WANANCHI WAWASUBIRI WARIOBA, SITTA MTAANI

BAADA ya kutokea malumbano kati ya Mwenyekiti wa Tume Maalum ya Kukusanya Maoni ya wananchi juu ya mchakato wa Katiba mpya, Jaji Joseph Warioba na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la katiba, Samuel Sitta, wananchi waliohojiwa wamesema wanawasubiri kwa hamu wanasiasa hao mitaani ili kuwasikiliza maneno yao.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la katiba, Samuel Sitta.
Mara baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) Andrew Chenge kuwasilisha rasimu ya katiba inayopendekezwa, ambayo iliyaacha baadhi ya mambo yaliyokuwa katika rasimu iliyowasilisha na Tume ya Warioba, Waziri huyo mkuu wa zamani wa Tanzania, alisema anamsubiri Sitta mtaani waweze kujieleza mbele ya wananchi, ili hoja zao zipimwe.
“Ni kweli, kama alivyosema Warioba, waje huku mitaani watuambie hoja zao nani tumsikilize na kumfuata, maana sisi wengine tunaona kama wanatuchezea tu akili, rasimu rasimu, yaani wanatuchanganya kabisa,” alisema Tom Sisiri, mfanyabiashara wa nguo za mitumba aliyetakiwa kutoa maoni yake.
Mwenyekiti wa Tume Maalum ya Kukusanya Maoni ya wananchi juu ya mchakato wa Katiba mpya, Jaji Joseph Warioba.
Shoyoza Ibrahim, mwanamke mjasiriamali mwenye duka la vyombo Mwenge jijini Dar es Salaam, alisema viongozi wanatakiwa kutoa elimu ya kutosha ili kuwafanya watanzania waelewe kinachojadiliwa, kwani hata maneno yenyewe yanayotumika, ni msamiati mkubwa kwao.
“Utawasikia wanasema sijui rasimu, akidi, muswada, mchakato na mambo mengine kama hayo, watu kama mimi naweza kuwa naelewa wanamaanisha nini wakisema hivyo, lakini ninajua kuna idadi kubwa ya watu hawajui maana ya maneno haya, sasa hii misamiati ingefafanuliwa kwa lugha rahisi za watu kuelewa, halafu ndiyo watoe somo sasa la nini kinachobishaniwa,” alisema.
Bunge Maalum la Katiba ambalo lilikuwa likipitia rasimu ya katiba iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba, linategemewa kumalizika mwishoni mwa wiki ijayo mjini Dodoma, likiwa na rasimu mpya inayopendekezwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post