Baba amuondoa Manyika Simba


Kipa chipukizi wa Simba, Peter Manyika, Manyika Peter.
Na Said Ally
BABA mzazi wa kipa chipukizi wa Simba, Peter Manyika, Manyika Peter, ameweka wazi kuwa anafurahia kuona mwanaye akiwa na maendeleo mazuri lakini akaenda mbele zaidi na kusema kuwa anajipanga kumfanyia mipango baadaye atakapokuwa tayari aende nje ya nchi akacheze soka la kulipwa.

Mzazi huyo ambaye alikuwa kipa maarufu enzi zake akizidakia Yanga, Sigara na Taifa Stars, amesema kuwa atafurahia zaidi akiona mwanaye anacheza soka na kufanikiwa zaidi kuliko yeye.
Manyika ambaye mara ya mwisho alikuwa kocha wa makipa katika timu ya Seeb FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Falme za Kiarabu, alijijengea umaarufu kutokana na kuwa kipa mwenye mbwembwe awapo langoni huku akivaa kofia, ameliambia gazeti hili kuwa ana imani kama mwanaye akiendelea kujituma basi atafika mbali.
Amesisitiza kuwa anachofanya kwa sasa ni kuandaa mipango ya kumfanya mtoto wake huyo kupiga hatua zaidi kwa kucheza soka la kimataifa ikiwa ni tofauti na yeye ambaye  mimi nilipoishia katika maisha yangu ya soka.
“Unajua japo bado ni mdogo lakini tayari ameanza kuonyesha kuwa ana kila sifa ya kucheza soka la kimataifa kutokana na mafundisho mbalimbali niliyokuwa nikimpa kipindi cha nyuma na ambayo anapatiwa na makocha wake wa sasa,” alisema Manyika baba.
Manyika mdogo amepata umaarufu baada ya kucheza kwa kiwango cha juu katika mechi dhidi ya Yanga, Jumamosi iliyopita na kuweka rekodi ya kuwa kipa mdogo zaidi kuwahi kucheza katika mechi ya wapinzani wao, ambapo kwa sasa ana umri wa miaka 18.

Post a Comment

Previous Post Next Post