Maafisa wa Polisi nchini Marekani wamesema rais wa Zambia, Michael Sata
alitibiwa na daktari katika chumba cha hoteli alimofikia lakini
hajalazwa hospitalini kama ilivyodaiwa.
Naibu Chifu wa Polisi wa New York, Kim Royster ameliambia shirika la
habari la Associated Press kuwa rais Sata alitibiwa na madaktari wa
Serikali ya Marekani siku ya Alhamisi kisha akapelekwa hospitalini
lakini hakulazwa.
Rais Sata aliwasili nchini Marekani akitokea Lusaka, Zambia kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa
Viongozi wa Dunia kwenye Kikao cha 69 cha Baraza Kuu
la Umoja wa Mataifa (UNGA - United Nations General Assembly) lakini
hakuweza kuhutubia Baraza la viongozi hao wapatao 193 kutoka pande
mbalimbali duniani siku ya Jumatano.
Sata mwenye umri wa miaka 77 ni rais wa tano wa Zambia aliyeingia
madarakani mwaka 2011 baada ya kuwania kiti hicho kwa mara tatu.
Mwezi Juni mwaka huu alienda nchini Israel kwa ajili ya matibabu na
ameshatibiwa nchini Uingereza na Afrika Kusini mara kwa mara ikielezwa
kuwa anasumbuliwa na 'kutapika' kila anachokula.
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa
baadhi ya maafisa wa Serikali wanaulaumu upinzani kwa 'kumloga' rais
Michael Sata.
Post a Comment