WINGA
machachari na kocha wa zamani wa Simba sc, Alhaj Abdallah Athumani Seif
‘King Abdallah Kibadeni Mputa’ amesema hataki tena presha ya kufundisha
klabu za ligi kuu soka Tanzania bara.
Akizungumza
katika mahojiano maalum na mtandao huu, Kibadeni aliyeiongoza Simba
mzunguko wa kwanza msimu uliopita kabla ya kurithiwa na Zdravko
Logarusic alisema anajenga akademi yake maeneo ya Chanika jijini Dar es
salaam ambapo atakuwa anafundisha soka vijana wadogo.
Akademi hiyo itakayojulikana kwa jina la ‘Kibadeni Soccer Academy’, KISA itakuwa inachukua vijana kutoka maeneo mbalimbali.
Kibadeni
mwenye rekodi ya pekee ya kufunga mabao matatu ‘Hat-trick’ katika mechi
ya watani wa jadi mwaka 1977 ambayo haijavunjwa mpaka leo alisema
amechoshwa na dharau za baadhi ya wadau wa michezo hasa wanaposema
hajasomea mpira wakati alikwenda Ujerumani na Brazil kupiga shule.
Akizungumzia
mechi ya watani wa jadi Oktoba 18 mwaka huu, Kibadeni mwenye rekodi ya
pekee Afrika mashariki na kati kwa kuifikisha Simba fainali ya kombe la
CAF mwaka 1993 alisema ni mechi ngumu, timu itakayocheza kwa umakini
itaweza kushinda, lakini hawezi kutabiri matokeo.
Hata
hivyo alishangazwa na sare tatu walizopata Simba katika mechi tatu za
kwanza akisema haoni sababu ya matokeo hayo kwasababu wamesajili
wachezaji wakali.
“Sielewi
kinachowakumba, kwa uongozi thabiti walionao, usajili waliofanya,
nashangaa kuona wanapata matokeo kama haya. Nadhani kuna sehemu
wamekosea, labda kuna watu wanawaombea dua mbaya kwasasa waliwafanyia
vitu vibaya”. Alisema Kibadeni.
Post a Comment