Viongozi hao ni Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar, Salum Mwalimu.Mkutano huo uliohutubiwa na viongozi hao, pia
ulihudhuriwa na viongozi wa mkoa wa Mwanza wa vyama vya NCCR-Mageuzi na
Chama cha Wananchi (CUF) ambavyo pamoja na Chadema wanaunda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo, walikuwa wamevaa sare za vyama vyao
vinavyounda Ukawa na muda wote walionekana kuwashangilia viongozi wao
walipopanda jukwaani.
Mnyika alisema baada ya serikali kuzuia maandamano yao nchi nzima
kupinga Bunge Maalum la Katiba, sasa wametangaza mbinu mpya ya
kuandamana kwa njia ya kutuma ujumbe mfupI wa simu (sms) na kwamba
watakapoandamana na kuzuiliwa waandamanaji watakuwa wanatuma sms kwa
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Rais na Mwenyekiti wa Kamati ya
Uandishi ya Bunge hilo, Andrew Chenge, ili kufikisha ujumbe wao.
Kwa upande wake, Mwalimu alisema vyama vitatu vinavyounda Ukawa ni
lazima wawe wamoja kuhakikisha upatikanaji wa katiba mpya aliyoiita ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukwame na kuwataka wanachama kujitokeza pale
yanapokuwapo maandamano kwa ajili ya kufikisha ujumbe.
Awali, Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Ilemela, Wanzagi Warioba, alisema
ni wakati sasa wa vyama hivyo vinavyounda Ukawa kuunganisha nguvu ya
pamoja kuwaondoa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na
kuwatumia polisi kuwadhibiti wapinzani.
“Ni muda wa kuungana ili kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa na
vitongoji, kuwang'oa kabisa hawa CCM ambao wanaamini nchi hii ni mali
yao pekee yao,” alisema Warioba.
Naye Kamishana wa NCCR-Mageuzi mkoa wa Mwanza, Amran Ramadhani, alisema
wakati wa mapambano na wadhalimu wa nchi hii kuwaondoa viongozi wa CCM
umewadia, hivyo wananchi wote wanatakiwa kuwa kitu kimoja na Ukawa
kuwaondoa.
“Pale Chadema watakaposimamisha mgombea, lazima vyama vingine tumpe
nguvu mgombea huyo, na CUF nao vile vile na NCCR-Mageuzi hivyo hivyo,
hakuna kuwaachia nafasi hawa CCM kuchukua uongozi katika ngazi yoyote,”
alisema Ramadhani.
Katibu Mwenezi wa CUF mkoa wa Mwanza, Hamza Shido, alisema muda wa
mapambano dhidi ya polisi na CCM umewadia kutokana na watu hao
kuwasumbua sana wananchi wasio na hatia yoyote.
" Tunaandamana bila silaha, lakini tunavurumishiwa mabomu na kukamatwa
ovyo...sasa ni wakati wa kupigania haki zetu kwa namna yoyote ile,”
alisema Shido.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje, alisema muda wa kuwaondoa viongozi
wa CCM katika uongozi ni sasa mara baada ya uchaguzi wa serikali za
mitaa baadaye mwaka huu.
“Tumenyanyaswa sana na polisi wa CCM, sasa tumefikia mwisho kwani
wanaelewa ni jinsi gani ambavyo wataondolewa madarakani na wananchi...
tunatengenez barabara, lakini wao wanasema ni sera ya CCM, sasa mbona
wabunge wao walikuwapo hawakuufanya hivyo?” alihoji Wenje.
Hata hivyo baada ya mkutano huo kumalizika askari wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) Mkoa wa Mwanza, walitumia mabomu kuwatawanya wafuasi wa
Chadema waliokuwa wakiwasindikiza viongozi wao wakiwa katika makundi.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment