
CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimembana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), kikimtaka aweke bayana vyama vya siasa
ambavyo havijakaguliwa hesabu zake na aeleze lini vitakaguliwa.
Shinikizo
la CHADEMA linakuja siku chache baada ya Ofisi ya CAG, kushindwa kutaja
chama cha siasa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(PAC), alichodai hakijakamilika kukaguliwa kutokana na kushindwa
kufanya nacho vikao.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha
na Utawala wa CHADEMA, Anthony Komu, alisema CAG alitoa kauli bungeni
kwamba si vyama vyote vimekaguliwa, kwamba kama sehemu ya jamii na chama
kinachopigania utawala wa sheria, wanamtaka aweke taarifa bayana.
"Hii ni
kwa sababu zilizotusukuma kupigania CAG kukagua vyama bado iko pale
pale. Mwaka 2005, CCM ilitumia fedha za EPA katika kampeni zake,
hatutaki utamaduni kama huo ujirudie tena kinyemela," alisema.
Alisisitiza
kuwa ni imani yao kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa, atachapisha ripoti
za vyama vyote kama sheria inavyomtaka kwa ajili ya rejea ya umma
unaolipa fedha hizo.
Akizungumzia
ukaguzi wa hesabu za CHADEMA, Komu alisema kuwa CAG ameainisha kasoro
kadhaa alizobaini na hivyo kutoa taarifa yake kwamba wanastahili kupewa
hati yenye mashaka 'Qualified opinion' ambayo tayari wamepatiwa.(P.T)
Komu,
alisema maeneo yote yaliyotajwa na CAG, yana maelezo ya kutosha na
kuitaka ofisi hiyo kusimamia sheria na kuweka hadharani mahesabu ya
vyama vingine kama ilivyofanya kwao.
Alisema
kuwa, Oktoba 5 mwaka huu, CHADEMA kilipokea taarifa rasmi ya ukaguzi wa
hesabu zinazoishia Juni 30 mwaka 2012, na ile ya Juni 30 mwaka 2013,
iliyoeleza kuwa chama hicho kina akaunti zaidi ya 200 wakihusisha zile
zinazoendeshwa na makao makuu, kanda, mikoa, wilaya, majimbo na hata
ngazi za chini.
Alisema
mashaka ya CAG, pia yamesimama katika salio la kufungia vitabu
kutohusisha akaunti zote zenye jina la chama na kwamba, inawezekana
akaunti hizo zilikuwa na fedha ambazo kinaweza kubadilisha kiasi
kilichotajwa.
Kwa
mujibu wa Komu, walimpatia CAG taarifa kuhusu akaunti hizo na ugumu wa
kuweza kuzipata kwa kile alichosema masharti ya benki yanaeleza kuwa,
wenye jukumu la kuendesha akaunti hizo ni viongozi wa ngazi husika.
Alisema
kuwa CHADEMA kimepokea taarifa hiyo ya CAG na kuichukua kama sehemu
muhimu ya kuboresha ujenzi wa chama kama taasisi ya kudumu na inayokua,
na kwamba changamoto zote alizoziainisha watazifanyia kazi.
Komu, alifafanua kuwa kwa mujibu wa wabunge wao, taarifa zilizopo zinaonyesha mpaka juzi ni CCM pekee ambayo haijakaguliwa.
Jumanne
wiki hii, Msaidizi wa CAG, Benja Majura, aliwasilisha taarifa ya ukaguzi
wa mahesabu kwa mwaka 2012/13 mbele ya PAC, akisema kuwa kati ya vyama
21 ni 12 tu ndivyo viliweza kupeleka mahesabu yake na kukaguliwa.
Kwamba
kati ya hivyo 12, kimoja wameshindwa kufikia hatua ya mwisho ya ukaguzi
kutokana na kukosa muda wa kufanya vikao kwa ajili ya shughuli hiyo.
Pamoja na
kubanwa akitaje chama hicho, Majura hakufanya hivyo, hatua iliyomfanya
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, kuingilia kati akiwataka wajumbe
wasubiri taarifa rasmi Oktoba 28 watakapokutana na msajili wa vyama.
Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/chadema-yamkaba-cag/
Post a Comment