
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mke wa Rais wa China Mama Peng Liyuan.
Na Anna Nkinda – Beijing, China
Mke
wa Rais wa China Mama Peng Liyuan ameahidi kutoa vifaa vya shule
vikiwemo vya maabara pamoja na vitabu kwa ajili ya shule ya Sekondari ya
WAMA-Nakayama ili wanafunzi hao waweze kusoma vizuri masomo ya
sayansi.
Mama
Liyuan aliitoa ahadi hiyo jana wakati akiongea na mke wa Rais Mama
Salma Kikwete katika ukumbi maarufu wa watu (Great hall of the People)
uliopo mjini Beijing.
“Nina
mapenzi na Taasisi ya WAMA, nakupongeza kwa kazi unayoifanya ukiwa Mke
wa Rais ya kuwainua wanawake kiuchumi na kuwasaidia watoto wa kike
ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi ambao nao
wanapata elimu sawa na watoto wengine”.
Najua
kitaaluma wewe ni mwalimu na unapenda shule mwaka huu nitakuunga mkono
zaidi katika masuala ya shule, hii itawasaidia wanafunzi kusoma
vizuri. Pia nitakuwa na ushirikiano endelevu na Taasisi ya WAMA”,
alisema Mama Liyuan.
Kwa
upande wake Mama Kikwete alishukuru kwa msaada huo na kusema kila
kwenye maendeleo changamoto hazikosekani alizitaja changamoto
zinazoikabili sekta ya elimu ambazo ni upungufu wa maabara, kutokuwepo
kwa wataalamu wa maabara na walimu wa masomo ya sayansi wa kutosha.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema katika upande wa elimu Serikali kwa kushirikiana na
wananchi wamejitahidi kujenga shule nyingi za Sekondari lakini bado
kuna upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi , kutokuwa na maabara za
kutosha, kutokuwa na vifaa vya maabara na upungufu wa wataalamu wa
maabara .
“Ninaomba
kuwe na ubadilishanaji wa ujuzi wa kazi (Exchange Program) kwa walimu
wetu wa nchi hizi mbili hii itawasaidia kupata utaalamu zaidi katika
fani zao na kutoa mfano wa wataalamu wa maabara ambao wakija nchini
watasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya sayansi
kwa njia ya vitendo”, alisema Mama Kikwete.
Shule
hiyo ambayo inamilikiwa na Taasisi ya WAMA wanafunzi wake ni watoto wa
kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi kutoka
mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani iko kijiji cha Nyamisati wilaya
ya Rufiji mkoani Pwani.
Hii
ni mara ya pili kwa Mama Liyuan kuiunga mkono Taasisi ya WAMA ambapo
mwaka 2013 alipotembelea nchini alitoa Yuan milioni moja sawasawa na
shilingi milioni 250 za kitanzania na mabegi ya shule 100 kwa ajili ya
wanafunzi wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama na vyerehani 20 kwa
ajili ya Umoja wa Vikundi vya WAMA (UVIMA).
Mama Kikwete ameambatana na mumewe Rais Prof. Jakaya Mrisho Kikwete nchini China kwa ziara ya kikazi ya siku sita.
Post a Comment