Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Hatua hiyo isiyotarajiwa, inafuatia Bunge Maalum la Katiba
kukamilisha rasimu hiyo Jumatano iliyopita, ikitarajiwa kupigiwa kura
mapema wiki ijayo.
Akizungumza kwenye adhimisho la miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Aidha, Jaji Warioba, alisema
Bunge hilo limeondoa mambo ya msingi yaliyopendekezwa na wananchi
yakiwa ni kiini cha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Adhimisho hilo lilitumika pia kumkumbuka muasisi wa LHRC, marehemu
Dk. Sengondo Mvungi, ambapo kitabu kinachoelezea maisha yake,
kinachoitwa ‘Sengondo Mvungi, breathing the Constitution’ ikimaanisha,
‘Sengondo Mvungi, pumzi ya Katiba’, kilizinduliwa.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, rasimu ya Katiba inayopendekezwa na BMK ni mfano wa ile iliyopo sasa ikiwa imewekewa viraka.
“Bunge limeacha mawazo ya wananchi na kuingia katika mikakati na
misimamo yao, walioona rasimu yetu siyo, watatoka bungeni watakutana
nasi mitaani, tutatetea maoni ya wananchi na wao watoke waje kutetea
mawazo yao,” alisema.
Jaji Warioba, alitoa mfano wa mambo ya msingi yaliyotokana na maoni
ya wananchi, yakaondolewa na BMK kuwa ni maadili, tunu za taifa,
mgawanyiko wa madaraka, miiko ya uongozi na Muungano.
MAADILI
Jaji Warioba, alisema wananchi waliotoa maoni walisisitiza masuala
yanayohusu maadili kwa taifa yaingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini hali
hiyo haikukubalika kwa BMK.
Kadhalika, alisema tunu za Taifa ambazo ni utu, uzalendo,
uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa zilizopendekezwa
na wananchi, rasimu hiyo ya bunge imezipunguza na kubaki nne tu.
Alizitaja zilizowasilishwa na rasimu ya bunge kuwa ni lugha ya Kiswahili, muungano, utu na udugu na amani na utulivu.
“Tunu za taifa zilizopendekezwa na wananchi, na siyo vyama vya
siasa wala tume zimeondolewa, Bunge linasema eti ni hiyo ni misingi ya
utawala,” alisema.
Aliongeza, “mimi siwaelewi kabisa kusema hizo siyo tunu za kitaifa, siwaelewi kabisa,” alisema.
Alisema, sura ya tatu ya rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume yake, ilihusu miiko ya uongozi.
Jaji Warioba, alisema sura hiyo ilieleza kuwa kiongozi wa umma
hapaswi kuwa na akaunti ya benki nje ya nchi na kutangaza mali na madeni
yake.
Pia, ilieleza kiongozi huyo anapaswa kuwasilisha kwenye ofisi za
umma zawadi anazopewa, kutotumia mali za umma kwa mambo binafsi,
kukomesha rushwa na ufisadi.
Alisema, miiko ya uongozi ilifanikisha kukabiliana na kadhia kama Ufilipino, Kenya, Namibia na Afrika Kusini.
“Tunajua ufisadi na rushwa ndiyo chanzo cha hayo yote, watu
wanapewa zawadi wanasaini mikataba ya hovyo, lakini tunapokuwa na miiko
yeyote atakayebainika amepokea zawadi au ana akaunti nje ya nchi
atawajibishwa… kwenye haya wameniita mimi ni shida,” alisema.
MADARAKA YA NCHI
Jaji Warioba, alisema wananchi walipendekeza kumuondoa Mwakilishi
asiyewajibika kwao, kuwapo ukomo wa ubunge na muundo wa serikali tatu,
lakini vimeondolewa na BMK.
“Wananchi walisema baadhi ya wabunge ni watalii kwenye majimbo yao,
wakataka wapate mamlaka ya kuwaondoa, cha ajabu wenyewe wamejipa
mamlaka ya kumfukuza mbunge asiyeshiriki kikao kimoja, na vyama vya
siasa vimejipa madaraka ya kuwaondoa wabunge wao, kwa nini mwananchi
anyimwe hili,” alihoji.
MGAWANYO WA MADARAKA
Alisema, Tume ilipendekeza kuwa kutokana na mwingiliano uliopo kati
ya Bunge na Serikali, ipo haja ya kuwapo mgawanyo wa madaraka kwenye
Katiba Mpya.
Alitoa mfano namna ushawishi wa Rais ulivyofanikishwa kurejeshwa
bungeni kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kukutana na viongozi
wa upinzani.
Aliongeza, “hata sasa, wakati rasimu yao inasema Katiba itaitwa ya
mwaka 2014, Rais anasema haiwezi kupatikana mwaka huu hadi 2016. Huu ni
muingiliano wa madaraka, ndio maana tume tuliona kila mhimili
ujitegemee.”
MUUNGANO
Jaji Warioba, alisema muundo wa serikali tatu ulipendekezwa na
wananchi na kwamba ndani ya Tume, kila mjumbe alikuwa na maoni yake.
“Mfano Baregu (Profesa Mwesiga Baregu) alitaka serikali mbili,
Joseph Butiku alitaka moja, Awadhi Said alikuwa muumini wa Muungano wa
mkataba, mimi ni serikali mbili kwenda moja,” alisema.
AZIPONDA KURA ZA MTANDAO
Jaji Warioba, alisema pamoja na kasoro iliyopo kupigia kura ibara
badala ya sura za rasimu ya Katiba inayopendekezwa, alipinga pia
utaratibu wa kuruhusu wajumbe wasiokuwapo bungeni kupiga kura.
“Kusaka kura kwa mtandao hakuwezi kutuletea Katiba ya maridhiano na
mimi nimeanza kukata tamaa, ninachoona mchakato huu utarudiwa mara
baada ya kupatikana kwa Rais mpya,” alisema na kuongeza:
LHRC BILA DK. MVUNGI
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema
endapo angekuwapo Dk. Mvungi, angeshangaa kuona maslahi ya taifa
yanatupwa na yale ya itikadi yanapewa kipaumbele.
Pia, alisema angeshangaa kuondolewa kwa vipengele kama kuwajibishwa
wabunge, ukomo wao na jinsi mchakato ulivyokiuka maoni ya wananchi.
Mjane wa Dk. Mvungi, Anna Mvungi, alisema baada ya kuteuliwa katika
tume, moja ya kauli zake (Dk. Mvungi) ilikuwa ni ‘nimetimiza nia
yangu’.
Mwenyekiti wa ukoo wa Mvungi, Adrian Mvungi, aliiasa LHRC kuondokana na woga na kuendeleza mapambano ya kutetea haki za watu.
Mmoja wa wahariri wa kitabu hicho, Profesa Chris Maina, alisema Dk.
Mvungi alikuwa ni Profesa kutokana na makala 20 alizoziandika kwa
wananchi na shauri kuhusu wanyonge na matatizo wanayoyapata. Kuhusu Tume
ya Warioba, alisema pamoja na `madongo’ wanayoyapa wamekuwa imara
kutokana na yote waliyosimamia waliyaamini.
“Jinsi tunavyopata vioja vya Dodoma tunazidi kuvumbua ubora wa tume
hii, wananchi wanajua mchele na pumba historia haifutwi na FFU,”
alisema.
Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia, alisema kuna
mazungumzo yanayoendelea yakivihusisha vyama vya siasa hususani vyenye
wabunge, ili kuinusuru Katiba Mpya.
“Yapo mazungumzo yanayoendelea yanahusisha vyama vyote vyenye
wawakilishi bungeni CCM, Chadema na NCCR-Mageuzi, tunataka Tanzania
isifike mahali tukamwaga damu kwa sababu ya ubinafsi wa watu wachache,”
alisema.
KITABU CHA DK. MVUNGI
Katika kitabu hicho zipo makala mbalimbali za wanataaluma, familia
na wanafunzi na walimu wake, wananchi na wanahabari ambazo zimemuelezea
jinsi alivyofanya kazi za utetezi wa wanyonge.
Kitabu hicho ambacho kimepambwa na picha 157 kina sura kumi ambazo
waandishi wake wametumia lugha mbalimbali kufikisha ujumbe ambazo ni
Kiswahili, Kingereza, Kijerumani na Kipare kilichokuwa lugha ya Dk.
Mvungi.
CHANZO:
NIPASHE

Awasubiri 'akina Sitta' wajieleze kwa wananchi
Post a Comment