Katibu
wa Kamati ya uchambuzi wa rasimu hiyo, Esther William (katikati)
akisoma tamko la Wanaharakati wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa
la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na TGNP
Mtandao kwa waandishi wa habari jana. Kulia ni Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Badi Darusi na Hamadi Masudi Mjumbe (kushoto).
Na Mwandishi wetu
WANAHARAKATI
wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa la wazi la semina za Jinsia na
Maendeleo (GDSS), linaloratibiwa na mtandao wa kijinsia (TGNP),
wameipinga rasimu ya Katibu kwa kutoweka mfumo mzuri wa wananchi kuweza
kumuwajibisha rais pindi anaposhindwa kutimiza majukumu yake.
Mtandao
huo, umetoa tamko hilo baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa Rasimu
inayopendekezwa na kutolewa na Bunge Maalum la Katiba mnamo Septemba 9,
mwaka huu mjini Dodoma. Tamko hilo wanalitoa kuhusianisha rasimu ya
Katiba inayopendekezwa na madai ya wanaharakati wa masuala ya kijinsia.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwakilishi wa GDSS,
Esther William alisema, rasimu ya katiba imeipa uwezo Bunge kumwajibisha
Rais pindi akishindwa kutekeleza majukumu yake na akienda kinyume na
sheria na taratibu za nchi. Lakini rasimu imewanyimwa wananchi haki yao
ya msingi ya kumuwajibisha kiongozi waliyemchagua kwa kura zao.
Alisema,
kabla ya kutoa tamko hilo waliainisha madai 12 ya kikatiba yanayowahusu
wanawake na makundi mengine ya walio pembezoni.Madai hayo ni pamoja na
Haki za wanawake zibainishwe kwenye katiba, sheria Kandamizi
zibatilishwe, haki ya kufikia, kutumikia, kunufaika na kumiliki
rasilimali ya nchi, utu wa mwanamke ulindwe, utekelezaji wa mikataba ya
kimataifa kuhusu haki za wanawake.
Pia,
haki sawa katika nafasi za uongozi, haki za wanawake wenye ulemavu,
haki ya uzazi salama, haki za watoto wa kike, haki ya kufaidi huduma za
msingi, wajibu wa wazazi katika matunzo ya watoto na katiba iunde chombo
maalum kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi.
“Mbali
ya kutaka rais awajibishwe, pia rasimu hii ibara ya 79 na 80 imeendelea
kumlimbikizia rais madaraka ya kuteua viongozi na watendaji mbalimbali
wa serikali, bila ya kufuata na kuzingatia ushauri atakaopewa na mtu au
mamlaka yoyote, hali hii bado inaendeleza mfumo mbaya wa mgawanyo wa
madaraka kikatiba na inaendeleza mfumo kanadamizi katika utoaji wa fursa
za kiuongozi,”alisema.
Kutokana
na malimbikizo hayo, William alisema kuwa rasimu ya katiba inatakiwa
iweke ukomo wa uteuzi kwa rais ili kutoa fursa kwa mamlaka nyingine
kufanya uteuzi wenye tija. Pia alitolea mfano wa nchi ya Kenya ambayo
imetoa fursa kwa wananchi kuhoji uteuzi unaofanywa katika ngazi
mbalimbali.
Mbali
na hayo, alipingana na katiba hiyo kwenye ibara ya 135 inayosema mbunge
awe anajua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiiingereza. Alidai kuwa
kipengele hicho kinadidimiza maendeleo ya taifa, kwani bunge linatakiwa
kupitia na kuchambua kwa kina mikataba mbalimbali ambayo kwa sehemu
kubwa ipo kwenye lugha ya kiingereza.
“Je
Kigezo hiki cha kujua kusoma na kuandika kwa mbuge kutaweza kumfanya
aweze kusimamia, kufanya uchambuzi wa kina na kuiwajibisha serikali
kikamilifu? Na je kwa kigezo na sifa hizi za mbunge itaondoa tatizo la
nchi kuingia mikataba mibovu? Tunadai rasimu hii ya katiba ibadilishe
sifa ya kiwango cha elimu ya mbunge kuwa kidato cha nne,” alihoji.
Hata
hivyo, anaeleza kwamba wanadai mawaziri wasiwe miongoni mwa wabunge ili
kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa mihimili yote mitatu iweze
kujitegemea, hali ya kuwa kuna ibara ya 111 kifungu cha (1) (d) imetaja
sifa ya kuwa waziri ni lazima awe ni mbunge, huku kikileta mgongano wa
madaraka kati ya mihimili miwili ya dola kati ya Bunge na serikali kwa
kumpa madaraka mbunge kuwa waziri au naibu waziri.
Akizidi
kupingana na baadhi ya vipengele hasa kwa upande wa Haki za wanawake,
William alieleza kwamba wanashangazwa kuona katika ibara ya 22(2) (b)
cha rasimu ikitoa fursa ya bila ukomo kwa wawekezaji kuweza kutumia
ardhi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na makazi.
“Lazima
tushangae kwani ibara 22 kiufungu cha (2) (d) imeainisha haki ya
wanawake kupata, kumiliki, kutumia, kuendeleza na kusimamia ardhi kama
ilivyo kwa mwanaume, kwanini kipengele hiki kisiweke ukomo kwa
wawekezaji kutumia ardhi ili kuweza kuepusha migongano na migogoro ya
kimaslahi na ya kikatiba kati ya wananchi na wawekezaji katika suala la
umiliki wa ardhi ili wanawake wapate nafasi ya kumiliki?, ” alihoji.
Licha
ya kutoa pongezi kwa kamati ya uandishi wa katiba na bunge maalum,
alisema bado wanashangazwa na vipengele mbalimbali, ambavyo vinashindwa
kutambua haki za wanawake, ikiwemo kutotambuliwa kwa suala la maji kama
haki ya msingi ya kikatiba ambapo asilimia 60 ya watu wa mjini ndio
wanapata maji safi na salama huku asilimia 42 ya wakazi wa vijijini ndio
wanaopata maji safi.
“Tunadai
haki ya kupata maji safi na salama iwe ni haki ya kikatiba ili kuweza
kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutembea umbali mrefu wa kutafuta maji,
pia tunaitaji katiba itamke wazi uwiano wa asilimia 50 kwa 50 katika
ngazi na nafasi mbalimbali za maamuzi, kama kisiasa, kiuchumi na
kijamii,”aliongeza.
Aidha,
akigusia uhuru wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), alisema wanapingana na
ibara ya 257 kifungu cha (3) kwa kutoa uhuru kuwa benki hiyo kutekeleze
majukumu yake bila kuingiliwa, kudhibitiwa au kupewa maelekezo na mtu au
mamlaka yoyote.
“Kifungu
hiki kinakinzana na dhana bora ya uwajibikaji na utawala bora kwa kutoa
mwanya wa ubadhirifu na matumizi mabatya ya fedha za umma kwa kigezo
cha watendaji wa benki kuu kutowajibishwa kutokana na makosa yao
kiutendaji pindi wanapokuwa madarakani, hivyo tunadai ibara hii
irekebishwe,”alisema.
Post a Comment