Ndugu Waandishi wa Habari.
Yahusu Katiba Inayopendekezwa na Hatima ya Wasanii wa Tanzania
Utangulizi.
Fleva Inc Film Academy ni taasisi inayojihusisha na shughuli za ukuzaji wa sanaa nchini hasa kwa yale
masuala yanayohusu tasnia ya filamu hapa Tanzania, ni taasisi
inayofanya kazi na kutoa mafunzo ya uigizaji, uongozaji wa filamu au
tamthilia,matangazo ya biashara , uandishi wa michezo ya kuigiza ya
jukwaani,uhariri wa filamu pamoja na utayarisahji wa Filamu kwa ujumla.
Fleva Inc Film Academy ni taasisi
inayotambulika na mamlaka inayosimamia shughuli za sanaa na inapatikana
Manispaa ya Temeke hapa Mjini Dar es Salaam.
Malengo ya Fleva Inc Film Academy.
Fleva Inc Film Academy ina malengo na madhumuni yafuatayo;
- Kutoa Mafunzo yanayohusu tasnia ya filamu yenye ubora unaondana na mabadiliko ya ukuaji teknolojia duniani kote.hasa kwa fani za uigizaji michezo ya kuigiza na filamu, Kutoa mafunzo ya kuhariri filamu, michezo ya kuigiza pamoja na tamthilia .
- Kushirikiana na serikali,asasi zisizo za serikali,vikundi vya kijamii katika mambo mbalimbali yatayoweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kwa Wasanii wa Tanzania na jamii kwa ujumla.
Ndugu Waandishi
kama tunavyofahamu tasnia ya filamu nchini imepitia hatua mbalimbali
katika ukuaji wake ili kufikia maendeleo yanayoonekana sasa. Lakini
jitihada hizi zimefanywa na kada mbalimbali za kisekta zikijumlisha
serikali na taasisi zake pamoja na Wadau na Wabia mbalimbali pamoja na
Wasanii wenyewe wakishirikiana na taasisi zao.
Lakini pamoja na
changamoto nyingi zilizopatikana katika maendeleo ya tasnia ya filamu
hapa nchini na sanaa nyinginezo kwa ujumla bado serikali yetu
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete imejaribu
kufanya maboresho na au utungaji wa sheria na kanuni kadhaa
zitazowezesha kutoa miongozo iliyo sahihi katika kulinda , kutetea,
kusimamia na ukuzaji wa tasnia za sanaa za ufundi, sanaa za maonesho,
filamu na muziki, baadhi ya sheria hizo ni za hakimiliki na hakishiriki
ya 1999 inayosimamia haki bunifu za Wasanii, sheria ya TRA ya mwaka 2014
inayosimamia kodi za mauzo ya kazi za filamu na muziki pamoja na sheria
namba ya 4 ya mwaka 1976 inayosimamia michezo ya kuigiza ambazo kanuni
zake zilizinduliwa mwaka 2011 Mjini Musoma. Pamoja na jitihada hizo
kufanyika bado sekta ya sanaa haikupewa uzito unaostahili kwa sababu
ilionekana si eneo ambalo linaweza kuwa na mchango katika pato la Taifa
letu, yaani sanaa ilionekana ni kiburudisho kwa watu Fulani na umuhimu
wake ulikuwa katika matukio na hafla maalumu.
Ndugu Waandishi,
nachukua fursa hii kuipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni Vijana na
Michezo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na taasisi zao
ambazo zimepewa majukumu ya kusimamia kazi za Wasanii kwa namna moja au
tofauti, zikiwemo,BASATA, COSOTA,TRA na Bodi ya Filamu Tanzania na
matunda ya majukumu yao yanaonekana.
Pamoja na jitihada hizo za awali
Naipongeza Serikali ya Mh Rais Dkt Mrisho Jakaya Kikwete kuanzisha
mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ambapo katika mchakato huo makundi mbali mbali ya kijamii
yalishirikishwa kuanzia hatua ya Mwanzo mpaka katika uundwaji wa Bunge
Maalum la Katiba, Kutokana na hilo sisi tunaofanya kazi katika sekta ya
Sanaa tuliwakilishwa na Ndg Paul Mtenda ambaye ni Mwenyekiti wa Chama
cha Waongozaji wa Filamu na Michezo ya kuigiza Tanzania(TAFIDA).
Ndugu Waandishi wa Habari
mchakato wa Bunge Maalum la Katiba na majukumu yake yamekamilisha
historia muhimu kwa Taifa la Tanzania ambapo tarehe 8/10/2014 katika
Uwanja wa Jamhuri Dodoma Mwenyekiti wa Bunge hilo maalumu Mh Samuel
Sita na kamati zake walimkabidhi rasmi KATIBA INAYOPENDEKEZWA kwa Mh
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.
Ndugu Waandishi, mimi ni mmoja
kati ya Walioalikwa na Bunge kuhudhuria sherehe hizo nikiwa Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama cha Wahariri wa Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania
(TAFEA) na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Fleva Inc Film Academy na
nikiwa Katibu Mstaafu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),
nimeipitia Katiba inayopendekezwa na hasa vifungu vinavyohusu maslahi na
haki za Wasanii Tanzania.
Kutokana na hilo nalipongeza Bunge
Maalumu Katiba kwa kazi nzito walioifanya na hasa kuthamini na kuyapa
umuhimu madai ya Wasanii wa Tanzania kwa kuingiza mambo ya msingi
yanayohusu sekta ya Sanaa na hasa katika ulinzi wa haki bunifu za kazi
za Wasanii, usimamizi na uendelezaji wa sekta ya Sanaa,utafiti na
taaluma kwa ujumla ambazo zimeorodheswa katika Sura ya tano kifungu
namba 59(1 -3) na 3(a) – (f) ukurasa 47 – 48.
Ndugu Waandishi,Pamoja na mazuri
yaliyoorodheshwa katika vifungu hivyo bado kuna changamoto kubwa
inayoikabili sekta sanaa hasa muziki na filam, nalo ni tatizo la bei
katika soko la filamu limekua si lenye kueleweka, katika hili naweza
kusema kuwa thamani ya kazi za msanii wa filamu na muziki bado
hazijatazamwa inavyostaahili na hasa tukizingatia kwamba tunafanya kazi
kubwa katika mazingira magumu lakini bado tatizo la bei ya zao letu
haijatazamwa kwa kina.
Kwa sababu kama Wavuvi, Wafugaji,
na Wakulima watakua na mizania ya bei ya mazao yao kama ilivyotajwa
katika Katiba Inayopendekezwa Sasa Sura 3 (13)(2)d ukurasa 10-11, kwa
nini pia katika zao la filamu pasiwepo na utaratibu wa bei elekezi kama
ilivyo katika bidhaa za mafuta na sasa kwa wafugaji,Wakulima na wavuvi?.
Lakini jambo hili halijachelewa kwa sababu zipo mamlaka zinazoweza
kukaana Wadau wake ili kuliongelea na kulipatia ufumbuzi.
Hivyo basi naziomba taasisi za
BASATA, COSOTA, Bodi ya Filamu na Mashirikisho husika kulitazama kwa
kina kama wanataka kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa Wasanii wenyewe ili
wawezekulipia kodi kadhaa zinazowakabili.
Mwisho napenda kuwashawishi
Wasanii wa Tanzania kuchukua hatua madhubuti katika kutafuta fursa
mbalimbali za kuiendeleza tasnia ya Filamu na Sanaa kwa ujumla lakini
pia kuipitia katiba hii inayopendekezwa ili Waielewe na kujua yaliyomo
ndani kuliko kupiga kelele ambazo majibu yake tayari yamepatiwa
ufumbuzi.
Lakini pamoja na hayo ili kuleta
tija na matokeo chanya ya Katiba hii INAYOPENDEKEZWA itapokuwa tayari na
tunaiomba Serikali na hasa mamlaka zinazosimamia sekta za sanaa
kuhakikisha inasimamia taratibu zote zinazoelekeza wajibu wa Wasanii na
Watendaji wake ili kufanikisha malengo.
Hongera Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Hongera Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
Nawatakia kazi njema
PAMOJA TUILINDE NA KUIENDELEZA TASNIA YA FIAMU TANZANIA.
WILSON R. MAKUBI
MKURUGENZI MKUU
FLEVA INC FILM ACADEMY
Post a Comment