kufundisha elimu ya
msingi.
“Wakati umebadilika…leo utamchukua Standard Seven ( Darasa
za Saba) kwenda chuo cha ualimu? Leo Division Four (waliopata Daraja la
Nne) wanakataliwa vyuo vya ualimu,” alisema.
Alisema, hali ya sasa ni tofauti na miaka ya nyuma kwa kuwa sasa, hata makatibu tarafa wana Shahada.
Kwa
mujibu wa tamko la Serikali, kuanzia sasa wanaosomea ualimu ngazi ya
Cheti na Stashahada, sharti wawe na ufaulu wa daraja la tatu.
Aidha,
Serikali imeamua kuanzia sasa wanaojiunga na mafunzo ya Stashahada ya
Ualimu katika masomo ya Sayansi wakiwa na ufaulu wa Daraja la Kwanza,
watasomeshwa bure. Pia wenye ufaulu wa Daraja la Pili na la Tatu,
watapewa mkopo.
Akizungumzia shule za sekondari za kata, Rais
Kikwete alipongeza maendeleo ya taaluma, kutokana na baadhi shule hizo
kuwa miongoni mwa wanaofanya vizuri katika mitihani ya taifa.
Kwa
mujibu wa Rais Kikwete, wakati shule hizo zinaanzishwa, hali ilikuwa
ngumu tofauti na sasa ambako yapo mabadliko. Alitoa takwimu kwamba kati
ya wahitimu 71,000 waliochaguliwa kuendelea na Kidato cha Tano, 20,000
wameachwa.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanafunzi wengi wa
shule za msingi na sekondari, Rais Kikwete aliagiza ifikapo mwaka 2016,
kila mwanafunzi awe na kitabu chake.
Alisema, serikali imeanza
kutenga fedha kwa ajili hiyo, zikiwemo Sh bilioni 21 zilizotengwa
katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2014/2015.
Rais aliagiza fedha kwa ajili ya vitabu zitengwe na azione kwa kuwa anataka taifa lipate wataalamu wengi.
Katika
mkutano huo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista
Mhagama alisema katika shule za msingi hivi sasa, wanafunzi watatu
wanatumia kitabu kimoja.
Kwa mujibu wa Mhagama, kupitia Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Wilaya ya Mbinga ilikuwa ya kwanza kitaifa
kwa maendeleo ya elimu.
Aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri,
wanayofanya wilayani humo. Alibainisha kuwa walimu 112 waliopangiwa
kufundisha katika shule za msingi walikwenda, na wengine 138
waliotakiwa kwenda kufundisha shule za sekondari, wanaendelea na kazi.
Post a Comment