SALAM ZA JUMUIYA YA WAISLAM AHMDIYYA KWA VIONGOZI WA DINI WA MKOA WA DSM

Ndugu Wapendwa wajumbe wa amani,
Assalaamu Alaikum Warahmatullaahi Wabarakaatuh (Amani iwe juu yenu na Rehema za Allah na Baraka Zake).
Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Morogoro inachukua fursa hii kutoa pongezi za dhati kwenu kwa juhudi yenu tukufu ya kustawisha amani nchini kwa kuungana pamoja watu wa dini na madhehebu mbali mbali kwenye hafla za michezo kwa nia njema kabisa ya kudumisha amani na upendo kwa watu wa dini na madhehebu tofauti.
Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya i pamoja nanyi katika juhudi hizo na tumefurahishwa nazo sana kwa sababu sisi tumekuwa pia ni wadau wa amani na upendo duniani kote kutokana na juhudi mbali mbali tunazoendelea kuzifanya duniani kote zikiongozwa na na Kiongozi wetu Mkuu Duniani Hadhrat Khalifatul Masih atba ambaye ameshazunguka sehemu mbali mbali duniani na kuyahutubia mabunge ya nchi mbali mbali akihamasisha amani, upendo na uadilifu.(P.T)
Ndugu zetu wapendwa! Si jambo la kufichika kwamba dunia leo inapita katika nyakati za ghasia sana. Mgogoro wa kiuchumi duniani unaendelea, karibuni kila wiki, kudhihirisha hatari mpya na za kutisha. Mfanano wa wakati wa kabla ya vita vikuu vya pili vya dunia unaendelea kutajwa na inaonekana dhahiri kwamba matukio yanaielekeza dunia kwa hatua zisizozuilika kuelekea kwenye vita kuu ya tatu ya kutisha ya dunia.
Kuna hisia iliyokithiri kwamba mambo yanaenda kwa kasi nje ya udhibiti na watu wanamtafuta mtu wa kuingilia kati na kutoa mwongozo madhubuti na imara wanaoweza kuuamini na kupenya hadi ndani ya mioyo na akili zao na kuwapa tumaini kuwa kuna njia iwezayo kuongoza kwenye amani. Matokeo yamadhara ya vita vya kinyuklia ni yenye kutisha kiasi hiki kwamba hakuna yeyote anayediriki hata kuyafikiria.
Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Duniani, Hadhrat Mirza Masroor Ahmad atba, Kwa miaka kadhaa iliyopita, sawa na mambo yalivyojitokeza, amekuwa hana woga wa kuitangazia dunia hali ya mambo iendavyo, sio kwa lengo la kutisha, bali kwa nia ya kuwaandaa wanadamu waweze kutafakari kwa kina, kuwa dunia imefikia wapi na namna gani yaweza kuepuka janga na kuelekea kwenye njia ya amani na usalama kwa ajili ya watu wote waishio ndani ya kijiji hiki dunia.
Khalifa Mtukufu alitangaza moja kwa moja kuwa njia pekee ya kuhakikisha amani inastawi na kudumu, ni kwa dunia kushikamana na njia za unyenyekevu na uadilifu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu na kujitupa. Mtu awe na ubinadamu, wenye nguvu wawatendee walio dhaifu kwa heshima, taadhima na uadilifu.
Na wale walio dhaifu na masikini waonyeshe shukrani na kushikamana na njia za ukweli na utawa. Na wote waelekee kwa Muumba wao kwa unyenyekevu na uaminifu kamili.
Mara kwa mara, Khalifa Mtukufu ameendelea kuwakumbusha watu, mmoja mmoja na kwa ujumla, kwamba njia ya kuliepuka shimo la maangamio ni kwa mataifa kuufanya uadilifu kuwa hitajio kamili la matendeano kati yao. Hata kama kuna uadui kati yao, bado wanahitajika kufanyiana uadilifu, kwa sababu historia imetufundisha kwamba hii ndio njia pekee ya kuondoa athari zote za chuki za siku zijazo na hivyo kujenga amani ya kudumu.
Hili ni fundisho la Kurani Tukufu alilolisisitiza ndani ya barua zake alizowaandikia viongozi mbali mbali wa dunia kwamba:
Na uadui wa watu usiwashawishini, kwa sababu waliwazuilieni Msikiti uliotukuzwa, ya kwamba mruke mipaka. Na saidianeni katika wema na utawa, wala msisaidiane katika dhambi na uasi. Na mcheni Allah; hakika Allah ni mkali wa kuadhibu. ( Sura 5: 3).
Katika barua aliyomuandikia Waziri Mkuu wa Israeli, Khalifa Mtukufu aliandika:
"Ni ombi langu kwako kuwa badala ya kuiongoza dunia kwenye mshiko wa vita kuu ya dunia, fanya juhudi za juu kabisa za kuiokoa dunia katika janga la kidunia. Badala ya kuitatua migogoro kwa nguvu, jaribu kuitatua kwa njia ya mazungumzo ili tuweze kuwapa zawadi vizazi vyetu vijavyo za mustakbali wenye kung'aa, badala ya kuwazawadia ulemavu na kasoro.
Kwa Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Khalifa Mtukufu alionya:
Hivi sasa kuna wasiwasi na fadhaa kubwa duniani. Katika baadhi ya sehemu, vita ndogo ndogo zimeibuka, wakati katika sehemu zingine mataifa makubwa yanajifanya ni kama yenye kutaka kuleta amani. Kila nchi inajishughulisha katika aidha kuzisaidia au kuzipinga nchi zingine, lakini mahitajio ya uadilifu hayatekelezwi. Ni kwa masikitiko makubwa kwamba kama tuzitazame hali za kidunia hivi sasa, tunakuta kwamba msingi wa vita nyingine ya dunia tayari umeshajengwa.
Kwa raisi Obama, Huzur alisema:
Kama vile wote tujuavyo, sababu kuu zilizoelekeza kwenye vita kuu ya pili ya dunia ilikuwa ni kushindwa kwa Umoja wa Mataifa wa wakati huo (League of Nations), na msukosuko wa kiuchumi ulioanza mnamo mwaka 1932. Leo wachumi waliobobea wanasema kwamba kuna mifanano mingi kati ya msukosuko wa sasa wa kiuchumi na ule wa mwaka 1932. Tunaona kwamba matatizo ya kisiasa na kiuchumi yameongoza tena kwenye vita kati ya mataifa madogo. Na migogoro ya ndani na hali ya kutoridhika imekithiri ndani ya nchi hizo. Hii hatimae itaongoza kwenye baadhi ya nguvu fulani kushika mamlaka ya nchi ambayo itatuongoza kwenye vita kuu ya dunia.
Ikiwa migogoro katika nchi ndogo ndogo haiwezi kutatuliwa kwa njia za kisiasa na mazungumzo, basi itaelekeza kwenye kuundika duniani kwa mashirika na makundi mapya. Huo utakuwa ni utangulizi wa ulipukaji wa vita kuu ya tatu ya dunia. Hivyo ninaamini kwamba, sasa, badala ya kuelekeza mwelekeo kwenye maendeleo ya dunia, ni muhimu zaidi, na kwa hakika ni lazima tuongeze juhudi zetu kwa kasi sana katika kuiokoa dunia na maangamio haya.
Kuna haja ya haraka kwa mwanadamu kumtambua Mungu wake Aliye mmoja, Aliye Muumba wetu, kwa kuwa hii ndio dhamana ya pekee ya kusalimika kwa wanadamu, waila dunia itaendelea kwa kasi kuelekea kwenye kujiangamiza.
Kwa Waziri Mkuu Wen Jiabao, wa Jamhuri ya watu wa China, Huzur aliandika:
"Ni dua yangu kwamba viongozi wa dunia watende kwa busara na wasiruhusu uadui kati ya mataifa na watu kwa kiwango kidogo kulipuka na kuwa mgogoro wa dunia nzima."
Na kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Huzur aliandika:
"Ni ombi langu kwamba katika kila kiwango na kila upande ni lazima tujitahidi kwa kiwango cha juu kabisa kuizima mioto ya chuki. Ikiwa tu tutafanikiwa katika juhudi hii, ndipo tutakapoweza kuwapa dhamana vizazi vijavyo ya mustakbali ung'aao. Hata hivyo, ikiwa tutashindwa katika jukumu hili, kusiwe tena na shaka yoyote ndani ya akili zetu kwamba kutokana na matokeo ya vita vya kinyuklia, kila mahali vizazi vyetu vijavyo vitalazimika kukabiliana na matokeo yenye kutisha yaliyosababishwa na matendo yetu na kamwe hawatawasamehe wazee wao kwa kuiongoza dunia kwenye janga la kidunia.
Ninakukumbusha tena kwamba Uingereza ni nchi mojawapo kati ya nchi zenye kuweza kutoa athari, bali inayo athari, kwa nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea. Waweza kuiongoza dunia hii kama unataka, kwa kuyatimiza mahitajio ya usawa na uadilifu. Hivyo Uingereza na nchi nyingine zenye nguvu ni lazima zitekeleze majukumu yao katika kuistawisha amani ya dunia. Mwenyezi Mungu Akuwezeshe wewe na viongozi wengine duniani kuuelewa ujumbe huu. Amin."
Ni ombi letu la dhati kwamba mwongozo huu uthibitike kuwa chimbuko la mwongozo kwa mwanadamu katika wakati huu wa hatari kubwa ili kwa kuzitekeleza kanuni za uadilifu na unyenyekevu na kwa kumuelekea Mwenyezi Mungu, mwanadamu abarikiwe na amani ya kudumu. (Amin).
Mwenyezi Mungu Aibariki nchi yetu Tanzania iwe mfano wa kuigwa na mataifa mengine katika ustawishaji wa haki, uadilifu, upendo na amani. Mwenyezi Mungu Awabariki wote wale, ambao kwa namna moja au nyingine, wanajitahidi katika ustawishaji wa malengo haya.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Dunia yetu. Amin.
Nimekuambatanishieni vipeperushi vinavyoonyesha jinsi Jumuiya yetu ilivyo pamoja nanyi katika jitihada hii takatifu tukitaraji mtakuwa nasi katika kuiombea juhudi hii mafanikio.
Wassalaam
Sheikh Asif Mahmud Butt
...............................................................................
Mbashiri wa Mkoa
Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya, Morogoro.

Post a Comment

Previous Post Next Post